Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yahimiza usawa wa matibabu ya saratani kwa watoto barani Ulaya

Mtoto mwenye saratani akiwa katika Taasisi ya Taifa ya Saratani ya Colombia.
PAHO/David Spitz
Mtoto mwenye saratani akiwa katika Taasisi ya Taifa ya Saratani ya Colombia.

WHO yahimiza usawa wa matibabu ya saratani kwa watoto barani Ulaya

Afya

Ikiwa leo ni siku ya Kimataifa ya saratani ya utotoni, 15 Februari 2022, Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO barani ulaya limetoa ripoti inayoonesha kukosekana kwa usawa baina ya nchi na nchi kwa suala la saratani ya watoto katika Kanda ya Ulaya ya WHO.

Dkt. Nino Berdzuli, Mkurugenzi, Idara ya mipango ya afya za nchi wa WHO  barani humo amesema wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo kuwa katika nchi zenye kipato cha juu saratani sio hukumu ya kifo kwa watoto na vijana tena lakini hali ni tofauti kwa zile za kipato cha chini.

“Miongo michache iliyopita tumeona maendeleo makubwa katika kuweza kuikabili saratani ya utotoni, na leo, tunaweza kuponya hadi asilimia 80 ya saratani za utotoni kutokana na teknolojia ya ubunifu, na kuboresha utambuzi na matibabu.”

Naye Marilys Corbex, Afisa Mkuu wa masuala ya kiufundi wa WHO barani Ulaya amesema mbali na kusherehekea mafanikio hayo lakini maendeleo haya hayajafikiwa kwa usawa katika nchi zote na kwamba sehemu kubwa ya maelfu ya watoto wanaopatikana na saratani kila mwaka bado wanakufa.

“Kiwango cha vifo ni kati ya asilimia 9 hadi asilimia 57% katika baadhi ya nchi ndani ya bara hili. Tofauti hii kubwa inawakilisha maelfu ya ukosefu wa usawa miongoni mwa watu wetu walio katika mazingira magumu zaidi katika Kanda, ambayo tunahitaji kushughulikia kwa haraka,” alisema Corex

Corex ameongeza kuwa “Ni muhimu kutambua kwamba, ikiwa tofauti katika viwango vya kuishi ni muhimu kati ya nchi za kipato cha juu na cha chini lakini pia, zinaweza pia kutofautiana sana ndani ya nchi moja katika makundi ya kijamii na kiuchumi au hata kulingana na jinsia".

Ripoti hii muhimu imeonesha taarifa ya tafiti kutoka nchi 53 wanachama wa Kanda ya Ulaya ya WHO, kutoka Iceland upande wa magharibi hadi Kyrgyzstan upande wa mashariki ambapo kati ya nchi hizo 34 yanachukuliwa kuwa nchi za kipato cha juu, nchi 14 za kipato cha kati na nchi 5 za kipato cha chini.

Maendeleo ya kukabiliana na saratani kwa watoto

Ripoti hiyo inaonesha maendeleo chanya kuwa kiwango cha jumla cha kuishi kwa miaka 5 kwa watoto walio na saratani kiliongezeka kutoka asilimia 30 katika miaka ya 1960 hadi zaidi ya asilimia 80 katika siku za hivi karibuni, mafanikio ambayo yamechangiwa na sababu tofauti, pamoja na dawa bora, uchunguzi na upatikanaji wa huduma.

Mkurugenzi, Idara ya mipango ya Afya za Nchi wa WHO  Dkt. Berdzuli ametoa wito kwa watunga sera akihimiza umuhimu wa kila nchi kufanya bidii ili kupunguza mapungufu ambayo bado yapo katika matunzo na matibabu ya saratani ya watoto, ili kila mtoto aliye na saratani apate nafasi bora zaidi ya maisha.

Mifano ya hadithi za kutokuwepo na usawa ni pamoja na pale ambapo kliniki hazikuwa na dawa za kutosha na wazazi walilazimika kutafuta dawa wenyewe, ukosefu wa ufahamu wa saratani ya utotoni na ufahamu wa itifaki za matibabu ya saratani ulimaanisha kuchelewa kutambua kuwa mtoto ana saratani kutokana na ukosefu wa vifaa vya watoto, watoto wenye saratani walitibiwa katika vituo vya watu wazima, na ambapo michango kwa mashirika ambayo hutoa dawa iliathiriwa na coronavirus">COVID-19 na familia zilikosa pesa za kununulia dawa zenyewe.