Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua ya Katibu Mkuu wa UN kuwasilisha vipaumbele vyake kwa Baraza Kuu ina maana gani?  

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza Kuu la Umoja waMataifa kuhusu vipaumbele vyake kwa mwaka 2022
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza Kuu la Umoja waMataifa kuhusu vipaumbele vyake kwa mwaka 2022

Hatua ya Katibu Mkuu wa UN kuwasilisha vipaumbele vyake kwa Baraza Kuu ina maana gani?  

Masuala ya UM

Hii leo Januari 21, mwaka 2022, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasilisha vipaumbele vyake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya ngwe nyingine ya mwaka baada ya mapumziko ya mwisho wa mwaka.   

Vipaumbele hivi alivyovitaja Bwana Guterres vinaeleza yale ambayo yeye akiwa ni kiongozi wa sekraterieti ya Umoja wa Mataifa, anakusudia kuvitekeleza.  

Ili kufahamu zaidi kuhusu tukio hili Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa imezunumza na Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Profesa Kennedy Gastorn kwanza kutaka kufahamu tukio hili la leo lina maana gani? Balozi Gastorn anaeleza akisema, “hili ni jambo la kiutaratibu na ni jambo la kikanuni. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kama moja ya mihimili ya Umoja wa Mataifa ni wajibu wake kuandaa vitu ambavyo atavifanyia kazi katika mwaka. Na mwaka kwa maana ya katika kikao cha 76 kilichoanza Septemba mwaka jana 2021 ambapo mwaka huu utaisha Septemba 2022. Sasa mpaka sasa hivi tumeshapita miezi takribani mitatu hivi tangu mwaka wa Umoja wa Mataifa umeanza. Kwa manaa ya mwaka wa 76. Kwa hiyo huu ni utaratibu ambao yeye anatakiwa kwanza kuandaa  ratiba ya shughuli zake ambazo atazifanya. Ratiba hizo zinatokana na majukumu ambayo amepewa na nchi wanachama katika maazimio mbalimbali aliyopewa kuyafanyia kazi. Mara kwa vipindi anapokuwa amemaliza labda muda wa miezi miwili mitatu katika mwaka husika, huwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anakuja kwa nchi wanachama kuwaelezea vipaumbele vyake katika majukumu mengi aliyonayo katika mwaka huo na ndio maana kwa utaratibu huu anakuja mwezi huu wa Januari akitueleza au akiwaelezea nchi wanachama ni mambo gani yatakuwa ni ya kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka huu wa 2022 ili pia nchi wanachama waweze kumpa ushirikiano n anchi wanachama waweze kujua majukumu hayo.” 

Balozi Kennedy Gaston, mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa.
Tanzania Mission
Balozi Kennedy Gaston, mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa.

 

Na je kuna hatua yoyote inayofuata ya ufuatuliaji wa utekelezaji inayofanywa na nchi wanachama baada ya Katibu Mkuu wa UN kutangaza vipaumbele vyake?   

“Ndio! Baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoa vipaumbele vyake, nchi wanachama wanafuatilia utekelezaji. Kwa maana kwamba sasa Katibu Mkuu anaendelea na utekelezaji wa hayo aliyoyasema na mwisho atakuja kurudi tena na kuweza kuwaelezea wanachama jinsi ambavyo ameweza kutekeleza vipaumbele vyake lakini pia anatumia nafasi hii kuamba ushirikiano kwa nchi wanachama katika vipaumbele vyake. Kumbuka, hata kitendo cha yeye kuja sasa hivi kwenye Baraza Kuu ni na kueleza vipaumbele vyake, ni sehemu ya mfumo wa Baraza Kuu kuweza kumsimamia na kuweza kufahamu shughuli zake.” Anafafanua Balozi Gastorn 

Na Katibu Mkuu Guterres akiwa ameyakusanya masuala yote muhimu katika vipengele vitano alivyoviita kama tahadhari ya moto unaopaswa kuangaliwa kwa hali ya dharura, pamoja na kutaja ugonjwa wa Covid-19, hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, matumizi mabaya ya mitandao na amani na usalama, kingine ametaja mfumo wa fedha duniani na kipengele hiki kikitaka marekebisho ya mfumo wa fedha duniani ambao kwa sasa kwa kiasi kikubwa unanufaisha nchi tajiri kuliko zinazoendelea na akionekana kulipa uzito bara la Afrika. Kwa nini Afrika? Balozi Profesa Kennedy Gastorn anaeleza akisema,  “Afrika ni miongoni mwa maeneo ambayo yako nyuma kiuchumi. Ni miongoni mwa maeneo ambayo yana changamoto nyingi hasa tunapoenda mwaka 2030 katika utekelezaji wa malengo yale endelevu na kwa hiyo msukumo wa Umoja wa Mataifa ni pamoja na kusaidia nchi za Afrika na kusaidia wadau wa maendeleo kuweza kushirikiana na Afrika kuweza kuleta maendeleo. Kwa hiyo ni jambo zuri. Na katika mktadha huo  unaweza kuona kwa jinsi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anajitahidi sana kuufanya Umoja wa Mataifa uwe na jicho maalumu kuhusu Afrika na hilo jicho linagusa nyanja zote za maslahi ya Afrika.”