Nuru yanyemelea bonde la Msimbazi, Tanzania, wadau washirikishwa

13 Novemba 2018

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia wanatekeleza  mradi wa kupunguza madhara ya mafuriko kwenye bonde la Msimbazi jijini Dar es salaam, mafuriko ambayo mapema mwaka huu yalisababisha vifo vya watu 15. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

Jiji la Dar es salaam, nchini Tanzania ambalo takwimu zinaonyesha kuwa kutokana na fursa za uchumi zilizopo, kila siku watu 1000 huingia jijini humo.

Licha ya fursa hizo, uchafuzi wa mazingira ikiwemo mto Msimbazi unatishia mazingira ya jiji hilo kutokana na taka zinazotupwa hovyo na kutelekezwa na hatimaye mvua zinaponyesha huleta madhara na  hata vifo kama anavyoelezea Habiba Mandoma, kiongozi wa wakazi wa bonde la Msimbazi.

"Mafuriko yanapotokea tunaathirika kwa njia nyingi. Mosi, afya zetu, haya maji ni machafu. Pia yanaharibu nyumba zetu, na watoto hawawezi kwenda shule kwa sababu vitabu vyao na sare za shule vimelowana.”

Sasa Benki ya Dunia kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania wameanzisha mradi wa kuboresha bonde hilo la Msimbazi ambapo warsha zinafanyika zikileta wadau wote wakiwemo viongozi wa serikali, wataalam wa kiufundi na wananchi kwa lengo la kuamua mustakabali wa bonde hilo.

Dkt. Venance Makota kutoka Baraza la Mazingira la TAifa, NEMC anafafanua matokeo ya warsha hiyo.

“Hadi sasa kuna mapendekezo matatu. Kuna kisiwa cha hazina, kuna bustani oevu na eneo litakaloendelezwa mbele ya mto. Hatimaye tutakuwa na chaguo moja ambayo itaboresha eneo hilo.”

Vikao vya kubaini mustakhbali huo vimefanyika kwa zaidi ya miezi tisa na uendelezaji wa mradi wa bonde la mto Msimbazi ni sehemu ya miradi mitatu ya Benki ya Dunia ya kujenga mnepo kwa miji nchini Tanzania.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter