Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna wakati nalala bila kula – Mjamzito nchini Ethiopia

Tangu Novemba 2020, mzozo kaskazini mwa Ethiopia umesababisha mamilioni ya watu kuhitaji usaidizi na ulinzi wa dharura.
© UNICEF/Christine Nesbitt
Tangu Novemba 2020, mzozo kaskazini mwa Ethiopia umesababisha mamilioni ya watu kuhitaji usaidizi na ulinzi wa dharura.

Kuna wakati nalala bila kula – Mjamzito nchini Ethiopia

Msaada wa Kibinadamu

Tathmini mpya ya uhakika wa upatikana wa chakula iliyotolewa mwishoni mwa mwezi Januari 2022 na Shirika la Umoja wa Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP, inaonesha takriban asilimia 40 ya wakazi wa Tigray Ethiopia wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula ikiwa ni miezi 15 ya migogoro kaskazini mwa Ethiopia.

Video ya WFP ikimuonesha Hiwot, mama wa watoto wanne ambaye kwa sasa ni mjamzito akiwa na binti yake ambaye awali alikuwa na utapiamlo lakini msaada wa chakula chenye lishe kutoka WFP umemsaidia sasa kuwa na hali nzuri. Mama huyu anaeleza kuwa hata yeye anategemea usaidizi wa lishe ya WFP katika kipindi chote cha ujauzito wake kwani familia yake inaishi kwa chai na injera, “kwa sababu ya uhaba wa chakula tunawapa watoto wetu kwanza na ikiwa kuna kitu chochote kimebaki ndio tunaweza kula. Vinginevyo, tunaenda kulala tumbo likiwa tupu. Ingawa mimi ni mjamzito sijapata mlo kamili.”

Hali hii si kwa Hiwot peke yake, utafiti wa WFP ulibaini asilimia 13 ya watoto wa Tigray walio chini ya miaka 5, nusu ya wanawake wote wajawazito na wale wanaonyonyesha wana utapiamlo, hivyo kusababisha matokeo mabaya ya ujauzito, uzito mdogo, udumavu na vifo vya uzazi.

Adrian Van Der Knaap, Naibu Mkurugenzi wa WFP nchini Ethiopia anasema inakadiria kwa wastani, familia zilizoathiriwa na mzozo kaskazini mwa Ethiopia zilikuwa zikipata chini ya asilimia 30 ya mahitaji yao ya kalori katika miezi iliyopita, na kwamba uhitaji wa chakula utaendelea kwa mwaka mzima wa 2022, “migogoro inaendelea kusababisha njaa zaidi na zaidi. Tuna watu milioni kadhaa huko Tigray katika hali mbaya sana, mamia ya maelfu ya watoto wenye utapiamlo sana huko Afar, huko Amhara pia hali sio nzuri. Kwa jumla zaidi ya watu milioni 9 hawana chakula kwa sasa.”

WFP imetoa ombi la msaada wa dola milioni 337 kusaidia wakazi wa  Kaskazini mwa Ethiopia katika kipindi cha miezi sita ijayo.  Na katika nchi ya Ethiopia ina pengo la ufadhili ambalo halijawahi kushuhudiwa la dola milioni 667  ili kuweza kubadili maisha ya watu milioni 12 katika kipindi cha miezi sita ijayo.