Janga la njaa Yemen ndio baya zaidi kusababishwa na binadamu katika historia:UNFPA

1 Novemba 2018

Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani, UNFPA kanda ya eneo la Waarabu amesema baa la njaa linalonyemelea nchini Yemen linaweza kuwa ndio baya zaidi kuchangiwa na binadamu katika historia ya karibuni.

Dkt. Luay Shabaneh, katika tarifa yake iliyotolewa hii leo amesema baa hilo linakadiriwa kuweza kuwaweka wanawake milioni mbili wanaonyonyesha na wajawazito katika hatari kubwa ya kifo.

UNFPA imetaja ukosefu wa chakula, watu kutawanywa, lishe duni, milipuko ya magonjwa na kuporomoka kwa huduma za afya vimeathiri kwa kiasi kikubwa afya na mustakabali wa wanawake milioni 1.1 wanyonyeshao na wajawazito na kusababisha visa vingi vya watoto kuzaliwa njiti, watoto kuzaliwa na uzito mdogo, wanawake kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua na mchakato wa uchungu wa kujifungua unaoweka rehani maisha yao.

Kwa mujibu wa shirika hilo karibu nusu ya vituo vya afya havifanyi kazi Yemen, vikiwemo vinavyotoa huduma ya afya ya uzazi ambayo vinapaswa kuwapima na kuwapatia tiba wanawake.

Ingawa ukata ndio changamoto kubwa kwa shirika la UNFPA, Dkt. Shabaneh amesema shirika hilo linasaidia vituo vya afya 184 vinavyotoa huduma ya afya ya uzazi na ambavyo viko mashakani kushindwa kutoa huduma hizo endapo fedha zaidi za ufadhili hazitopatikana.

 

TAGS: UNFPA, Njaa, Yemen, msaada, wanawake,

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter