Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua mpya zahitajika kukabiliana na matatizo ya afya ya akili kazini:WHO/ILO 

Changamoto za afya ya akili katika maeneo ya kazi
WHO
Changamoto za afya ya akili katika maeneo ya kazi

Hatua mpya zahitajika kukabiliana na matatizo ya afya ya akili kazini:WHO/ILO 

Afya

Hatua madhubuti zinahitajika ili kukabiliana na changamoto za afya ya akili miongoni mwa wafanyakazi , kwa mujibu wa wito mpya  wa pamoja uliotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO na lile la kazi duniani ILO. 

Machapisho mawili ambayo yote yanalenga ujumbe mmoja wa kushughulikia changamoto ya afya ya akili kazini  ambayo ni muongozo mpya wa kimataifa wa WHO kuhusu afya ya akili na uwajibikaji kazini na tamko la pamoja la kisera la WHO na ILO, yanakadiria kwamba takriban siku bilioni 12 za kazi hupotea kila mwaka kutokana na matatizo ya msongo wa mawazo na wasiwasi vinaougharimu uchumi wa dunia karibu dola trilioni 1. 

Mwongozo huo mpya wa kimataifa wa WHO kuhusu afya ya akili kazini unapendekeza hatua za kukabiliana na hatari ya afya ya akili kama vile mzigo mkubwa wa kazi, tabia mbaya na mambo mengine ambayo husababisha adha kazini.  

Kwa mara ya kwanza WHO inapendekeza mafunzo ya mameneja, ili kuwajengea uwezo wa kuzuia mazingira ya kazi yenye kuongeza shinikizo na kushughulikia ipasavyo na wafanyakazi walio katika changamoto. 

Ripoti ya kimataifa ya WHO kuhusu afya ya akili iliyochapishwa mwezi Juni 2022 ilionyesha kuwa watu bilioni 1 walikuwa wanaishi na matatizo ya afya ya akili mwaka 2019 , na asilimia 15 ya watu wazima wenye umri wa kufanya kazi walipitia matatizo ya afya ya akili. 

Wakimbizi na wahamiaji wanakabiliwa na sababu nyingi zinazoathiri afya yao ya akili na ustawi wao
© WHO/Ploy Phutpheng
Wakimbizi na wahamiaji wanakabiliwa na sababu nyingi zinazoathiri afya yao ya akili na ustawi wao

Chachu za changamoto za afya ya akili 

WHO imesema kazi huongeza changamoto za kijamii ambazo zinaathiri vibaya afya ya akili. Masuala ya ubaguzi na ukosefu wa usawa, uonevu na unyanyasaji wa kisaikolojia ni malalamiko makubwa ya unyanyasaji wa mahali pa kazi ambayo yana athari mbaya kwa afya ya akili limeongeza shirika hilo lakini kujadili au kuzungumzia masuala ya afya ya akili bado ni mwiko katika mipangilio ya kazi ulimwenguni kote. 

Mwongozo huo pia unapendekeza njia bora zaidi za kushughulikia mahitaji ya wafanyikazi walio na changamoto za afya ya akili, kama vile kupendekeza hatua zitakazowasaidia kurejea kazini na kwa wale walio na hali mbaya ya afya ya akili, na kuweka mikakati ya hatua zitakazowawezesha kuingia katika ajira ya kulipwa.

Muhimu zaidi, miongozo inataka uingiliaji kati unaolenga kulinda afya ya akili ya wahudumu wa afya, wahudumu wa kibinadamu na wahudumu wa dharura. 

Kwa mujibu wa Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus mkurugenzi mkuu wa WHO "Ni wakati wa kuzingatia athari mbaya ambazo kazi inaweza kuwa nazo kwa afya yetu ya akili. Ustawi wa mtu binafsi ni sababu tosha ya kuchukua hatua, lakini afya mbaya ya akili inaweza pia kuwa na athari ya kudhoofisha utendaji kazi na tija ya mtu. Miongozo hii mipya inaweza kusaidia kuzuia tamaduni na hali mbaya za kazi na kutoa ulinzi unaohitajika sana wa afya ya akili na usaidizi kwa watu wanaofanya kazi.” 

Mahala pa kazi mjini Shangai China
Zhu Xiaoyi
Mahala pa kazi mjini Shangai China

Tamko la kisera la WHO na ILO 

Tamko la pamoja la kisera la WHO na ILO linafafanua miongozo ya WHO katika suala la mikakati ya kiutendaji kwa serikali, waajiri na wafanyakazi, na mashirika yao, katika sekta za umma na za kibinafsi.  

Lengo ni kusaidia uzuiaji wa hatari za afya ya akili, kulinda na kukuza afya ya akili kazini, na kusaidia wale walio na matatizo ya afya ya akili, ili waweze kushiriki na kustawi katika ulimwengu wa kazi.  

Tamko hilo limeongeza kuwa uwekezaji na uongozi utakuwa muhimu katika utekelezaji wa mikakati hiyo. Akisisitiza kuhusu hilo Guy Ryder, mkurugenzi mkuu wa ILO amesema "Watu wanatumia sehemu kubwa ya maisha yao kazini hivyo mazingira salama na yenye afya ya kufanya kazi ni muhimu. Tunahitaji kuwekeza ili kujenga utamaduni wa kuzuia matatizo ya afya ya akili kazini, kuunda upya mazingira ya kazi ili kukomesha unyanyapaa na kutengwa kwa jamii, na kuhakikisha wafanyakazi walio na matatizo ya afya ya akili wanahisi kulindwa na kuungwa mkono.” 

Taratibu za kisheria zilizopo 

Katika eneo la Tambakunda mfanyakazi wa IOM anamueleza chifu wa kijiji mchakato wa kuelezea mahitaji ya watu wenye matatizo ya afya ya akili wanaohitaji huduma zaidi za afya
IOM/Robert Kovacs
Katika eneo la Tambakunda mfanyakazi wa IOM anamueleza chifu wa kijiji mchakato wa kuelezea mahitaji ya watu wenye matatizo ya afya ya akili wanaohitaji huduma zaidi za afya

Mkataba wa ILO wa usalama na afya kazini (Namba 155) na pendekezo (Namba 164) hutoa mifumo ya kisheria ili kulinda afya na usalama wa wafanyakazi.  

Hata hivyo, Atlas ya afya ya akili ya WHO imegundua kuwa ni asilimia 35% tu ya nchi ndizo zilizoripoti kuwa na programu za kitaifa za kukuza na kuzuia matatizo ya afya ya akili yanayohusiana na kazi. 

WHO na ILO wamesema janga la COVID-19 limesababisha ongezeko la asilimia 25% la wasiwasi na msongo wa mawazo ulimwenguni kote, likifichua jinsi serikali ambazo hazikujiandaa kwa athari za janga hilo kwa afya ya akili, na kufichua uhaba wa kimataifa wa rasilimali za kushughulikia afya ya akili.  

Mwaka 2020, serikali ulimwenguni kote zilitumia wastani wa asilimia 2% tu ya bajeti zake za afya kwa ajili ya afya ya akili, huku nchi za kipato cha chini zikitenga chini ya 1% ya bajeti zake kwa ajili hiyo.