Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tani bilioni 50 za mchanga na changarawe hutumika kila mwaka duniani:UNEP

Mfanyakazi wa kufyatua mchanga akiwa mahali pa kazi ya ujenzi ..
ILO/Apex Image
Mfanyakazi wa kufyatua mchanga akiwa mahali pa kazi ya ujenzi ..

Tani bilioni 50 za mchanga na changarawe hutumika kila mwaka duniani:UNEP

Tabianchi na mazingira

Mchanga na changarawe ni bidhaa muhimu sana na zinazoshika nafasi ya pili zinazotumika zaidi duniani kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP, na hivyo matumizi yake yanapaswa kufikiriwa  upya na kwa kina.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo “Mchanga na uendelevu: Mapendekezo 10 ya kimkakati ya kuepuka zahma” tani bilioni 50 za mchanga na changarawe zinazotosheleza kujenga ukuta wa upana wa mita 27 na urefu wa mita 27 kuzunguka dunia hutumika kila mwaka na hivyo kuzifanya rasilimali hizo kushika nafasi ya pili ya bidhaa zinazotumika zaidi baada ya rasilimali ya maji. 

UNEP inasema kutokana na utegemezi wa bidhaa hizo mchanga ni lazima utambuliwe kama rasilimali ya kimkakati na uchumbaji na matumizi yake vinahitaji kufikiriwa kwa makini. 

Ripoti hiyo inatoa mwongozo unaohitajika uliokusanywa kutoka kwa wataalamu kote duniani ili kubadili mbinu  za sasa na kutumia mpya zilizoboreshwa za uchimbaji na usimamizi wa rasilimali ya mchanga. 

Ripoti imeongeza kuwa uchimbaji wa mchanga katika maeneo ambako una jukumu muhimu kama vile kwenye mito, na kwenye mifumo ya ikolojia ya pwani au baharini, kunaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo, kujaa kwa chemichemi ya maji, kupoteza ulinzi dhidi ya mawimbi yaletwayo na dhoruba au vimbunga na athari kwa bayoanuai, hali ambayo ni tishio kwa uwezo wa watu kuishi, miongoni mwa mambo mengine , lakini pia kwa usambazaji wa maji, uzalishaji wa chakula, uvuvi, au katika sekta ya utalii. 

Kulingana na waandishi wa ripoti hiyo, mchanga lazima utambuliwe kama rasilimali ya kimkakati, sio tu kama nyenzo ya ujenzi, bali pia kwa majukumu yake mengi katika mazingira.  

Wamesisitiza kuwa serikali, viwanda na watumiaji wanapaswa kupanga bei ya mchanga kwa njia ambayo inatambua thamani yake halisi ya kijamii na kimazingira.  

Kwa mfano, wamesema kuweka mchanga ufukweni kunaweza kuwa mkakati wa gharama nafuu zaidi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na jinsi unavyolinda mazingira dhidi ya vimbunga na athari zitokanazo na kujaa kwa kina cha bahari, hivyo wanataka huduma kama hizo kujumuishwa katika thamani ya mchanga.