Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya mazingira safi na yenye afya: Mambo 6 unayohitaji kufahamu

Takriban watu 50,000 wameathirika na mafuriko katika mkoa wa Gatumba nchini Burundi kwa mwaka uliopita
© UNICEF/Karel Prinsloo
Takriban watu 50,000 wameathirika na mafuriko katika mkoa wa Gatumba nchini Burundi kwa mwaka uliopita

Haki ya mazingira safi na yenye afya: Mambo 6 unayohitaji kufahamu

Tabianchi na mazingira

Tarehe 8 Oktoba, sauti ya makofi makubwa na yasiyo ya kawaida ilisikika karibu na chumba cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi. Vita vilivyopiganwa kwa miongo kadhaa na wanaharakati wa mazingira na watetezi wa haki, mwishowe vilizaa matunda. 

Kwa mara ya kwanza kabisa, Baraza la Umoja wa Mataifa ambalo kazi yake ni kukuza na kulinda haki za binadamu kote ulimwenguni, limepitisha azimio la kutambua upatikanaji wa mazingira yenye afya na endelevu kama haki ya kila mkazi ulimwenguni. 

Azimio hilo pia limetaka nchi kufanya kazi pamoja, na na washirika wengine, kutekeleza mafanikio haya. 

"Kitaalamu labda hiyo ilikuwa uzoefu wa kusisimua zaidi ambao nimeupata au ambao nitawahi kuwa nao. Ulikuwa ushindi mkubwa wa timu. Ilichukua mamilioni ya watu, na miaka na miaka ya kazi kufanikisha azimio hili ", amesema David Boyd, Mwandishi Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu na Mazingira, ambaye alikuwa kwenye chumba cha mkutano wakati Rais wa Baraza hilo Nazhat Shameem kutoka Fiji, alipogonga nyundo mezani na kutangaza matokeo ya kupiga kura. 

Upigaji kura ulikuwa wa siri ambapo kura 43 za kuunga mkono na 4 za kukataa na kura zilihesabiwa kama ushindi na kupitisha maandishi ambayo yanataja juhudi za asasi za kiraia 1,100, watoto, vijana na asilia, ambao wamekuwa wakifanya kampeni ya kutambuliwa ulimwenguni, utekelezaji na ulinzi wa haki ya binadamu kwa mazingira salama, safi, yenye afya na endelevu. 

Lakini kwa nini utambuzi huu ni muhimu, na inamaanisha nini kwa jamii zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi? 
  
Haya ni mambo 6 muhimu unayohitaji kufahamu, yaliyokusanywa na sisi hapa kwenye Habari za UN.   

1. Kwanza, hebu tukumbuke kile Baraza la Haki za Binadamu linafanya, na maazimio yake yanamaanisha nini 

Baraza la Haki za Binadamu ni chombo kati ya serikali na mfumo wa Umoja wa Mataifa, unaohusika na kuimarisha, kukuza na kulinda haki za binadamu kote ulimwenguni na kushughulikia hali za ukiukaji wa haki za binadamu na kutoa mapendekezo juu yake. 

Baraza linaundwa na nchi 47 wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo huchaguliwa kwa wingi wa kura katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa – UNGA na zinawakilisha kila kanda ya ulimwengu. 

Maazimio ya Baraza la Haki za Binadamu ni  ya kisiasa ambayo yanawakilisha msimamo wa wanachama wa Baraza (au wengi wao) juu ya maswala na hali fulani. Nyaraka hizi zimetayarishwa na kujadiliwa kati ya Mataifa na kuendeleza masuala maalum ya haki za binadamu. 

Kwa kawaida huchochea mjadala kati ya mataifa, asasi za kiraia na mashirika ya serikali; kuanzisha ‘viwango vipya’, mistari au kanuni za mwenendo; au kuonyesha sheria zilizopo za mwenendo. 

Maazimio huandikwa na "kikundi cha msingi": Costa Rica, Maldives, Moroko, Slovenia na Uswisi, ndizo nchi ambazo zilileta azimio la 48/13 kwa kupitishwa kwake katika baraza, ikitambua kwa mara ya kwanza kuwa na hali safi, yenye afya na mazingira endelevu ni haki ya binadamu. 

Mabinti wakiwa wametoka kuteka maji mjini Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo
© UNICEF/Scott Moncrieff
Mabinti wakiwa wametoka kuteka maji mjini Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo

2.Lilikuwa azimio la miongo kadhaa likitengenezwa 

Mnamo mwaka wa 1972, ulifanyika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira huko Stockholm, ambao ulimalizika na tamko la kihistoria, ulikuwa wa kwanza kuweka masuala ya mazingira miongoni mwa masuala ya kutia wasiwasi kimataifa na kuashiria mwanzo wa mazungumzo kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea juu ya kiungo kati ya ukuaji wa uchumi, uchafuzi wa hewa, maji na bahari, na ustawi wa watu ulimwenguni kote. 

Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wakati huo, zilitangaza kuwa watu wana haki ya kimsingi ya "mazingira yenye ubora unaoruhusu maisha ya utu na ustawi," ikitaka hatua madhubuti. Walilitaka Baraza la Haki za Binadamu na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua. 

Tangu mwaka 2008, nchi ya Maldives ambayo ni ya kisiwa kidogo na inayoendelea, imekuwa mstari wa mbele kwenye kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, imekuwa ikiwasilisha maazimio kadhaa juu ya haki za binadamu na mabadiliko ya tabianchi, na katika muongo mmoja uliopita, juu ya haki za binadamu na mazingira. 

Katika miaka michache iliyopita, kazi ya Maldives na mataifa washirika wake, na vile vile mwandishi maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu na mazingira na asasi zisizo za kiserikali tofauti, wamekuwa wakisogeza jamii ya kimataifa kuelekea kutangazwa kwa haki mpya ya ulimwengu. 

Msaada kwa Umoja wa Mataifa kutambua haki hii ulikua wakati wa janga la COVID-19. Wazo hilo liliidhinishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Michelle Bachelet, pamoja na asasi za kiraia zaidi ya 1,100 kutoka kote ulimwenguni. Karibu nchi 70 kwenye Baraza la Haki za Binadamu pia waliongeza sauti zao kwenye wito wa kikundi kikuu cha baraza hilo juu ya haki za binadamu na mazingira kwa hatua hiyo, na mashirika 15 ya Umoja wa Mataifa pia yalituma tangazo la pamoja linalotetea hilo. 

"Kuongezeka kwa magonjwa yanayoibuka kikanda, dharura za mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa sumu unaoenea na upotezaji mkubwa wa bioanuwai kumeleta mustakabali wa sayari kwenye ajenda ya kimataifa", kundi la wataalam wa Umoja wa Mataifa limesema katika taarifa iliyotolewa mnamo Juni 2021, katika Siku ya Mazingira Duniani. 

Uchafuzi wa hewa huko Dhaka, Bangladesh, unaongoza msururu wa shida za kiafya kwa wakaazi wa jiji hilo.
© UNICEF/Habibul Haque
Uchafuzi wa hewa huko Dhaka, Bangladesh, unaongoza msururu wa shida za kiafya kwa wakaazi wa jiji hilo.

3. Ilikuwa ni hadithi ya Daudi dhidi ya Goliathi… 

Ili kufikia mwisho kura na uamuzi, kikundi kikuu huongoza mazungumzo mazito kati ya serikali, majadiliano na hata semina za wataalam, katika miaka michache iliyopita. 

Levy Muwana, wakili wa vijana na mtaalam wa mazingira kutoka Zambia, alishiriki katika moja ya semina hizo. “Kama mtoto mdogo, niliathiriwa na ugonjwa wa kuhara damu, ugonjwa wa vimelea, kwa sababu nilikuwa nikicheza kwenye maji machafu karibu na nyumba yetu. Miaka michache baadaye, msichana mmoja alikufa katika jamii yangu kutokana na kipindupindu. Matukio haya ni ya kawaida, chakusikitisha yanajitokeza mara nyingi zaidi. Magonjwa ya kuambukiza yanayotokana na maji yanaongezeka ulimwenguni, haswa kote kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya tabianchi", aliwaambia wanachama wa Baraza Agosti iliyopita. 

Muwana aliweka wazi kuwa hadithi yake haikuwa ya kipekee, kwani mamilioni ya watoto ulimwenguni wameathiriwa sana na athari mbaya za shida ya mazingira. "watu milioni 1.7 kati yao hufa kila mwaka kutokana na kuvuta pumzi hewa chafu au kunywa maji machafu", alisema. 

Mwanaharakati huyo, pamoja na zaidi ya watoto na washirika wanaunga mkono 100.000 walikuwa wamesaini ombi la haki ya mazingira bora kutambuliwa, na mwishowe walisikilizwa. 

"Kuna watu ambao wanataka kuendelea na mchakato wa kutumia ulimwengu wa asili na hawana mashaka juu ya kuwadhuru watu kufanya hivyo. Kwa hivyo wale wapinzani wenye nguvu sana wamezuia chumba hiki kuendelea mbele kwa miongo. Ni kama hadithi ya David na Goliathi kwamba asasi hizi zote za kijamii ziliweza kushinda upinzani huu wenye nguvu, na sasa tuna chombo hiki kipya ambacho tunaweza kutumia kupigania ulimwengu wenye haki na endelevu zaidi, "anasema David Boyd, Mwandishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu na Mazingira. 

