Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi Hoima, Uganda, waishukuru UN kwa ulinzi mwaka 2021

Wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakisherehekea siku ya wakimbizi duniani, huko Hoima nchini Uganda.
UN/ John Kibego
Wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakisherehekea siku ya wakimbizi duniani, huko Hoima nchini Uganda.

Wakimbizi Hoima, Uganda, waishukuru UN kwa ulinzi mwaka 2021

Wahamiaji na Wakimbizi

Kuelekea mwaka mpya wa 2022 wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wanaoishi katika makazi ya wakimbizi ya Kyangwali wilaya ya Hoima nchini Uganda wametoa shukrani zao kwa Umoja wa Mataifa huku wakiomba usaidizi zaidi mwaka ujao wakati huu ambapo bado kuna changamoto za kimaisha zinazosababishwa na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.
 

Miongoni mwa wakimbizi hao ni Benjamini Basebanya ambaye anazungumzia changamoto alizokumbana nazo akisema, “unajua shule zimefungwa, hakuna pes ana watu hawafanyi kazi kwa kuwa wamezuiwa kutokana na ugonjwa wa COVID-19. Mipango ilikuwa mingi tulikuwa tunajaribu kupata elimu zaidi angalau mwaka ujao tutakuwa kiwango Fulani cha masomo, lakini shule zimefungwa.”
Hata hivyo amesema tangazo la serikali ya kwamba shule zitafunguliwa mwaka ujao ni mpango mzuri kwa kuwa wakati huu wa kufungwa shule baadhi ya vijana wameharibika na kutumbukia kwenye ulevi.

“Kifedha tuko chini sana kutokana na COVID-19 lakini tuko tayari kurejea shuleni. Unajua kutokuwepo shuleni wasichana wadogo wameolewa, wavulana wadogo wameoa na kuangalia miaka miwili hawajasoma na wanaona ndio mwisho wa maisha,” amesema Benjamin.

Alipoulizwa wito wake kwa viongozi wa Uganda na Umoja wa Mataifa mkimbizi huyo kutoka DRC amesema “ni kuwashukuru sana kwa sababu kiusalama tumelindwa tuko salama. Labda wajitahidi zaidi sana kiukweli msaada tumepunguzwa sana, tuko hapa na hatuna kazi. UNHCR ndio imetulinda hapa. Watuongezee, watusaidie watuongezee fedha za chakula awali tulipata shilingi 31,000 za Uganda na sasa tunapata shilingi 13,000 za Uganda. Fedha imepunguzwa sana.”

Mkimbizi mwingine hapa Kyangwali ni Faraja Lanem wa Kijiji cha Kasonga ambaye amesema “mwaka 2021 tumepata shida ya COVID-19 lakini tumepata ulinzi kutoka UNHCR kwani walitupatia chanjo. Tunashukuru sana. Shida sasa wakati wa Corona ni uhaba wa chakula, mashamba hatuna tena na hata fedha tumepunguziwa.”

Kwa upande wake kijana Clement Faustine anasema “tulikuwa tunaendelea vizuri lakini baadaye maendeleo yakaporomoka, biashara ikashuka. Serikali na UNHCR walitulinda sana wakati wa COVID-19 ilipokuwa mbayá sana. Walitupatia barakoa tunashukuru sana.”

Jane Nyarugendo akiwa na mwanae kwenye makazi ya wakimbizi ya Kyangwali nchini Uganda. Jane ambaye ni mkimbizi wa ndani amenufaika na mradi wa UN-women wa uwezeshaji wanawake.
UN/ John Kibego
Jane Nyarugendo akiwa na mwanae kwenye makazi ya wakimbizi ya Kyangwali nchini Uganda. Jane ambaye ni mkimbizi wa ndani amenufaika na mradi wa UN-women wa uwezeshaji wanawake.

Tabu Mawazo naye kutoka DRC anasema “ jinsi mimi niko hapa nafanya biashara, nakuwa makini na hii COVID-19 kwa kuwa huwezi tu kukaa nyumbani ukisema utapata Corona. Mimi nashukuru Mungu jinsi ananipitisha kwenye hii COVID-19 na mimi najua hii miaka inakuja miaka itakuwa vizuri kwa kuwa wametupatia chanjo.”

Msimamizi wa makazi ya wakimbizi ambaye ni mwakilishi wa ofisi ya Waziri Mkuu Johnbosco Kyaligonza aneleeza jinsi COVID-19 ilivyoathiri ulinzi wa wakimbizi akisema, “bila shaka maingiliano yetu nao pamoja na wadau wetu yalikatishwa kama njia ya kudhibiti COVID-19 mikutano yote iliahirishwa na hatungeweza kuwafikia wlala wao kutufikia kwa urahisi wakati huo. Hali hiyo kwa njia moja iliathiri ulinzi wetu kwao.”

Hata hivyo anasema wataendelea kupokea wasaka hifadhi akisema, “agizo la Rais kuhusu kufungwa kwa  mipaka bado linatekelezwa. Lakini kutokana na kuwepo kwa mipaka isiyodhibitiwa hauwezi kufahamu wanakopitia, unaona tu wamefika ofisini na wakishafika hapa hatuna haki ya kuwafukuza na kuwarejesha nchini mwao bali tunawakaribisha na kuwapatia kuwapatia ulinzi.”

Bwana Kyaligonza anatoa ombi la msaada kwa jamii ya kimataifa kutokana na ongezeko la wakimbizi akisema, “tunaomba wahisani kutoa msaada zaidi kwa wakimbizi kwani mahitaji ya wakimbizi yanaongezeka. WFP ilipunguza mgao wa chakula lakini idadi ya wakimbizi inaongezeka.

Mkuu wa ofisi ya Hoima ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) Uganda ni Thomas Faustini, anawahakikishia ulinzi wakimbizi wote. “ujumbe pekee kwa wakimbizi ikizingatiwa kuwa hapa tunaishi kindugu na kwa amani na jamii za wenyeji, naahidi kuwa UNHCR itaendelea kuwepo hapa na kutoa huduma kwa wakimbizi mwaka 2022.”

UNHCR Uganda na ilivyodhibiti COVID-19 Kyangwali

Anaeleza jinsi walivyodhibiti mlipuko wa COVID-19 katika makazi haya ya Kyangwali akisema “tulihakikisha kwamba kuna pengo kati ya mtu na mtu badala ya mikusanyiko, pia tuliwapatia barakoa na kuweka vifaa vya kinga kama vile ndoo za maji ya kunawia mikono kwenye makazi ya wakimbizi na sehemu za mgao wa chakula.”

Na kisha akazungmuzia mbinu bunifu zinazotumika kuendeleza elimu miongoni mwa watoto wakiwa majumbani akisema, “tulisambaza nyenzo za wanafunzi kujisomea nyumbani na pia mafunzo ya wanafunzi katika vikundi vidogo vidogo katika jamii. Halikadhalika wadau wetu World Child Holland wameanzisha mafunzo ya majumbani kupitia kompyuta ndogondogo ambao ni mradi bunifu sana.”

Yote kwa yote anaipongeza serilali ya Uganda kwa ukarimu wake kwa wakimbizi akisema, “bila shaka kila wakati tunapenda  kuipongeza Uganda kwa será  yake ya kufungua milango kwa wakimbizi kwa miaka mingi sasa. Wakati COVID-19 iliposhamiri kulikuwa na mapigano DRC, wasaka hifadhi walikuwa wanakimbia licha ya  mipaka kufungwa lakini serikali ya Uganda ilitambua kuwa watu hao wanahitaji ulinzi.”