Hatimaye shehena za misaada ya kibinadamu zaingia Tigray- WFP
Hatimaye shehena za misaada ya kibinadamu zaingia Tigray- WFP
Msafara wa malori 50 ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP yaliyosheheni misaada ya kibinadamu leo hii hatimaye yameingia Mekelle mji mkuu wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia baada ya vuta ni kuvute ya muda mrefu.
Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Addis Ababa, Ethiopia imesema shehena hiyo ya tani 900 ni pamoja na vyakula na kwamba hata hivyo idadi ya marambili ya malori yaliyowasili leo inapaswa kuingia jimboni humo kila siku ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu.
Takribani watu milioni 4 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula jimboni Tigray, na WFP inatakiwa kusafirisha zaidi ya tani za ujazo 10,000 za chakula na lita za ujazo 150,000 za mafuta kila wiki kwa niaba ya wadau wa kibinadamu.
“WFP inakaribisha ruhusa kutoka serikali ya Ethiopia kwa msafara huu wa sasa kuingia salama jimboni Tigray,” amesema Tommy Thompson, mratibu wa masuala ya dharura wa WFP.
Hata hivyo amesema wanahitaji kuongeza maradufu idadi hiyo ya magari yanayoingia kila siku na kwamba ili kukidhi mahitaji ya watu ya kuokoa maisha yao, wanahitaji siku mbili kufika Mekelle badala ya siku nne walizotumia sasa.
Ameongeza kuwa hifadhi yao ya chakula na mafuta ni chini mno na kinatia shaka akisema tunachofanya sasa ni kupeleka kila tulicho nacho. Mafuta pekee tunahitaji tenki 20 zifikie Tigray kila mwezi.
Msafara wa leo ni pamoja na tenki la kubebea mafuta lita elfu 48, malori 29 ya WFP yenye chakula, malori 6 ya WFP yakiwa na vifaa vya kuhifadhi vyakula na bidhaa nyingine, na malori 14 yenye vifaa afya na vya kujisafi.
Malori 29 ya ngano, dengu na mafuta ya kupikia yatasaidia watu 200,000 huko Tigray wenye mahitaji ya dharura.
Msafara huo ulisafiri kilometa 445 kwa siku nne kutoka Semera hadi Mekelle kupitia Abala. Ulipitia maeneo yenye vituo 10 vya ukaguzi ambapo shehena hizo zilikaguliwa kwa kina.
Huu ni msafara wa kwanza wa WFP wenye shehena za kibinadamu kuingia Tigray tangu kuanza tena kwa operesheni za mapigano maeneo ya kaskazini-magharibi tarehe 2 mwezi huu wa Julai kufuatia mapigano. Tangu wakati huo, WFP imeshagawa mlo wa dharura kwa watu 135,000.
TAGS: WFP, Ethiopia, Tigray, Msaada wa Kibinadamu