4. Lakini lina faida gani, ni azimio lisilo la kisheria? 

Bwana Boyd anaelezea kuwa azimio linapaswa kuwa kichocheo cha hatua kubwa zaidi kwa kila suala moja la mazingira ambalo tunakabiliwa nalo. 

"Kwa kweli ni la kihistoria, na lina maana sana kwa kila mtu kwa sababu tunajua hivi sasa kwamba 90% ya watu ulimwenguni wanapumua hewa iliyochafuliwa. 

"Kwa hivyo mara tu ikiwa tunaweza kutumia azimio hili kama kichocheo cha vitendo vya kusafisha hali ya hewa, basi tutakuwa tukiboresha maisha ya mabilioni ya watu", anasisitiza. 

Maazimio ya Baraza la Haki za Binadamu hayawezi kuwa ya kisheria, lakini yana ahadi kubwa za kisiasa. 

"Mfano bora tulio nao wa tofauti gani maazimio haya ya Umoja wa Mataifa yanafanya ikiwa tutaangalia nyuma maazimio ya 2010 ambayo kwa mara ya kwanza ilitambua haki ya maji. Hicho kilikuwa kichocheo kwa serikali ulimwenguni kote ambao waliongeza haki ya maji kwa katiba zao, sheria zao za juu na zenye nguvu zaidi ", Bwana Boyd anasema. 

Mwandishi huyo ameaitaja Mexico, ambayo baada ya kuongeza haki ya maji katika katiba, sasa imepanua maji salama ya kunywa kwa jamii zaidi ya 1,000 za vijijini. 

"Kuna watu bilioni ambao hawawezi tu kufungua bomba na kuwa na maji safi, salama yanayotoka, na kwa hivyo unajua, kwa jamii elfu moja katika vijijini vya Mexico, huo ni uboreshaji kabisa wa kubadilisha maisha. Vivyo hivyo, Slovenia, baada ya kuweka haki ya maji katika katiba yao kwa sababu ya maazimio ya Umoja wa Mataifa, basi walichukua hatua kuleta maji salama ya kunywa kwa jamii za Warumi wanaoishi katika makazi yasiyokuwa rasmi nje kidogo ya jiji”. 

Kulingana na Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa -UNEP, kutambuliwa kwa haki ya mazingira bora katika kiwango cha ulimwengu kutasaidia juhudi za kushughulikia shida za mazingira kwa njia iliyoratibiwa zaidi, yenye ufanisi na isiyo ya kibaguzi, kusaidia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs, kutoa ulinzi mkali wa haki na wa watu wanaotetea mazingira, na kusaidia kuunda ulimwengu ambao watu wanaweza kuishi kwa amani na mazingira asilia. 

Wanafunzi wa shule ya msingi Lycée français jijini New York ( Shule ya Kifaransa) wakiandamana kuhusu mabadiliko ya tabianchi
Emmanuel Rouy/Lycée Français d
Wanafunzi wa shule ya msingi Lycée français jijini New York ( Shule ya Kifaransa) wakiandamana kuhusu mabadiliko ya tabianchi

5. Uhusiano kati ya haki za binadamu na mazingira hauwezi kupingika 

Bwana Boyd amejionea mwenyewe athari mbaya ambazo mabadiliko ya tabianchi tayari yameleta katika haki za watu. 

Katika safari yake ya kwanza kwenye nchi mojawapo kama Mwandishi Maalum, alikutana na jamii ya kwanza ulimwenguni ambayo ililazimika kuhamishwa kabisa kwa sababu ya kuongezeka kwa viwango vya bahari, mmomonyoko wa pwani na kuongezeka kwa nguvu ya dhoruba. 

"Unajua, kutoka paradiso hii nzuri ya ukingo wa maji kwenye kisiwa cha Fiji, ilibidi wahamishe kijiji chao chote kuelekea bara kilometa tatu za mraba. Wazee, watu wenye ulemavu, wanawake wajawazito, sasa wametenganishwa na bahari ambayo imedumisha utamaduni wao na maisha yao kwa vizazi vingi”. 

Hali hizi hazionekani tu katika nchi zinazoendelea. Bwana Boyd pia alitembelea Norway ambapo alikutana na wenyeji wa Sami pia wanaokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

“Nilisikia hadithi za kusikitisha sana huko. Kwa maelfu ya miaka utamaduni wao na uchumi wao umekuwa ukitokana na ufugaji wa nyumbu, lakini sasa kwa sababu ya hali ya hewa ya joto wakati wa baridi, hata huko Norway, kaskazini mwa ukanda wa Aktiki, wakati mwingine kuna mvua. 

"Nyama wa ng'ombe ambaye kwa maelfu ya miaka alikuwa ameweza kuondoa theluji wakati wa msimu wa baridi ili kuufikia ukungu uliofunikwa ambao uliwasaidia, sasa hawawezi kufuta barafu - na wanakufa na njaa".

