Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Washindi wa tuzo ya mazingira ya UNEP mwaka 2021 watangazwa

Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) 2021 Mabingwa wa Dunia.
UNEP
Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) 2021 Mabingwa wa Dunia.

Washindi wa tuzo ya mazingira ya UNEP mwaka 2021 watangazwa

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira duniani UNEP leo limewatangaza washindi wanne wa tuzo yake ya juu kabisa ya mazingira ijulikanayo kama “champions of the Earth Award” kwa mwaka 2021.

Mashujaa hao wanne wa mazingira waliojitwalia tuzo ya UNEP ni pamoja na Waziri mkuu wa Barbados Mia Motteley ambaye ameshinda katika upande wa sera na uongozi kwa sauti yake ya kuchagiza dunia endelevu na kuweka bayana hatari inayozikabili nchi za visiwa vidogo zinazoendela ikiwemo nchi yake ya Barbados ambayo sasa imegeukia nishati mbadala, imeahidi kuachana na mafuta kisukuku na kuingia katika sekta endelevu ya usafiri. 
 
Mwingine ni mwanasayansi Dkt. Gladys Kalema-Zikusoka kutoka Uganda ambaye ameshinda upande wa sayansi na ubunifu, akiwa ni Daktari wa kwanza wa wanyama pori katika mamlaka ya wanyapori nchini Uganda  na mtaalam anayetambulika kimataifa katika masuala ya nyani na magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wananyama kwenda kwa binadamu au zoonotic .

Washindi wengine ni wanawake kutoka jamii ya watu wa asili wajulikanao kama “Sea women of Melanesia” wakijumuisha wanawake kutoka Papua New Guinea na visiwa vya Solomon, wameshinda tuzo katika upande wa uchagizaji na kuchukua hatua kutokana na mchango wao wa kuwapa mafunzo wanawake kutoka jamii za asili ya kufuatilia na kutathimini athari za kubabuka kwa matumbawe wakitumia sayansi ya bahari na teknolojia. 

Msitu wa Unamat huko Puerto Maldonado, Peru.
CIFOR/Marco Simola
Msitu wa Unamat huko Puerto Maldonado, Peru.

Na mshindi wa mwisho ni Maria Kolesnikova kutoka Jamhuri ya Kyrgystan aliyeshinda upande wa mtazamo wa ujasiriamali. Ni mwanaharakati wa mazingira, mchagijazi wa masuala ya vijana na mkuu wa shirika la Movegreen linalofuatilia na kuboresha hali ya hewa Asia ya Kati. 

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa UNEP Inger Anderson washindi hawa wanapewa tuzo hiyo kutokana na mchango wao ulioleta mabadiliko makubwa katika masuala ya mazingira na uongozi wao katika kusongesha mbele hatua madhubuti kwa niaba ya watu na sayari dunia. 

Pia amesema “Wanatetea, kuhamasisha na kuchukua hatua kukabiliana na changamoto kubwa kabisa za mazingira katika zama zetu ikiwemo ulinzi wa mifumo ya maisha na ufufuaji wake.” 

Bi. Anderson ameenda mbali zaidi na kuongeza kuwa“ Washindi wa tuzo ya mwaka huu ni wanawake ambao sio tu wanatuhamasisha lakini pia wanatukumbusha kwamba tunazo suluhu mikoni mwetu , tuna ujuzi na teknolojia ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi na kuepuka zahma kubwa.”