Skip to main content
Watoto nchini Côte d’Ivoire wanachora barakoa usoni ili kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa kuvaa barakoa ili kujilinda na COVDI-19

Mwaka 2022 uwe mwaka wa kutokomeza janga la Corona na kuimarisha sekta ya afya

© UNICEF/Frank Dejongh
Watoto nchini Côte d’Ivoire wanachora barakoa usoni ili kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa kuvaa barakoa ili kujilinda na COVDI-19

Mwaka 2022 uwe mwaka wa kutokomeza janga la Corona na kuimarisha sekta ya afya

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limesema bado lina matumaini kuwa mwaka 2022 unaweza kuwa mwaka sio tu wa kutokomeza awamu mbaya ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 bali pia kusaka mbinu thabiti za kuwa salama zaidi kiafya.
 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo leo huko Geneva, Uswisi wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni miaka miwili tangu kubainika kwa ugonjwa wa COVID-19.

Amesema ili kujenga uimara zaidi kutokana na mafanikio yaliyopatikana sasa sambamba na changamoto siyo tu kwa kugawa kwa uwiano na kwa haraka chanjo zilizopo hivi sasa kupitia majukwaa ya COVAX na AVAX bali pia kusaidia nchi kutengeneza chanjo hizo na kuzisambaza kwa kila mtu kokote aliko na kisha tiba mpya zifuate na zifikie kila mtu.

Dkt. Tedros ameonya “virusi vya COVID-19 vitaendelea kunyumbulika na kutishia mifumo ya afya iwapo hatutaimarisha hatua za pamoja kudhibiti janga hili.”

Mmoja wa Raia wa Uganda akipokea chanjo yake ya kwanza ya Covid-19 huko Hoima, Uganda.
John Kibego
Mmoja wa Raia wa Uganda akipokea chanjo yake ya kwanza ya Covid-19 huko Hoima, Uganda.

Vitisho pacha

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa WHO, hivi sasa virusi vya COVID-19 aina ya Delta na Omnicron ni vitisho pacha vinavyochochea ongezeko la wagonjwa katika idadi ambayo haikuwahi kufikiwa, hali ambayo pia inasababisha ongezeko la watu wanaolazwa hospitali kupata matibabu sambamba na idadi ya watu wanaokufa kutokana na ugonjwa huo.

“Nina wasiwasi kuwa Omnicron inasambaa kwa haraka zaidi huku Delta nayo inaenea wakati huo huo na hivyo kuongeza idadi kubwa ya wimbi kubwa la wagonjwa” amesema Dkt. Tedros akifafanisha na Tsunami ya wagonjwa.

Kuna mafanikio

Akimulika mafanikio ya kukabili Corona, Dkt.Tedros ametambua  matumizi ya sayansi, majawabu sahihi na mshikamano.

“Maendeleo katika utengenezaji wa chanjo mpya ni mfano usio kifani wa matumizi ya sayansi,” huku akisema wakati mwingine siasa zimekwamisha mshikamano.

Bibi anapata chanjo ya COVID-19 katika hospitali ya Kathmandu, Nepal.
© WHO/Blink Media/Uma Bista
Bibi anapata chanjo ya COVID-19 katika hospitali ya Kathmandu, Nepal.

“Vitendo vya baadhi ya nchi kuzingatia zaidi uzawa na kujilimbikizia vifaa vya kujikinga kama vile barakoa, chanjo na vingine vya kufanyia uchunguzi kumekwamisha hoja ya msingi ya kuwepo kwa uwiano na hivyo kuweka mazingira bora kwa aina au lahaja mpya za virusi kuibuka,” amesema Dkt. Tedros.

Jambo lingine ni kuenea kwa taarifa za uongo na zile za kupotosha mambo ambayo yanapeleka mrama mafanikio ya sayansi na kuamini mbinu za ukweli za kuokoa maisha.

Mwelekeo 2022

Ameeleza kuwa ingawa mwaka 2021 imekuwa na changamoto, “nasihi kila mtu aweke azimio lake la mwaka mpya wa 2022 kufanikisha lengo la kupatia chanjo asilimia 70 ya wanaopaswa kuchanjwa dhidi ya COVID-19 ifikapo katikati ya mwaka 2022.

Dkt. Tedros amesema watu ambao hawajapatiwa chanjo wako hatarini zaidi kufariki dunia kutokana na aina mpya ya virusi vya COVID-19.

Amepongeza hatua mpya bunifu za kufikia jamii zilizo hatarini ili zipate chanjo akitolea mfano mipango inayoanzia kwenye jamii na kuwashirikisha wananchi na kuwafikia kwa magari ya kutoa chanjo popote waliko.

Amesema WHO kwa upande wake itasaidia nchi ambazo ziko tayari kuimarisha mipango yao ya kutoa chanjo za Corona kwa wananchi sambamba na zile chanjo zilizo kwenye kampeni za kawaida.