Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afghanistan: zaidi ya kazi 500,000 zimepotea tangu Taliban walipotwaa nchi - ILO

Wakimbizi wa ndani wakisimama kwenye mstari kusubiri mgao wa msaada mjini Kabul, Afghanistan
© UNHCR/Tony Aseh
Wakimbizi wa ndani wakisimama kwenye mstari kusubiri mgao wa msaada mjini Kabul, Afghanistan

Afghanistan: zaidi ya kazi 500,000 zimepotea tangu Taliban walipotwaa nchi - ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO limesema ajira zilizotoweka nchini Afghanistan kufuatia ambadiliko ya utawala mwezi Agosti mwaka jana wa 2021 zilifikia zaidi ya nusu milioni kwenye robo ya tatu ya mwaka jana na makadirio ni kwamba kiwango hicho kinaweza kufikia laki tisa katikati yam waka huu wa 2022.

Taarifa ya ILO iliyotolewa leo Bangkok, Thailand imenukuu makadirio mapya ya shirika hilo kuhusu mweleko huo yakisema kuwa kusinyaa kwa fursa za ajira kwa asilimia 14 ifikapo katikati yam waka huu ni taswira halisi ya idadi ya wafanyakazi walioondolewa kwenye ajira kutokana na mabadiliko ya utawala sambamba na janga la kiuchumi linaloshamiri pamoja na vikwazo dhidi ya wanawake kufanya kazi. 

Jumla ya saa ambazo kazi ilifanyika katika uchumi wa Afghanistan inakadiriwa kupungua kwa asilimia 13 katika robo ya tatu ya mwaka 2021 ikilinganishwa na hali ya dhahania bila mabadiliko yoyote katika utawala. 

ILO inasema wafanyakazi wanawake wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na mzozo huo. Tayari kwa viwango vya kimataifa wakiwa chini, viwango vya ajira kwa wanawake vinakadiriwa kupungua kwa asilimia 16 katika robo ya tatu ya 2021 na hali ya kukata tamaa inayoonyesha kushuka kwa hadi asilimia 28 kufikia katikati ya mwaka huu wa 2022. 

Ramin Behzad, Mratibu Mwandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani, ILO kwa Afghanistan, anasema, "hali nchini Afghanistan ni muhimu na msaada wa haraka wa kuuweka sawa uchumi na ahueni unahitajika. Ingawa kipaumbele ni kukidhi mahitaji ya haraka ya kibinadamu, ahueni ya kudumu na shirikishi itategemea watu na jamii kupata ajira zenye staha, maisha na huduma za kimsingi." 

Sekta muhimu zimeharibiwa tangu kuchukuliwa kwa mamlaka hiyo ikiwa ni pamoja na kilimo, utumishi wa umma na sekta ya ujenzi ambazo zote zimeshuhudia upotevu mkubwa wa kazi au wafanyakazi kutolipwa. 

ILO inaendelea kukuza ajira zenye tija na kazi zenye staha kwa watu wa Afghanistan kwa kuzingatia ajira ya dharura, uwekezaji mkubwa wa ajira, kukuza biashara na ukuzaji wa ujuzi.