Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziara ya viongozi wa dini kwa wakimbizi wa ndani Tambura nchini Sudan Kusini yawajengea matumaini

Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini
UNMISS
Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini

Ziara ya viongozi wa dini kwa wakimbizi wa ndani Tambura nchini Sudan Kusini yawajengea matumaini

Wahamiaji na Wakimbizi

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umefanya ziara na viongozi wa dini kuwatembelea wakimbizi wa ndani walioko Nagero huko Tambura li kuweza kuwajengea matumaini lakini pia kusikiliza mahitaji yao.

Helikopta ya walinda amani ya Umoja wa Mataifa ikiruka juu ya mji wa Nagero katika Jimbo la Equatoria Magharibi, waliomo ndani ya usafiri huo ni ujumbe wa maaskofu wanne kutoka baraza la makanisa la Sudan Kusini ambao wanasafiri kuepeleka ujumbe wa mshikamano, matumaini na amani kwa familia zilizokimbia makazi yao baada ya kuzuka ghasia huko Tambura.

Walipofika katika kambi ya wakimbizi wa ndani wamekaribishwa kwa kujionea kwa macho yao hali ilivyo mbaya. Watu hawa hawana maji safi, chakula, hospitali, au shule kwa ajili ya watoto wao. Nguo zao zikiwa zimechanika. 

Jocye Peter, mama wa watoto sita, alitembea kwa siku nne kukimbia mapigano mapema mwezi Juni, kambini hapa Nagero anapata angalau aina fulani ya usalama.

“Baadhi ya majirani zangu waliuawa hivyo niliamua kukimbilia hapa na watoto wangu, nikimuacha mume wangu. Tunapokaa hapa, tunakufa njaa. Hatuna hata vyombo. Pia tunaugua magonjwa na hakuna dawa hospitalini hapa Nagero. Wakati mwingine tunaweza kupata dawa, kama paracetamol, labda vidonge viwili au vitatu. Ikiwa haisaidii, basi tunachagua dawa za kienyeji. Hapa hata maji ni shida.”

Akitoa maneno ya tumaini na faraja kwa wananchi hawa, Askofu mstaafu, Arkanjelo Wani Lemi, anasema viongozi wa dini wanashikamana na jamii ya eneo hilo. “Tumekuja hapa ili tuweze, si tu kuwasikiliza, bali pia kuomba pamoja nao. Tumekuja ili turudishe matumaini kwa sababu watu walio katika hali ya namna hii ambao wameacha nyumba zao, hali ya kutokuwa na tumaini inaonekana kutanda, na kwa hiyo tumekuja kuwatia moyo. Tumekuja kuwapa ushauri  waweze kuishi kwa amani baina yao na kutafuta amani na machaguo bora ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo kama njia bora ya upatanishi baina yao.”

Mzozo tuu ulipoanza UNMISS ilichukua hatua za haraka kwa kuanzisha kituo cha muda hapa Tambura kwa ajili ya kutoa ulinzi, kuzuia vurugu na kuwajengea amani wananchi kama anavyoeleza Stella Abayomi Afisa wa masuala ya kiraia wa UNMISS.

“Sisi UNMISS, tutaendelea kwenda kuzitembelea hizi jumuiya. Tunaendelea kuhamasisha jamii juu ya amani. Tunaendelea pia kuangalia jinsi wanavyoishi. Tunawauliza wanaendeleaje? Je, ni mambo gani yakifanyika wanafirikiri yanaweza kuwasaidia kurejea katika hali ya kawaida na ni mambo gani wanayotarajia kutoka kwa jamii, asasi za kiraia, na hata UNMISS tunapaswa kufanya ili kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida. Kwa hiyo, tunaendelea kwenda katika maeneo hayo ili kuwahakikishia wanajamii hawa na kuwajengea imani na taratiiibuu wanaanza kurejea katika hali yao ya zamani kabla ya kuyakimbia makazi yao sababu ya machafuko.”

Ujumbe wa kulinda amani Sudan Kusini umeahidi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wa kidini na washikadau wengine wote ili kusaidia jamii hizi za wahamiaji wa ndani ili waweze kumaliza migogoro inayowakabili na kupata amani, kusudi kubwa likiwa ni kuwawezesha kujenga upya maisha yao na kuwa na matumaini ya maisha bora ya baadaye.