Tuna hofu na ukatili wa kingono uliofanyika Sudan wakati wa maandamano- Patten

Waandamanaji wakikusanyika mbele ya Makao Makuu ya jeshi la Sudan mjini Khartoum (11 April 2019)
Masarib/Ahmed Bahhar
Waandamanaji wakikusanyika mbele ya Makao Makuu ya jeshi la Sudan mjini Khartoum (11 April 2019)

Tuna hofu na ukatili wa kingono uliofanyika Sudan wakati wa maandamano- Patten

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo, Pramila Patten amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya hali inayoendelea nchini Sudan kufuatia taarifa ya madai ya kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kingono na unyanyasaji wa kijinsia wakati wa maandamano yaliyofanyika nchini humo tarehe 19 mwezi huu wa Desemba.

Taarifa iliyotolewa hii leo jijini New  York, Marekani na ofisi ya mwakilishi huyo maalum wa Katibu Mkuu imesema vitendo hivyo vinadaiwa kufanywa na vikosi vya usalama dhidi ya wanawake na wasichana kwenye mji mkuu wa Sudan , Khartoum.

Siku hiyo ya maandamano walikuwa wanafanya kumbukumbu ya miaka mitatu tangu maandamano makubwa yaliyosababishwa kuondolewa madarakani kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Omar Al Bashir sambamba na kupinga mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka hu una makubaliano ya amani yaliyotiwa Saini tarehe 21 mwezi uliopita wa Novemba.

Bi. Patten ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya ripoti za uhakika za ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo vitendo vitendo vya ubakaji na ubakaji wa magenge kwa wanawake na wasichana ambavyo vilitumika kama mbinu ya kutawanya waandamanaji waliotaka kuketi kwenye kasri jioni ya tarehe 19 mwezi Desemba.

“Nina hofu Zaidi kwa kuwa baadhi ya manusura wa ukatili wa kingono waliowasilisha malalamiko yao mahakamani na kusaka matibabu baada ya matukio hayo wengine wameogopa kufanya hivyo wakihofia unyanyapaa na hofu ya visasi,” amesema Bi. Patten.

Ametaka kusitishwa mara moja kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na unyayasaji nchini Sudan huku akitoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua za makusudi ili manusura waweze kupata matibabu, Pamoja na usaidizi wa kisheria na kisaikolojia.

Halikadhalika Bi. Patten ametaka mamlaka zichukue hatua kuhakikisha vitendo kama hivyo havirudiwi tena na wahusika wawajibishwe kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2467 la mwaka 2019.
Kwa upande wa jamii ya kimataifa, ikiwemo Baraza la Usalama amesihi zitumie ofisi zao ili kuzungumza na viongozi wa Sudan kutaka kukomeshwa kwa ghasia na vitisho dhidi ya raia.