Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la COVID-19 laionesha dunia nguvu ya mitandao ya intaneti

Sehemu kubwa ya ukuaji mkubwa tangu 2019 umechangiwa na kuongezeka kwa matumizi ya mtandao katika nchi zinazoendelea, ambapo kupenya kwa mtandao kumekua kwa zaidi ya 13%.
WSIS Forum 2018 Photo Contest, Nagaland Tribe Connecting the World, India
Sehemu kubwa ya ukuaji mkubwa tangu 2019 umechangiwa na kuongezeka kwa matumizi ya mtandao katika nchi zinazoendelea, ambapo kupenya kwa mtandao kumekua kwa zaidi ya 13%.

Janga la COVID-19 laionesha dunia nguvu ya mitandao ya intaneti

Ukuaji wa Kiuchumi

Janga la COVID-19 limeweza kuionesha dunia nguvu ya mtandao wa intaneti na uwezo wake katika kubadilisha maisha ya watu mtandaoni, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika jukwaa maalum ya kujadili masuala ya mitandao ya intaneti nchini Poland. 

Tafiti zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka miwili tangu mwaka 2019 zaidi ya watu milioni 782 wameweza kuingia kwenye mtandao wa intaneti na kuutumia ijapokuwa kumekuwa na kasoro mbalimbali ikiwemo ufikiaji usio na usawa, kauli za chuki na uhalifu mitandaoni. 

Jukwaa la Umoja wa Mataifa la utawala wa mtandao linakutana kwa siku tatu kujadili namna ya kukabiliana na changamoto na hatari zinazojitokeza wakati wa kutumia mitandao.

"Janga la COVID-19 limeonesha  nguvu ya kubadilisha maisha iliyoletwa na mtandao. Teknolojia ya kidijitali imeokoa maisha kwa kuwezesha mamilioni ya watu kufanya kazi, kusoma na kushirikiana kwa usalama mtandaoni. Lakini janga hilo pia limekuza mgawanyiko wa dijitali na upande wa giza wa teknolojia: kuenea kwa haraka kwa habari potofu, udanganyifu wa tabia za watu na zaidi.Tunaweza tu kushughulikia changamoto hizi kwa umoja, kupitia ushirikiano ulioimarishwa." Amesema Katibu Mkuu Guterres.

Kauli mbiu ya jukwaa hilo ni Kuunganishwa na Mtandao inalenga kuongeza juhudi za pamoja ili kufikia ufikiaji wa wote na muunganisho wa maana, ushirikishwaji wa kiuchumi na ulinzi wa haki za binadamu mtandaoni.

Msichana mmoja mwenye umri wa miaka saba akisomea nyumbani wakati huu shule zimefungwa huko Georgia kwa sababu ya janga la COVID-19.
© UNICEF Georgia
Msichana mmoja mwenye umri wa miaka saba akisomea nyumbani wakati huu shule zimefungwa huko Georgia kwa sababu ya janga la COVID-19.

 

Akibainisha athari za janga la Corona katika mazingira ya kidijitali, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Uchumi na Masuala ya Kijamii Liu Zhenmin amesema "Jukwaa la Utawala wa Mtandao linatoa ahadi ya kuunda mustakabali wa kidijitali kwa ulimwengu, kugeuza janga la COVID-19 kuwa fursa. Hakika, hili ni rahisi kusema kuliko kufanya, kwani utawala wa mtandao wa kimataifa ni mgumu. Lakini kwa umoja tunaweza kufanikiwa kwa pamoja.”

Zhenmin ametolea mfano ajira za kijiditali katika Ukanda wa Kusini mwa Afroka zinakadiriwa kuwa milioni 230 ifikapo 2030 na zinaweza kuingiza mapato ya takriban dola bilioni 120, ikiwa ajira hizo zitasaidiwa na fursa za mafunzo milioni 650. 

Jukwaa hilo linafanyika Katowice, Poland, kuanzia tarehe 6 hadi 10 Disemba, linawaleta pamoja wavumbuzi zaidi ya 7,000, watendaji wakuu wa teknolojia, vijana, mawaziri na wabunge ili kuchochea juhudi za kujenga mustakabali wa kidijitali ulio wazi, salama na huria kwa wote.