Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya maisha ya watu Pembe ya Afrika yako njiapanda:UNICEF 

Ukame mkali unaua mifugo katika jamii ya wafugaji Higlo Kebele nchini Ethiopia.
© WFP/Michael Tewelde
Ukame mkali unaua mifugo katika jamii ya wafugaji Higlo Kebele nchini Ethiopia.

Mamilioni ya maisha ya watu Pembe ya Afrika yako njiapanda:UNICEF 

Tabianchi na mazingira

Taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF inasema hali ya utapiamlo nchini Somalia imefurutu ada ambapo Watoto milioni 1.4 karibu nusu ya Watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini humo wanauwezekano mkubwa wa kupata utapiamlo.

Na kati ya hao 330,000 watahitaji matibabu kwa sababu ya kuwa na unyafuzi. 

UNICEF inasema hii ni kutokana na hali mbaya ya ukame inayoikabili Pembe ya afrika ikiwemo Kenya, Ethiopia na Somalia ambayo imeathirika zaidi. Nchi hizo zinashuhudia wimbi la tatu la ukame mfululizo na baya kuwahi kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni. 

Kwa mujibu wa UNICEF Somalia pekee watu milioni 4.1 sawa na asilimia 25% ya watu wake wote wanahitaji haraka msaada wa chakula ili kuokoa maisha. 

Changamoto ya maji 

Shirika hilo la kuhudumia Watoto limesema watu milioni 2.6 wanahitaji huduma ya dharura ya maji, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka huku ukame ukizidi kuwa mbaya.  

Katika baadhi ya maeneo, bei ya maji imepanda kwa asilimia 72%. UNICEF inasema ukosefu wa maji huongeza milipuko ya magonjwa mathalani visa vya surua mwaka 2021 vilikuwa 7,500 ambayo ni mara mbili ya ilivyokuwa mwaka 2020 na 2019 zikijumuishwa pamoja.  

Angalau watu 60,000 wako katika hatari ya kuambukizwa magonjwa ya kuhara, ikiwa ni pamoja na kipindupindu limeonya shirika hilo. 

(PHOTO)

Uhamiaji 

Familia zinachukua hatua za kukata tamaa ili kuishi. Tangu Novemba, takriban watu 500,000 wameyahama makazi yao wakitafuta chakula, maji na malisho, na kuongeza wengine milioni 2.9 ambao tayari ni wakimbizi wa ndani. 

Watu kama Hinda Mohamed mwenye umri wa miaka 40 ambaye nilikutana naye Somaliland mnamo Desemba, alikuwa ametembea kwa siku 2 na watoto wake wawili na wazazi wake wazee amenukuu msemaji wa UNICEF mjini Geneva na kuongeza kuwa alikuwa amepoteza mbuzi na kondoo wake 200 kwa kukosa maji na malisho.  

Sasa akiwa hana lolote, mume wake anafanya kazi duni. Anasema kijiji chake kizima kilikimbia na hataki kurudi nyumbani. Pia mkimbizi huyo wa ndani amesema huu ndio ukame mkali zaidi kuhusuhudia tangu mwaka 2017. 

UNICEF inasema wakimbizi wa ndani ni kundi lililo hatarini zaidi na waliyojifunza kutokana na baa la njaa la mwaka 2011 yanaonyesha kwamba idadi kubwa ya vifo vilitokea miongoni mwa wale waliokimbia makazi yao. 

Hatari kwa wanawake na watoto  

Kwa mujibu wa UNICEF ukame huongeza hatari za ulinzi kwa watoto. “Tuna wasiwasi kuhusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia. Tuna wasiwasi kuhusu ndoa za utotoni. Na tuna wasiwasi kuhusu ukatili wa kijinsia, ambao tayari ulikuwa unaongezeka kwa asilimia 35 kati ya mwaka 2020 na 2021. Mwaka 2021, watoto 1,200 (wakiwemo wasichana 45) walisajiliwa na kutumiwa na makundi yenye silaha, watoto 1,000 walitekwa nyara. Katika matukio mengi, watoto hawa walikuwa waathirika wa ukiukwaji wa haki zao mara nyingi.” 

(PHOTO)

Je, haya yote yanamaanisha nini? 

UNICEF inasisitioza kuwa wakati wa kuchukua hatua ni sasa. Kwa sababu ukisubiri mpaka mambo yawe mabaya zaidi, au mpaka baa la njaa litangazwe, unaweza kuwa umechelewa.  

Shjirika hilo linasema historia inaonyesha kuwa utapiamlo unapochanganyikana na milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu na surua, vifo huongezeka haraka sana hasa miongoni mwa watoto. 

Kwa UNICEF 

Kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa hivi sasa linatoa ombo ladola milioni  $48m huku likiwa na pengo la dola milioni $38 kukidhi mahitaji yote.  

Na linahitaji haraka  dola milini $7 kufikia mwezi Machi ili kuagiza vifaa vya RUTF na kuzuia kukatika kwa msaada wa kibinadamu kuanzia Juni na kuendelea. Vinginevyo, watoto 100,000 walio na utapiamlo mkali sana watakosa matibabu ya kuokoa maisha.