Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ninaishi na VVU lakini nina afya njema na uwezo mkubwa wa kazi. Msitubague - Wu Megnam

Utepe mwekundu- ishara ya kimataifa ya kampeni ya kupambana na VVU na UKIMWI
Public Health Alliance/Ukraine
Utepe mwekundu- ishara ya kimataifa ya kampeni ya kupambana na VVU na UKIMWI

Ninaishi na VVU lakini nina afya njema na uwezo mkubwa wa kazi. Msitubague - Wu Megnam

Haki za binadamu

Shirika la kazi la Umoja wa Mataifa ILO limeendelea mara zote kuhamasisha mazingira mazuri ya kazi ikiwemo kutokuwepo kwa ubaguzi au unyanyapaa kwa wafanyakazi kutokana na hali zao iwe ulemavu au ugonjwa.  Kisa hiki cha  Wu Mengnan wa China, ambaye miaka 15 iliyopita yeye na mumewe walipimwa na kukutwa na Virusi Vya UKIMWI, VVU kinaonesha kuwa bado kuna haja ya kufanya zaidi ili kukomesha ubaguzi na unyanyapaa mahali pa kazi au wakati wa kutafuta ajira. Taarifa ya Anold Kayanda inaeleza zaidi.

« Jina langu ni Wu Mengnam. Mume wangu aliniambukiza Virusi Vya UKIMWI, VVU zaidi ya miaka 10 iliyopita. » Hivyo ndivyo anavyoanza kueleza mwanamke huyu raia wa China akisema kutokana na hali hiyo, maisha yamebadilika sana.  

Anasema miaka hii imekuwa migumu sana na alilazimika kumuhudumia mume wake kipindi cha kuugua na wakati huo huo kumlea mtoto wake wa kiume. Mume wake alipofariki, familia ikavunjika na mzigo wa kumlea mtoto wao ukaangukia mabegani mwake peke yake. 

« Nilitaka kufanya kazi kwa bidii ili kupata pesa lakini nikagundua kuwa waajiri wote wazuri walikuwa wanataka vipimo vya afya na watu wanaoishi na VVU kama mimi wote walikataliwa. » Anasema Wu na kwa hivyo kwa miaka yote amebakia kufanya kazi za vibarua au muda mfupimfupi huku na kule kuanzia zile zinazolipa kidogo mno na hata zile zisizo za kuaminika. Maisha yakawa magumu, « Kazi nyingi kwa watu wanaoishi na VVU ni kazi za chnichini tu. Wanafanya kwa miezi mitatu au mitano na kisha wanabadili kwenda kwenye nyingine. Hawataki kukaa katika eneo moja kwa muda mrefu kwa sababu kuna vipimo vya afya katika maeneo ya kazi kila mwaka ambavyo wanaviogopa kwa hivyo wanakimbia. Wengi wao wanalipwa Yuan laki chache kwa mwezi, kama hapa au Yuan elfu mbili kwa mwezi takribani dola 300 hivi za kimarekani. Hawawezi hata kufikiria kuhusu kazi nzuri zinazolipa vizuri. » Anasema Wu. 

Bi Mengnam anasema kila anapomtazama mtoto wake, mara nyingi anajisikia vibaya kwa kushindwa kumpatia maisha mazuri  kama anavyosema, « ninatumai ninaweza kutengeneza Yuan 3,000 hadi 5000, takribani dola 780 kwa mwezi ili mambo yangu yaweze kuwa mepesi zaidi na mzigo wa kisaikolojia na mashinikizo mengine yataondoka. Mimi ni mtu ninayeishi na Virusi Vya UKIMWI lakini nina uwezo. Nina afya na nina uwezo wa kufanya kazi. Ni matumaini yangu kuwa siku moja jamii haitakuwa inatutazama kwa namna tofauti na watatoa fursa sawa kwa wenye maambukizi.”