Chanjo chanjo chanjo ndio jawabu mujarabu dhidi ya Omnicron- WHO

4 Januari 2022

Virusi aina ya Omnicron vikiendelea kuwa sababu ya kasi kubwa ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 hivi sasa duniani kote, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO hii leo limesema ni muhimu hatua zaidi zikachukuliwa ili kusaidia nchi zote kupata haraka iwezekanavyo chanjo dhidi ya Corona kwa kuwa ndio mkombozi iwapo mtu anaambukizwa na tayari ana chanjo. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi hii leo, Dkt. Abdi Mahmud ambaye ni mtaalamu wa masuala ya maambukizi ya magonjwa WHO amesema, ingawa hawajatapa takwimu mpya katika kipindi hiki cha sikukuu, hadi tarehe 29 mwezi uliopita wa Desemba nchi 129 duniani kote zilisharipoti uwepo wa virusi aina ya Omnicron.

Amesema takribani nchi zote hizo hazikuwa na uwezo wa kufanikisha asilimia 70 ya utoaji wa chanjo ya Corona kwa wananchi wake kama ilivyopendekezwa na WHO  kama njia mojawapo ya kudhibiti maambukizi.

Mtaalamu  huyo ametumia kile wanachoona Afrika Kusini kama kipimo cha wastani kwa nchi nyingine akisema, “tunachoona sasa ni kile tunachokona katika nchi nyingine. Kuna ongezeko kubwa la idadi ya wagonjwa lakini kiwango cha vifo ni kidogo nchini Afrika Kusini. Hata Marekani kuna idadi kubwa ya wagonjwa na wanaolazwa. Huko Uingereza nako jiini London, idadi ya wagonjwa wanaolazwa ni kubwa. Idadi ya waliolazwa  tarehe 29 mwezi Desemba mwaka 2021 ilikuwa 700 ikilinganishwa na 900 mwaka 2020 wakati hatuna chanjo. Tuna chanjo watu wamechanjwa lakini tunaona watu wengi zaidi walio hatarini ambao hawajachanjwa wakifika hospitalini kulazwa.”

Kwa mantiki hiyo amesema ujumbe wake ni “kama umechanja umelindwa, na iwapo uko hatarini au  hujachanjwa, hii Omnicron hata kama madhara yake ni madogo kwa wengine itakupata kwa ukali mno, kwa hiyo chanjo ni muhimu sana.”

Dkt. Mahmud amezungumzia pia taarifa ya kwamba Omnicron inaathiri zaidi sehemu ya juu ya mwili tofauti na aina zingine za virusi zilizokuwa zinaathiri mapafu na kusababisha vichomi au numonia lakini amesema tafiti zaidi zinahitajika.

WHO imetaka ifikapo mwezi Juni mwaka huu wa 2022, kila nchi iwe imepatia chanjo asilimia 70 ya wananchi wake ili kudhibiti kusambaa na kunyumbulika kwa virusi vya Corona.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter