UNCDF yachochea maendeleo mji wa Kibaha nchini Tanzania

15 Julai 2020

Mtaji kutoka shirika la maendeleo ya mitaji la Umoja wa Mataifa, UNCDF kwa halmashauri ya mji wa Kibaha mkoani Pwani nchini Tanzania umewezesha ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani na hivyo kuchochea maendeleo si tu ya jamii bali ya mkoa husika.

UNCDF ilifanya kazi na halmashauri ya mji wa Kibaha kwa kuipatia mtaij wa fedha wa uwekezaji na msaada wa kiufundi katika kujenga kituo kipya cha basi.

Innocent Byarugaba, ambaye ni Afisa Mawasiliano wa Halmashauri ya Kibaha anasema kuwa, “kwa kifupi tukiongelea ubora wa kituo hiki cha basi, ni kituo bora kabisa Tanzania kwa sababu ukilinganisha na kule tulikotoka, kilikuwa ni kituo ambacho kilikuwa kimejengwa kwenye hifadhi ya barabara.”

Hivi sasa kituo hicho kinahudumia zaidi ya abiria 14,000 kila siku, hali iliyoibua ongezeko la mahitaij ya bidhaa na huduma na kuwa kivutio kwa biashara na watu kujipatia ajira hususan wakazi wa kibaha, wakiwemo vijana wa kike.

Aneth Skoyo ni mmojawao na anasema kuwa, “katika kituo cha zamani sikuweza kuzunguka, nilisalia kwenye ofisi kwa sababu nilikuwa mwajiriwa. Lakini sasa naweza kufanya biashara na najitegemea.”

Kwa Halmashauri ya mji wa Kibaha, kituo kimejengwa wakati muafaka ambapo Bwana Byarugaba anasema, “kwanza kituo cha awali hakikuwa na sehemu maalum ya mabasi kupitia, kwa hiyo mabasi yalikuwa yanaweza kupita upande wowote na pengine kama kuna mvua kubwa na kwa sababu ya tope lililokuwepo, yanapitiliza barabara kuu na hayaingii kituoni na hivyo abiria walikuwa wanaachwa licha ya kwamba walikuwa wamelipa nauli zao.

Kibaha ni kituo cha mpito kwa magari yanayosafiri kwenda na kutoka mikoa 29 ya Tanzania na nchi jirani za Kenya, Tanzania, Uganda,  Malawi, na Zambia kwa hiyo uwepo wa kituo hiki unawezesha mji wa Kibaha kutumika kikamilifu na sasa mapato yameongezeka maradufu kutoka asilimia 30  hadi 60.

Bwana Byarugaba anasema kuwa manufaa ni zaidi ya mapato kwa halmashauri kwa kuwa, “pamoja na kwamba imeongeza mapato kwa halmashauri na serikali kwa ujumla, pili kituo kimetoa ajira nyingi, kumbuka kuwa humu ndani kuna vijana ambao wanauza bidhaa ndogo ndogo, matunda na biskuti. Vijana hawa wamejiajiri, badala ya kwenda mitaani kuiba, sasa wako sehemu wanapata fedha wanatunza familia zao.”

Sasa halmashauri inajenga na soko karibu na kituo, huku barabara za mizunguko na miundombini mingine kama ya majitaka na umeme nayo ikiimarishwa na hivyo kuchochea utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud