WFP kupunguza mgao wa chakula kwa wayemen kuanzia  mwezi ujao, kisa? Ukata!

22 Disemba 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP hii leo limeonya kuwa linaendelea kukumbwa na uhaba wa fedha za kuendesha operesheni zake za  kusambaza msaada wa chakula kwa watu milioni 13 nchini Yemen na kwa hiyo litalazimika kupunguza mgao wa chakula kwa baadhi ya wananchi kuanzia mwezi ujao wa Januari.

Mkurugenzi wa WFP kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Corinne Fleischer amefafanua kupitia taarifa iliyotolewa leo mjni Sana'a Yemen kuwa kuanzia mwezi ujao, watu milioni 8 watapunguziwa mgao ilihali watu milioni 5 walio katika hatari ya kutumbukia kwenye baa la njaa wataendelea kupata mgao kamili.

WFP inasema punguzo hilo la mgao wa chakula linakuja wakati mbayá kwa famila za Yemen ambazo tayari zinategema msaada wa chakula kutoka shirika hilo ili ziweze kuishi.

Katika kipindi cha miezi mitatu, uhaba wa mlo wa kutosha ambacho ni moja ya kipimo kinachotumiwa na WFP katika kufuatilia njaa, umeongezeka kwa kasi kubwa na kuathiri nusu ya familia wakati huu ambapo thamani ya sarafu ya Yemen inashuka na mfumuko wa bei unachochea kuporomoka kwa uchumi.

Kama hiyo haitoshi, mapigano nayo yanashamiri katika maeneo mbalimbali nchini Yemen na kuendelea kulazimisha familia kukimbia makazi yao.

“Kila wakati tunapopunguza mgao wa chakula tunatambua kuwa watu wengi zaidi ambao tayari wanakabiliwa na njaa, wataendelea kukosa chakula na hivyo kuungana na wengine wengi ambao wanakumbwa na njaa hivi sasa,” amesema Fleischer na kuongeza kuwa licha ya nyakati hizi ngumu bado wanalazimika kutumia rasilimali kidogo walizo nazo kukidhi mahitaji ya chakula.

Mwakilishi huyo wa WFP anasema kama hali ya ukata itaendelea, mgao zaidi wa chakula utalazimika kupunguzwa sambamba na huduma za mgao wa vyakula shuleni na tiba dhidi ya utapiamlo kwa Watoto.

Zaidi ya watu milioni 16.2 nchini Yemen, sawa na nusu ya wakazi wote wa taifa hilo wanakabiliwa na njaa kali. Nusu ya Watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano nao wako hatarini kukumbwa na utapiamlo mkali.

Ni kwa mantiki hiyo WFP inahaha kupata dola milioni 813 ili iweze kuendelea kutoa msaada wa chakula kwa walio hatarini zaidi nchini Yemen, fedha ambazo zitawasogeza hadi mwezi Mei.
Na kwa mwaka mzima wa 2022, WFP itahitaji dola bilioni 1.97 ili kutoa misaada muhimu kwa familia zinazokabiliwa na njaa nchini Yemen.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter