Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufufuaji wa soko la kazi unaenda kinyumenyume: ILO 

Kiwanda cha bidhaa za mauzo ya nje nchini Bangladesh.
ILO/Marcel Crozet
Kiwanda cha bidhaa za mauzo ya nje nchini Bangladesh.

Ufufuaji wa soko la kazi unaenda kinyumenyume: ILO 

Ukuaji wa Kiuchumi

Migogoro mingi ya kimataifa inasababisha kuzorota kwa hali ya soko la ajira duniani, na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa ndani ya nchi na kati ya nchi na nchi. Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani, (ILO). 

Toleo la 9 la Ufuatiliaji wa ILO kuhusu Ulimwengu wa Kazi, limegundua kuwa baada ya mafanikio makubwa katika robo ya mwisho ya mwaka 2021, idadi ya saa za kazi duniani ilipungua katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2022, hadi asilimia 3.8 chini ya kiwango cha kabla ya mgogoro (robo ya nne ya mwaka 2019). Hii ni sawa na upungufu wa kazi milioni 112. 

Taarifa ya ILO iliyotolewa hii leo mjini Geneva, Uswisi imeeleza kuwa hali hii inawakilisha kushuka kwa kiwango kikubwa cha takwimu zilizochapishwa na ILO mnamo Januari 2022. 

Migogoro mingi mipya na iliyounganishwa ya kimataifa, ikijumuisha mfumuko wa bei (hasa katika bei ya nishati na chakula), mtikisiko wa kifedha, kutokopesheka, na  kuvurugika kwa mnyororo wa usambazaji - unaochochewa na vita nchini Ukraine - inamaanisha kuwa kuna hatari inayoongezeka ya kuzorota zaidi kwa saa za kazi mwaka wa 2022, pamoja na athari pana katika soko la ajira duniani katika miezi ijayo. 

Uchokozi wa Urusi dhidi ya Ukraine tayari unaathiri soko la ajira nchini Ukraine na kwingineko, kama inavyofafanuliwa katika muhtasari wa hivi karibuni wa ILO. 

Ripoti hii pia imegundua kuwa wakati nchi za kipato cha juu zilipata ahueni katika saa zilizofanyiwa kazi, uchumi wa chini na wa chini kati ulikumbwa na misukosuko katika robo ya kwanza ya mwaka na pengo la asilimia 3.6 na 5.7 mtawalia ikilinganishwa na kipimo cha kabla ya mgogoro. Mwelekeo huu wa  kutofautiana huenda ukawa mbaya zaidi katika robo ya pili ya 2022. 

Katika baadhi ya nchi zinazoendelea, serikali zinazidi kubanwa na ukosefu wa nguvu ya fedha na changamoto za uhimilivu wa deni, wakati makampuni ya biashara yanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa kiuchumi na kifedha na wafanyakazi wanaendelea kuachwa bila upatikanaji wa kutosha wa ulinzi wa kijamii. 

Zaidi ya miaka miwili baada ya janga hili kuanza, wengi katika ulimwengu wa kazi bado wanateseka kutokana na athari kwenye soko la wafanyakazi. 

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Ryder amesema, "ahueni ya soko la ajira duniani imekwenda kinyumenyume. Ahueni isiyo sawa na dhaifu imefanywa kutokuwa na uhakika zaidi na mchanganyiko unaojiimarisha wenyewe wa migogoro. Athari kwa wafanyakazi na familia zao, hasa katika ulimwengu unaoendelea, itakuwa mbaya na inaweza kutafsiri kuwa mgawanyiko wa kijamii na kisiasa. Sasa ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kwamba tufanye kazi pamoja na kuzingatia kuunda ahueni inayozingatia mwanadamu." 

Ripoti hiyo inaeleza msururu wa hatua za kuchukua kama njia ya kusonga mbele, ambayo inaambatana na Wito wa Kimataifa wa Kuchukua Hatua wa ILO kwa ajili ya ahueni inayomhusu binadamu, na mpango wa Umoja wa Mataifa unaoongozwa na ILO. Hatua hizo ni pamoja na:  

Usaidizi wa wakati unaofaa na mzuri wa kudumisha uwezo wa ununuzi wa mapato ya wafanyakazi na hali ya jumla ya maisha ya wafanyakazi na familia zao. 

Mazungumzo ya haraka ya pande tatu ili kusaidia marekebisho yanayofaa na ya haki ya mishahara ikijumuisha kima cha chini cha mishahara, uimarishaji wa mifumo ya hifadhi ya jamii na usaidizi wa mapato, na utoaji wa hatua za uhakika wa chakula inapobidi. 

Marekebisho makini ya sera za uchumi mkuu ili ziweze kushughulikia shinikizo zinazohusiana na mfumuko wa bei na uhimilivu wa deni huku zikisaidia urejeshaji wa wingi wa kazi na ujumuishaji. 

Msaada kwa vikundi na sekta zilizokumbwa na hali ngumu, hasa wafanyakazi walio katika mazingira magumu na wale wanaofanya mabadiliko kutoka kwa uchumi usio rasmi kwenda kwa uchumi rasmi. 

Sera za muda mrefu za kisekta zilizoundwa vyema zinazokuza uundwaji wa ajira zenye hadhi, kusaidia uendelevu na ushirikishwaji, na kusaidia biashara, hasa biashara ndogo ndogo na za kati (MSMEs).