Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNCDF yawezesha mradi wa umeme wa maporomomoko ya maji Tanzania

Usaidizi kutoka mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya mitaji, UNCDF kwa kampuni ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji AHEPO huko Ruvuma kumewezesha wananchi wa Mbinga kupata huduma ya umeme.
UNCDF/Video
Usaidizi kutoka mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya mitaji, UNCDF kwa kampuni ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji AHEPO huko Ruvuma kumewezesha wananchi wa Mbinga kupata huduma ya umeme.

UNCDF yawezesha mradi wa umeme wa maporomomoko ya maji Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya mitaji, UNCDF imewezesha wakazi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kupata huduma ya nishati salama isiyo na madhara siyo tu kwa binadamu bali pia mazingira.

 

Hatua hiyo ni kwa kutambua kuwa kupata huduma za nishati ni msingi wa maendeleo na hitaji la msingi katika kukidhi mahitaji ya binadamu na ukuaji wa uchumi. Ukosefu wa huduma ya msingi ya nishati kwa ajili ya taa, kupika,  kutia joto, usafirishaji na mawasiliano kunasababisha jamii hususan wanawake kutumia muda mwingi kwa ajili ya kujikimu mahitaji hayo. 

Huduma hiyo ya nishati salama ya umeme unaozalishwa kwa maji inatokana na mradi wa kampuni ya Andoya Hydroelectric power, AHEPO kwa usaidizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya mitaji, UNCDF.

Sasa situmii tena nguvu nabonyeza tu kitufe

Miongoni mwa wanufaika ni Heri Ndunguru ambaye anasema,“nilianza na mashine za kusagisha kwa kutumia dizeli. Madhara yake yalikuwa unatoka unga mweusi sana, na hivyo hata wateja nilipata kwa shida kweli.”

Bwana Ndunguru anaendelea kusema kuwa, “baada ya kuja kwa huu umeme wa Andoya nikabahatika kubadilisha nikaweka mota hizo za umeme unanisaidia sana. Kwanza  nafanya kazi kwa wepesi bila maumivu. Zamani nilikuwa nazungusha kwa mkono na kifua naumia sana, lakini sasa hivi ni kubonyeza tu. Kwa hiyo kwa kweli kuna faida kubwa sana. Pia imenisaidia hata faida napata na ndio ikaniwezesha kununua mashine ya kuranda. Pia naranda mbao. Nikapata tena mashine ya kuchomelea, tunachomea hapa mageti, pikipiki. Kwa hiyo nimefaidika nao sana huu umeme wa Andoya.”

Lakini nini msingi wa kuanzishwa kwa umeme wa Andoya? Janet Andoya ni muasisi mwenza wa kampuni ya AHEPO na anasema “malengo ya kuanzisha huu mradi ni kwamba tuliona katika vijii hivi kuwa hawana aumeme, kwa hiyo na hivyo hawana umeme na tukaona tunayo maji ya kutosha ambayo kama yakishughulikiwa vizuri tunaweza kupata umeme.”

Bila umeme wakati wa kujifungua wangemulika kwa mshumaa?

Ama hakika umeme umebadili jamii hii. Hayawi hayawi, yamekuwa! Miezi 9 tu ya utekelezaji wa wazo la nishati salama, shule 6 sasa zina masomo ya nyongeza nyakati za jioni, hospital 2 sasa zinaendesha huduma zake kwa saa 24, ikimaanisha wanawake wanaweza kujifungua salama muda wowote ule wa siku. Taasisi 12 kati ya taasisi 70 za umma wilayani Mbinga zimeunganishwa na umeme huu, biashara ndogo na kati 63 kati ya 380 zimeunganishwa na umeme, na zaidi ya yote kaya 256 nazo zina umeme.

Emmanuel Budeba ni daktari katika zahanati ya kilimani wilayani Mbinga na ni shuhuda wa mabadiliko hayo akisema, “tuna jokofu la chanjo ambalo tunatumia kuhifadhia chanjo na inaturahisishia watu wa kijiji tunachohudumia na vijiji jirani visivyo na umeme wanafuata huduma huku. Na huo mwanga unatusaidia hasa kusaidia wanawake wajawazito wanaojifungua usiku. Kwamba tunatumia mwanga tunaweza kuwahudumia kwa urahisi, tofauti na tusingekuwa na mwanga wau meme.”

Hoja ya Dkt. Budeba inaungwa mkono na mwanakijiji Elizabeth Ndunguru akisema, “nilijifungua hapa saa nane za usiku. Uliweza kunisaidia umeme wa Andoya wa maji. Yaani hapa kukosa umeme,kw amama mjamzito kama mimi unaweza kufa. Kwa sababu unatakiwa uongezewe njia, tungemulikia na nini. Umeme unasaidia.”

Umoja wa Mataifa unasema wanawake ndio wabebao mzigo wa kufanya kazi ikiwemo zile zisizo na ujira. Uwepo wa umeme utawezesha wanawake kuweka mizania kwenye maisha yao. Na ndio maana ya malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs namba 1, la kutokomeza umaskini, 5 la usawa wa jinsia na 7 la nishati salama na nafuu kwa kila mtu.

Na kwa kupitia mradi wa nishati ya AHEPO kwa usaidizi wa UNCDF malengo hayo  yanafikiwa.

TAGS: UNCDF, Ruvuma, Tanzania, AHEPO, SDGs