Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko yavuruga ndoto za wanawake wa Ziwa Albert, Uganda 

Agnes Ongyera, Afisa Ujasiriamali wa kikundi cha wajasiriamali wanawake cha Kaiso, KWG huko Hoima Uganda akionesha bidhaa wanazotengeneza.
UN/ John Kibego
Agnes Ongyera, Afisa Ujasiriamali wa kikundi cha wajasiriamali wanawake cha Kaiso, KWG huko Hoima Uganda akionesha bidhaa wanazotengeneza.

Mafuriko yavuruga ndoto za wanawake wa Ziwa Albert, Uganda 

Tabianchi na mazingira

Mbali na janga la Janga la Corona au COVID-19 ambalo limeikumba dunia kwa zaidi ya miaka miwili, wananchi wa Uganda waishio karibu na Ziwa Albert kwa miaka hiyo miwili wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ziada ya mafuriko.

Wanawake wanachama wa kikundi cha Kaizo Women’s Group (KWG) wilayani Hoima ni moja wapo ya vikundi ambayo mipango yao ilikwamishwa na atahri za mafuriko na ambao sasa wanaomba msaada wa kifedha kutoka serikali katika juhudi zao za kujikwamua kutokana na uharibifu wa maji huku wakikabiliana na janga la COVID-19.

Mwandishi wetu wa Uganda, John Kibego amefanya mahojiano na Ongyera Aness afisa wa ujasiriamali katika kikundi hicho cha KWG ambaye amamueleza “watu walikuwa wengi sana hapa Hoima kabla ya mafuriko lakini sasa watu wengi wamekimbia, kulikuwa na watu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo -DRC lakini wamekimbia wamerudi kwao sababu maisha yamekuwa magumu”

Aness anasema wakati serikali ilipotangaza kufunga biashara na mikusanyiko walikuwa na mipango mbalimbali na kubwa  walitumia agizo la serikali la kila mwananchi kuvaa barakoa kama fursa kwao wanakikundi.

Kituo cha afya cha Butyaba nchini Uganda kimetwama kwenye maji kutokana na ongezeko la maji kwenye ziwa Albert.
UN/ John Kibego
Kituo cha afya cha Butyaba nchini Uganda kimetwama kwenye maji kutokana na ongezeko la maji kwenye ziwa Albert.

“Tulianza kufundisha watu kushona barakoa na mwenyekiti wetu alitusimamia tukanunua malighafi yakutengenezea barakoa, tulikuwa tunashona kisha tunaenda kuuza na tulikuwa tunapata hela tunagawana kama tunapata elfu 5 mwenyeduka tunampatia 2500. Yule aliyekuwa anashona alikuwa anapata dawio lake kwa asilimia kadhaa na hela nyingine tunaweka kununua malighafi, na nyingine tunapata fedha ya kikundi.”

Lakini baada ya mafuriko kuja na watu kupoteza nyumba zao biashara hiyo iliharibika na mauzo yakashuka kabisa “Mtu hawezi kutoa pesa yake na kununua barakoa wakati hana hela ya kula kuokoa maisha yake.”Amesema afisa huyo wa kikundi cha KWG na kuongeza kuwa “Tulikuwa tunauza mavurushi ya barakoa ya elfu 50 kwa wiki lakini sasa tunauza barakoa tatu watu hakuna wa kununua”

Kikundi hicho kilikuwa kikitumia fedha wanazozipata katika shughuli zao kukopeshana wanakikundi na kurejesha pamoja na faida kidogo . pia walikuwa na vitegauchumi vingena kama kukodisha maturubai lakini sasa hivi hawapati wateja.

Kikundi hicho kimeiomba serikali iwasaidie kuwapatia fedha kidogo ili waone namna watakayo fanya katika kujitafutia riziki kwakuwa hapo awali walikuwa wanachangishana wenyewe kwa wenyewe lakini sasa hawana fedha.