Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame waongeza zahma ya kutokuwa na uhakika wa chakula Pembe ya Afrika:FAO

Mama wa jamii ya rendile akiwa na watoto wake Marsabit Kaskazini Mashariki mwa Kenya, baada ya kupokea msaada wa chakula (Marsabit)
Khoboso HarguraAdichareh/KPL
Mama wa jamii ya rendile akiwa na watoto wake Marsabit Kaskazini Mashariki mwa Kenya, baada ya kupokea msaada wa chakula (Marsabit)

Ukame waongeza zahma ya kutokuwa na uhakika wa chakula Pembe ya Afrika:FAO

Tabianchi na mazingira

Ukame wa muda mrefu ulioghubika eneo la Pembe ya Afrika ikiwemo nchini Kenya unachochea hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula limeonya shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO na kuongeza kuwa sasa watu milioni 12 hadi milioni 14 katika eneo hilo wako katika hatari wakati huu mazao yao yakiendelea kukauka na mifugo kudhoofika.

Katika eneo la Marsabiti nchini Kenya picha za video ya shirika la FAO zilizopigwa kutoka angani zinadhihirisha hali ya ukeme iliyotamalaki. Hali hiyo imewafanya maafisa wa ngazi ya juu wa FAO kufunga safari na kwenda kwenye kauti hiyo ya Marsabiti na pia ya Isiolo  Kaskazini mwa nchi hiyo ambako kumeathirika zaidi na ukame. 

Lengo lao likiwa kuzungumza na jamii kuhusu hali halisi ya ukame na hatua zinazochukuliwa na FAO kukabiliana na ukame huo. 

Ziara yayo imehusisha maafisa wanne akiwemo naibu mkurugenzi mkuu wa FAO Beth Bechdol ambaye anasema,“ni fursa kwetu kuelewa kazi ambayo tumeifanya kwa mafanikio ya kutokomeza nzige wa jangwani. Lakini sasa la msingi zaidi ni kutathimini changamoto ambazo zinaikabili nchi kutokana na ukame unaoendelea kama mabadiliko ya hali ya hewa na la msingi zaidi athari zinazoikabili sekta ya mifugo hususani wakulima na wafugaji wa vijijini ambao wameathirika zaidi na changamoto hizi.”  

Hivi sasa FAO inahitaji haraka dola milioni 130 ili kutoa msaada unaohitajika kwa jamii zilizoathirika zaidi katika nchi tatu za Pembe ya Afrika ikiwemo Kenya.  

Kwa wafugaji FAO inalenga kufikisha lishe na chakula cha mifugo, huduma za afya ya mifugo,  lita 10,000 za maji na kukarabati visima vinavyotumia nishati ya jua au sola. 

Na kwa familia za wakulima inatarajia kugawa mbegu zinazokomaa haraka za ulezi, mahidi, mbaazi , maharagwe na mboga za majani.