Hadithi hiyo inajirudia nchini Kenya, ambako wafugaji wanapoteza mifugo yao kwa sababu ya ukame ambao unasababishwa na mabadiliko ya hali ya tabianchi. 

"Hawajafanya chochote kusababisha tatizo hilo la ulimwengu lakini wao ndio wanateseka, na ndio sababu ni suala la haki za binadamu. 

“Ndio maana ni suala la haki. Nchi tajiri na watu matajiri wanahitaji kuanza kulipia uchafuzi wa mazingira ambao wameusababisha ili tuweze kusaidia jamii hizi zilizo katika mazingira magumu na watu hawa walio katika mazingira magumu kubadilika na kujenga maisha yao ”, Bwana Boyd alisema 

Mabadilko ya tabianchi yanaathiri nchi nyingi ikiwemo Fiji iliyokumbwa na kimbunga mwaka 2016.
OCHA/Danielle Parry
Mabadilko ya tabianchi yanaathiri nchi nyingi ikiwemo Fiji iliyokumbwa na kimbunga mwaka 2016.

6. Nini kinafuata? 

Azimio la Baraza linajumuisha mwaliko kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia kuzingatia suala hilo. Mwandishi Maalum anasema ana "matumaini kwa uangalifu" kwamba Baraza hilo litapitisha azimio kama hilo mwaka ujao. 

“Tunahitaji hii.Tunahitaji serikali na tunahitaji kila mtu ahame katika hali ya uharaka. Namaanisha, tunaishi katika hali ya hewa, bioanuwai, na shida ya uchafuzi wa mazingira, na pia shida ya magonjwa haya yanayoibuka kama COVID-19 ambayo yana sababu za kimazingira. Kwa hiyo ndio sababu azimio hili ni muhimu sana, linaeleza kila serikali ulimwenguni 'lazima iweke haki za kibinadamu katikati ya hatua za hali ya hewa, uhifadhi, kushughulikia uchafuzi wa mazingira na kuzuia majanga ya magonjwa ya mlipuko ya baadaye"

Kwa Dkt. Maria Neira, mkuu wa masuala ya mazingira katika shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO, azimio hilo tayari lina athari muhimu na athari ya kuhamasisha. 

"Hatua inayofuata itakuwa ni jinsi tunavyotafsiri azimio hilo juu ya haki ya kusafisha hewa na ikiwa tunaweza kushinikiza, kwa mfano, kwa kutambuliwa kwa Miongozo ya Ubora wa Hewa Duniani ya WHO na viwango vya kuambukizwa kwa vichafuzi fulani katika ngazi ya nchi. Pia itatusaidia kusongesha sheria na viwango fulani katika ngazi ya kitaifa”, anaelezea. 

Uchafuzi wa hewa, haswa matokeo ya kuchoma mafuta, ambayo pia husababisha mabadiliko ya hali ya tabianchi, husababisha vifo 13 kwa kila dakika moja ulimwenguni. Dk Neira anataka kumalizika kwa "mapigano ya kipuuzi" dhidi ya mifumo ya ikolojia na mazingira. 

"Uwekezaji wote unahitaji kuwa katika kuhakikisha upatikanaji wa maji salama na usafi wa mazingira, kuhakikisha kuwa umeme unafanywa na nishati mbadala na kwamba mifumo yetu ya chakula ni endelevu." 

Kwa mujibu wa WHO, kufanikisha malengo ya Mkataba wa Paris kutaokoa mamilioni ya maisha kila mwaka kwa sababu ya kuboreshwa kwa hali ya hewa, lishe, na mazoezi ya mwili, kati ya faida zingine. 

“Dharura ya hali ya hewa imekuwa suala la kuishi kwa watu wengi. Ni mabadiliko ya kimfumo tu, makubwa na ya haraka yatakayowezesha kujibu mgogoro huu wa ikolojia duniani ", anasema Mwandishi Maalum. 

Kwa Bwana Boyd, idhini ya azimio la kihistoria katika Baraza la Haki za Binadamu ilikuwa wakati wa "kitendawili". 

"Kulikuwa na hali fulani ya kushangaza ya kufanikiwa na pia wakati huo huo hisia ya ni kazi ngapi zinabaki kufanywa kuchukua maneno haya mazuri na kuyatafsiri katika mabadiliko ambayo yatafanya maisha ya watu kuwa bora na kufanya jamii yetu iwe endelevu zaidi". 

Haki mpya iliyotangazwa ya mazingira yenye afya na safi pia itashawishi mazungumzo mazuri wakati wa mkutano ujao wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP26,  huko Glasgow, ambayo imeelezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kama nafasi ya mwisho ya 'kugeuza wimbi' na kumaliza vita dhidi ya sayari yetu.