Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yakabidhi vifaa vya kidijitali Kigoma Tanzania

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Rashidi Mchata, (kushoto) akipokea televisheni 14 na laptop 9 zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo,FAO. Katikati ni Mwakilishi Msaidizi wa FAO nchini Tanzania, Charles Tulahi.
FAO Tanzania
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Rashidi Mchata, (kushoto) akipokea televisheni 14 na laptop 9 zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo,FAO. Katikati ni Mwakilishi Msaidizi wa FAO nchini Tanzania, Charles Tulahi.

FAO yakabidhi vifaa vya kidijitali Kigoma Tanzania

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO hii leo limekabidhi seti 14 za televisheni na kompyuta ndogo 9 kwa serikali ya mkoa wa Kigoma nchini Tanzania ili kusaidia kusongesha uelewa wa jamii kuhusu masuala ya lishe na kutumia pia mawasiliano ya kidijitali katika kuimarisha sekta ya kilimo. 

Vifaa vimekabidhiwa na Mwakilishi Msaidizi wa FAO Charles Tulahi ambaye amesema,“vifaa hivi vitasaidia sana katika mawasiliano hususani hizo kompyuta ndogo kwenye uandaaji wa ripoti. Lakini vilevile tunashirikiana na wizara ya kilimo kuhakikisha kwamba tunajenga kilimo cha kidijitali ambacho tunafikiria hizo teknolojia za habari na mawasiliano zina mchango mkubwa katika kubadiliha kilimo chet una lishe Tanzania. Lakini na Televisheni tulizozitoa tunafikiria, tunaanzisha lakini ni eneo ambalo tunafikiri linaweza kusambaa hata katika vituo vingine na kuleta mchango mkubwa katika eneo hili la lishe na kuweza kuwafahamisha wananchi taarifa mbalimbali kuweza kujifunza lakini vile vile kuamsha ari ya kuweza kutafuta taarifa zaidi kutoka kwa maafisa lishe na wataalamu wengine wa lishe. Tunafikiri tunaweza kuchangia kwa namna hiyo.”

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma, Rashid Mchata amesema, “vifaa hivi vitatusaidia sana. Kama unavyofahamu mkoa wa Kigoma ni moja ya mikoa ambayo katika utekelezaji wa lishe tuko chini na tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba tunapambana na udumavu na tatizo la utapiamlo. Kwa hiyo vifaa hivi vitasaidia pindi pale ambapo wananchi wetu wanapotembelea vituo vya afya kwa ajili ya kupata matibabu, kutokana na video mbalimbali ambazo zinaelezea namna ya kuandaa chakula bora ambacho kina lishe bora ili wanaporudi katika maeneo yao waweze kuzingatia.”