Ningalikataliwa kuingia Uganda, ningaliuawa – Mkimbizi kutoka DRC

Wakimbizi kutoka Sudan Kusini ambao wanasoma katika shule moja ya sekondari huko mjini Hoima nchini Uganda.
UN
Wakimbizi kutoka Sudan Kusini ambao wanasoma katika shule moja ya sekondari huko mjini Hoima nchini Uganda.

Ningalikataliwa kuingia Uganda, ningaliuawa – Mkimbizi kutoka DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

Tarehe 20 mwezi huu wa Juni ilikuwa ni siku ya wakimbizi duniani ambapo Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ilipata fursa ya kuzungumza na wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC walioko nchini Uganda.

Mmoja wao katika simulizi yake alisema, “Uganda isingalinifungulia mpaka, ningaliuawa,” na ndipo mwandishi wetu John Kibego akamuuliza kulikoni?

Mkimbizi huyo Dorica Alinda, mwanafunzi katika shule ya sekondari ya Destiny iliyoko Hoima nchini Uganda anaishi makazi ya wakimbizi ya Kyangwali. “Nimetoka mji wa Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC. Mimi mwanamke hawangekubali niingie Uganda, ningaliuawa,” anasema Dorica.

Anafafanua kuwa ubakaji kule umezidi na wanawake wananyanyaswa, “kwa kutusaidia kuingia hapa Uganda, tumepata usaidizi, na tumepata haki yetu kama wanawake, tofauti na DRC vita ilipoanza.”

Alipoulizwa kuhusu ujumbe wake kwa Umoja wa Mataifa na serikali ya Uganda na DRC, Dorica anasema, “kwa sababu wametusaidia, tumefika huku wametupokea, wanawake wanawapatia haki zao, naomba tu waendelee kutusaidia kwa sababu vita ingali ipo.”

Wanafunzi wakimbizi kutoka Sudan Kusini wakiwa kwenye shule iliyoko mji wa Hoima nchini Uganda.
UN
Wanafunzi wakimbizi kutoka Sudan Kusini wakiwa kwenye shule iliyoko mji wa Hoima nchini Uganda.

Nilikimbia risasi na mabomu! Nilinusurika- Faustine

Faustine Isaya yeye alitoka DRC mwaka 2009 alipoulizwa kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wakimbizi duniani, “ ni haki ya binadamu mtu kusaka usalama,” Faustine anasema hakika ni haki ya mtu kwa kuwa anasaka usalama akikumbuka alikotoka akisema, “kule kulikuwa vita kwa kuwa tulikutana nao waasi Katiguru na tulikimbia hadi Bunagana na serikali ya Uganda ikatukaribisha na kutuleta kwa kambi.”

Kijana huyu anasema kama si kupata fursa ya kuingia Uganda, watu wengi wangeuawa. “Nashukuru wamepatia wazazi shamba na pesa kidogo ya kusomesha watoto.”

Faustine kilio chake ni kwamba hivi sasa yeye na nduguye wanasoma, na mama yake amekuwa mzee na hana pesa ya kusomesha watoto. “Watusaidie kwa chakula kwa sababu wameleta wakimbizi kwenye shamba letu.”

Betty Najuisca, mwanafunzi pia mjini Hoima ana majonzi kwa kuwa, “nikitoka DRC nilikuwa na wazazi lakini mmoja aliuawa wakati wa vita. Tulitoka DRC tukakimbia, walikuwa wanapiga mabomu, watu wengi waliuawa. Hakuna uwezo wa kukaa pale kwa kuwa mapigano yalikuwa makali. Lakini mpakani walitupokea na kutuleta kambini.”

Ombi la Betty ni msaada zaidi kama chakula, karo ya shule na mahitaji mengine ya binadamu.

Iddi Mugenyi, raia wa Uganda anaunga mkono hatua ya serikali yake kukaribisha na kukirimu wageni akisema, “ni haki ya kila mtu kupata hifadhi kwa sababu kule wanakotoka kuna vita na mapigano. Wanakuwa kwenye mazingira yasiyo salama na hivyo wanatafuta usalama nchi nyingine.”

Uganda kuendelea kuacha mipaka wazi

Johnbosco Kyaligonza ni Kamandanti wa makazi ya wakimbizi ya Kyangwali na anasema Uganda itaacha mlango wake wazi kwa wasaka hifadhi huku Thomas Faustine , Mkuu wa ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi (UNHCR), Kyangwali anasema, “bila shaka tunapenda kushukuru serikali ya Uganda kwa será yake bora ya kuendelea kupokea wakimbizi. Wakati wa COVID-19 Uganda ilishirikiana nasi na kufungua mipaka na kupokea wakimbizi.