Husisheni wadau kutoka kila nyanja mnapojadili kuhusu teknolojia ya intaneti-Guterres
Akihutubia mkutano wa jukwaa la usimamizi wa intaneti,IGF,unaofanyika hii leo mjini Paris Ufaransa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, katika miaka 13 tangu mkutano wa kimataifa uliofanyika Tunisia mwaka 2005, dunia ya kidijitali imebadilika kwa kasi, fursa mpya zimefunguka na hivyo masuluhisho ya kidijitali yanabadili maisha ya watu na kwamba yanaweza kusongesha mbele kazi ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
Licha ya faida hizo, Guterres pia ametahadharisha kuwa masuala mapya nayo yameibuka kuhusiana na usalama mitandaoni, data na akili bandia, mitandao ikitumika kueneza chuki,ukandamizi na udhibiti.
“Tunahitaji kuangalia mbali zaidi ya vichwa vya habari ili kuona jinsi gani intaneti na mitandao ya kijamii inavyoweza kutumiwa kugawanya watu, kuhamasisha ukabila na kueneza chuki.” Amesema Katibu Mkuu.
Guterres amesema kwa muda majukwaa yameanzishwa kujadili masuala haya na mengine na hivyo IGF inapaswa kufikiria itakavyoshiriki katika utatuzi.
Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameshauri kuwa wakati wadau wanajadili iwapo bado IGF inaendanda na hali ya sasa, wawahusishe wadau kutoka katika nyanja mbalimbali.
“Unapojadili data na akili bandia unaweza kuhitaji kuwaalika wanafilosofia, unaweza kuhitaji kuwaleta wana anthropolojia na wataalam ambao hawajajumuishwa katika mikutano ya kiteknolojia”
Aidha Guterres ametoa wito kuwa ni muhimu kupata habari kutoka kwa watu wenye ulemavu ambao ni miongoni mwa watumiaji wabunifu wa teknolojia za kidijitali. Pia akisisitiza ziwekwe juhudi za kuwafanya wanawake wasikike kwa kuwa wamekuwa hawawakilishwi ipasavyo katika katika masuala ya kiteknolojia.
Vile vile ameutaka mkutano wa IGF kutowasahau zaidi ya nusu ya wakazi wote duniani ambao bado hawajayafikia matumizi ya intaneti yenye tija.