Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hata hapa Umoja wa Mataifa, mabalozi wengi wanazungumza Kiswahili- Profesa Kennedy Gastorn 

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Kennedy Gastorn wakati wa mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.
UN News/Anold Kayanda
Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Kennedy Gastorn wakati wa mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Hata hapa Umoja wa Mataifa, mabalozi wengi wanazungumza Kiswahili- Profesa Kennedy Gastorn 

Utamaduni na Elimu

Lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya kwanza ya kiafrika inayozungumzwa na watu wengi zaidi barani Afrika, ikiendelea kupokelewa na kutumiwa katika vyombo mbalimbali vya maamuzi kama vile kufanywa miongoni mwa lugha rasmi za SADC.

Assumpta Massoi amemhoji Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Profesa Kennedy Gastorn kuhusu juhudi za kuweza kukipa nafasi zaidi Kiswahili katika Umoja wa Mataifa. 

Balozi Profesa Kennedy Gastorn anasema, “lugha ya Kiswahili ni lugha muhimu sana. Kwanza kumbuka ni lugha ya ukombozi wa Afrika. Lugha ya Tanzania lakini kwa kweli imetumika katika kuleta maendeleo makubwa sana ndani ya nchi ya Tanzania na nje ya mipaka ya nchi ya Tanzania hasa kusini mwa Afrika. Ikumbukwetu tu kuwa wakati wa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi za SADC, walichukua uamuzi madhubuti kabisa kwamba Kiswahili kitakuwa ni lugha ya nne rasmi ya SADC. Na lugha ya Kiswahili tayari ni lugha ya shirikisho la Afrika yaani AU."

Amesema kwa wao kwenye Umoja wa Mataifa, "kazi yetu kubwa sana kwakweli ni kujaribu kutumia nafasi, yaani kutafuta fursa za kuweza kuendeleza Kiswahili na watu wengi wamekuwa wakitoa mapendekezo kwamba sasa tujaribu tuweze kuona tufanyeje ili tuweze kukisukuma Kiswahili kipate nafasi ambayo kwakweli inafaa. Nchi nyingi hata hapa Umoja wa Mataifa, mabalozi wengi wanaongea Kiswahili na wanatambua mchango wa Kiswahili. Kwa hiyo ni mkakati mzuri sana na katika hili labda tumshukuru tena Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa jinsi ambavyo amejitahidi sana kukifanya Kiswahili kiende mbele. Amekikuza Kiswahili katika ngazi ambayo kwakweli wengi hatukufikiria. Kimefika sehemu ambako kwakweli sasa ni jukumu letu sisi kama nilivyosema kuweza kutumia nafasi tulizonazo, kutafuta fursa na namna ambavyo tunaweza kukiendeleza Kiswahili katika mikutano yetu, katika kukitangaza na kadhalika.”