Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zozote za kijeshi Ukraine zinahatarisha haki za binadamu:OHCHR

Watu wakiwa nje ya jengo la makazi lililoharibiwa na makombora huko Marinka, Ukrainia.
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Watu wakiwa nje ya jengo la makazi lililoharibiwa na makombora huko Marinka, Ukrainia.

Hatua zozote za kijeshi Ukraine zinahatarisha haki za binadamu:OHCHR

Amani na Usalama

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet leo ameongeza sauti yake katika hali inayoendelea kuwa tete nchini Ukraine. Kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva Uswi Bi.

Bachelet amesema “Kufuatia uamuzi uliotangazwa na Rais wa Shirikisho la Urusi jana usiku kuhusu Ukraine, nina wasiwasi mkubwa kwamba ongezeko lolote la hatua za kijeshi huleta hatari kubwa ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu pamoja na ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.” 

Tweet URL

Ameongeza kuwa “Katika wakati huu muhimu, kipaumbele, juu ya yote, lazima kiwe kuzuia kuongezeka zaidi kwa machafuko, na kuzuia vifo vya raia, kuhama na uharibifu wa miundombinu ya raia.”  

Kamishina mkuu amezisihi pande zote kukumbuka wajibu wao kimataifa wa kudumisha amani na sio vita “Natoa wito kwa pande zote kusitisha uhasama na kuandaa njia ya mazungumzo badala ya kuweka mazingira ya kuleta vurugu zaidi.” 

Amehitimisha taarifa yake kwa kusisitiza kuwa ofisi ya haki za binadamu itaendelea kufuatilia kwa karibu pande zote husika kwenye mtastari wa makabiliano huko Mashariki mwa Ukraine. 

Baraza kuu kukutana kujadili hali hiyo 

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid amesema “Kabla ya mkutano wa Baraza Kuu kesho Jumatano utakaomulika hali ya Ukraine, natoa wito kwa wahusika kuzidisha mazungumzo na kutuliza mwelekeo wa sasa wa machafuko kupitia mazungumzo. Kuzingatia kikamilifu katiba ya Umoja wa Mataifa, madhumuni yake na kanuni zake na hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha amani ya kudumu."