Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa ufupi: Maji; Gaza; Saratani ya utotoni

Mwanamke akichota maji kutoka kwa chanzo kilichotengenezwa na UNICEF katika jimbo la Kasai, DR Congo.
© UNICEF/Gwenn Dubourthoumi
Mwanamke akichota maji kutoka kwa chanzo kilichotengenezwa na UNICEF katika jimbo la Kasai, DR Congo.

Habari kwa ufupi: Maji; Gaza; Saratani ya utotoni

Msaada wa Kibinadamu

Leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani limetoa muongozo mpya na nyenzo za kuboresha usambazaji mdogo wa maji. Mwongozo huo wa “ubora wa maji ya kunywa: usambazaji mdogo wa maji”, na vipengele vinavyohusiana vya ukaguzi wa usafi, unalenga kuboresha ubora wa maji hususan ya kunywa, kujenga utoaji wa huduma thabiti zaidi, na kupambana na kuongezeka kwa magonjwa katika jamii zilizo hatarini na zenye uhaba wa rasilimali hiyo muhimu.

WHO inasema ingawa hatua zimepigwa lakini bado kuna watu bilioni 2.2 duniani kote ambao wanakosa rasilimali hiyo muhimu kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo za mwaka 2022 na wengi wao wanaishi vijijini.

Umeme Gaza

Gaza, Leo wakati changamoto ya kukatika kwa umeme ikiendelea katika ukanda huo na kwingineko pia mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema mashambulizi ya anga yakiendelea kulenga mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah na kusambaa kwa ripoti kwamba vikosi vya Israel vimefanya operesheni ya kijeshi ndani ya jengo la hospitali ya Nasser, wasiwasi juu ya uwezekano wa uvamizi wa ardhini wa mji huo wa mpakani wenye wakazi wengi unazidi kuongezeka.

Jeshi la Israel lilithibitisha leo Alhamisi katika ujumbe wa mtandao wa X kwamba vikosi vyake maalum vilifanya kile walichokiita "operesheni sahihi na ndogo" ndani ya hospitali ya Nasser kusini mwa Gaza, ambacho kituo kikubwa zaidi cha afya kinachofanya kazi katika eneo hilo. 

Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP katika eneo linalokaliwa la Gaza Matthew Hollingworth ameonya kwamba mashambulizi Rafah itakuwa janga kubwa la kibinadamu kwani, “Rafah yenyewe imefurika watu pomoni, Zaidi ya watu milioni moja na nusu wako katika mji ambao tayari ulikuwa ni mdogo. Kila kona ambayo mtu anaweza kujenga hema imetumika kujenga hema.”

Saratani ya utotoni 

Na leo ni siku ya kimataifa ya saratani ya utotoni ambapo mwaka huu shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO linajikita na jukumu muhimu la wazazi, madaktari wa familia na madaktari wa watoto katika kubaini mapema saratani hiyo ya utotoni.

Kwa mujibu wa WHO hakuna aliye tayari kuwekeza kila kitu kwa mustakbali wa watoto kuliko wazazi. Hivyo shirika hilo limesisitiza kwamba kwa kutambua mapema ishara na dalili za aina za saratani na kuchukua hatua muafaka kunaweza kuokoa maisha ya m toto. Duniani kote WHO inasema watoto zaidi ya 1000 wanabainika kuwa na saratani kila siku.