Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhusiano baina ya mihadarati na mitandao ya kijamii lazima uvunjwe: INCB Ripoti

Rundo la dawa haramu za kulevya ( Kutoka maktaba)
© Commonwealth of Australia
Rundo la dawa haramu za kulevya ( Kutoka maktaba)

Uhusiano baina ya mihadarati na mitandao ya kijamii lazima uvunjwe: INCB Ripoti

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Bodi ya kimataifa ya kudhibiti madawa ya kulevya (INCB), ambayo ni chombo huru, kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, imetoa wito kwa serikali kufanya jitihada zaidi kudhibiti mitandao ya kijamii ambayo inasifu tabia mbaya zinazohusiana na madawa ya kulevya na kuchagiza mauzo ya bidhaa zinazodhibitiwa au kupigwa marufuku.

Katika ripoti yake ya kila mwaka, iliyotolewa leo, INCB imebainisha kuongezeka kwa ushahidi wa uhusiano kati ya umaarufu katika mitandao ya kijamii na matumizi ya dawa za kulevya, hulka ambayo huathiri vibaya vijana, ambao ni watumiaji wakuu wa majukwaa ya mitandao ya kijamii, na kundi rika lenye viwango vya juu vya watumiaji wa dawa za kulevya. 

Ripoti hiyo pia inatoa wito kwa sekta binafsi kudhibiti na kutathimini majukwaa yao na kupunguza utangazaji na uendelezaji wa matumizi yasiyo ya matibabu ya ya mihadarati.

Ripoti imeongeza kuwa pamoja na majukwaa ya mitandao ya kijamii, wahalifu wanatumia zana nyingine nyingi za kidijitali, kama vile sarafu za kidijitali, malipo ya simu na huduma za kielektroniki, ambazo hurahisisha uhamishaji wa fedha kimataifa na kwa haraka zaidi, na kuwaruhusu kuficha chimbuko la fedha haramu na hivyo kujiongezea faida.

Matumizi ya mihadarati miongoni mwa vijana barubaru ni tatizo kubwa kote duniani
© UNICEF/Giacomo Pirozzi
Matumizi ya mihadarati miongoni mwa vijana barubaru ni tatizo kubwa kote duniani

Jamii zahujumiwa na biashara ya mihadarati

Magenge ya uhalifu wa kupangwa  yanaendelea kuingiza mamilioni ya dola kutokana na ulanguzi wa dawa za kulevya, imeonya ripoti hiyo ya INCB, ikisistiza kuwa “hali hiyo ina matokeo mabaya kwa jamii na maendeleo ya kiuchumi, kuanzia ufisadi na hongo, hadi kuongezeka kwa uhalifu wa kupangwa, vurugu, umaskini na ukosefu wa usawa.”

Ili kukabiliana na athari mbaya na gharama za biashara hiyo kwa binadamu biashara hiyo, shirika linapendekeza kwamba serikali zishughulikie hatua zote za ulanguzi wa dawa za kulevya kuanzia uzalishaji na upanzi, hadi uuzaji, na ufichaji haramu wa faida na zishirikiane taarifa za kijasusi kuhusu uhalifu wa kupangwa katika ngazi ya kimataifa.

"INCB iliona mtiririko wa fedha haramu kuwa unastahili kuangaliwa mahususi na kuchunguzwa kwa sababu biashara ya madawa ya kulevya ni tasnia yenye faida kubwa kwa magenge ya uhalifu wa kupangwa", amesema Rais wa INCB, Jagjit Pavadia na kuongeza kuwa "Makundi haya yanategemea mtiririko wa fedha haramu kupanua na kuendeleza shughuli zao za uhalifu"

Cambodia, cannabis inachanganywa na heroin ambapo inavutwa na watumiaji.
© UNICEF/John Vink
Cambodia, cannabis inachanganywa na heroin ambapo inavutwa na watumiaji.

Nchi zinazoendelea zimeathirika zaidi

Ripoti inasema mitiririko hii inaelekeza rasilimali mbali na mipango ya kupunguza umaskini na kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ambayo ina athari kubwa kwa nchi zinazoendelea, ambapo kuna hitaji kubwa la fedha kukuza ukuaji wa uchumi na kupunguza pengo la usawa.

Katika nchi za Kiafrika, kwa mfano, ripoti inasema gharama ya uhalifu wa kupangwa ni kubwa sana inakadiriwa kuwa dola bilioni 88.6, takriban asilimia 3.7 ya pato la taifa la bara hilo na karibu kiasi sawa na mapato ya kila mwaka ya usaidizi rasmi wa maendeleo na uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni. zinapotea kwa sababu ya mtiririko haramu wa kifedha kila mwaka.

“Hii inasababisha kupotea kwa rasilimali za umma na kudhoofisha juhudi za kukusanya fedha kwa ajili ya maendeleo.”

Uhalalishaji wa bangi unakiuka kanuni za dawa

Kuharamishwa na kutozwa faini kwa bangi katika nchi nyingi kumetajwa na ripoti ya INCB kama sababu ya kutia wasiwasi, huku Bi Pavadia akisisitiza kwamba "kuhalalishwa kwa matumizi yasiyo ya matibabu ya bangi kunakiuka mikataba ya udhibiti wa dawa za kulevya".

Katika ripoti hiyo, bodi ya kudhibiti mihadarati inaangazia hitaji la uelewa wa pamoja wa dhana za kuhalalisha, kuharamisha, na kukataza sheria kulingana na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya, na inasisitiza umuhimu wa hatua zenye usawa kwa makosa yanayohusiana na mihadarati kama mwongozo mfano kanuni katika masuala ya haki ya jinai, kwa kuheshimu haki za binadamu na ustawi wa umma.

Msichana mwenye umri wa miaka 18 akiwa amelala pendeni ya mwanaye mchanga kwenye kituo cha malazi ya muda kwa ajili ya wanawake walioathirika na mihadarati mjini Bishkek Kyrgyzstan
© UNICEF/Shehzad Noorani
Msichana mwenye umri wa miaka 18 akiwa amelala pendeni ya mwanaye mchanga kwenye kituo cha malazi ya muda kwa ajili ya wanawake walioathirika na mihadarati mjini Bishkek Kyrgyzstan

Mapungufu makubwa

Kwa mujibu wa ripoti wahalifu wanaendelea kupata fursa rahisi ya kufikia masoko halali ya mihadarati, kwa watangulizi, na kupata kemikali zinazohitajika ili kutengeneza dawa haramu.

INCB inahimiza kuboreshwa kwa udhibiti na kanuni zinazosimamia uuzaji wa vianzilishi, ikitolea mfano utafiti uliofanywa na shirika hilo mwaka 2021, ambao ulionyesha mapungufu makubwa katika udhibiti wa utengenezaji, biashara na usambazaji wa kemikali hizo 

INCB

• INCB ni chombo huru, cha kimahakama kinachopewa jukumu la kukuza na kufuatilia utiifu wa serikali katika mikataba mitatu ya kimataifa ya udhibiti wa dawa za kulevya: Mkataba wa kwanza wa mwaka 1961 wa dawa za kulevya, mkataba wa 1971 wa dawa za matatizo ya kisaikolojia, na mkataba wa 1988 dhidi ya usafirishaji haramu wa dawa za kulevya na madawa ya saikolojia.

• Ikianzishwa na mkataba wa kwanza wa Madawa ya Kulevya wa 1961, INCB wanachama wake kumi na watatu wa bodi wanachaguliwa kwa nafasi ya kibinafsi na Baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC kwa vipindi vya miaka mitano.