Ghasia zikisababisha vifo Sudan, Bachelet ataka serikali ichukue hatua

17 Januari 2019

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya ghasia zinazoendela nchini Sudan ambazo hadi sasa zimesababisha kuuawa kwa watu 24 na wengine wengi wamejeruhiwa.

Ghasia hizo zinatokana na maandamano yaliyoanza tarehe 16 mwezi uliopita kwenye miji mbalimbali nchini Sudan ambapo waandamanaji wanapinga ongezeko la bei za bidhaa.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema kuwa kuna taarifa za uhakika ya kwamba vikosi vya usalama vinatumia nguvu kupita kiasi ikiwemo silaha za moto dhidi ya waandamanaji, hali ambayo inatia wasiwasi mkubwa.

Akihojiwa mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Ravina Shamdasani amesema, “vikosi vya usalama wanafuata waandamanaji hadi hospitali ya Omdurman na kufyatua risasi pamoja na mabomu ya kutoa machozi. Hii kwa uhakika haikubaliki, tunatoa wito kwa mamlaka zihakikishe kuwa haki ya watu kukusanyika na kuandamana kwa amani inalindwa bila kujali mirengo yao ya kisiasa.”

Msemaji huyo amemnukuu Kamishna Bachelet akisema kuwa, "kuna malalamiko ya kweli lakini si kwamba tunasema ni rahisi kupatia majibu. Lakini jawabu kandamizi linaweza kufanya malalamiko hayo kuwa mabaya zaidi.”

Amesema Sudan ni mwanachama wa mikataba ya kimataifa hivyo ilinde waandamanaji badala ya kuwashambulia na itatua mkwamo unaoendelea kwa njia ya mazungumzo.

Kamishna Mkuu amesema anatambua kuwa serikali pamoja na tume ya taifa ya haki za binadamu wameanzisha kamati za kusaka ukweli wa kinachoendelea, lakini ni vyema uchunguzi huo ufanyike haraka, kwa kina na kwa uwazi kwa lengo la kuwajibisha wahusika.

Halikadhalika amesihi wale wote waliokamatwa kiholela wakati wakitekeleza haki yao ya kuandamana waachiliwe huru haraka na haki zao zilindwe.

Serikali ya Sudan imethibitisha kuwa hadi tarehe 6 mwezi huu watu 816 walikuwa wamekamatwa kuhusiana na maandamano hayo yaliyoitishwa na vyama vya upinzani na miongoni mwao ni waandishi wa habari, viongozi wa vyama vya upinzani na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter