Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo wa ‘Kafala’ watesa wafanyakazi wa ndani wahamiaji Lebanon

Mwanamke mmoja akitazama picha za wafanyakazi wahamiaji nchini Qatar
ILO/Aparna Jayakumar
Mwanamke mmoja akitazama picha za wafanyakazi wahamiaji nchini Qatar

Mfumo wa ‘Kafala’ watesa wafanyakazi wa ndani wahamiaji Lebanon

Haki za binadamu

Nchini Lebanon wafanyakazi wahamiaji wanaokwenda nchini humo kwa lengo la kujipatia kipato ili kunufaisha familia zao kule watokako, wanajikuta katika mazingira duni na hatarishi ikiwemo ubaguzi, ikiwa ni miongo miwili tangu kupitishwa kwa azimio la kimataifa la kupinga aina zote za ubaguzi ikiwemo wa rangi na kijinsia.

Mfumo wa ‘Kafala’ au udhamini na umiliki wa wafanyakazi hao unaofanywa na wale wanaowadhamini umekuwa ni chanzo cha tatizo linalosababisha wafanyakazi hao wa ndani wanawake kutoka nchi za kigeni kutegemea zaidi huruma za wale wanaowamiliki au waliowafadhili.

Wanatuona kama bidhaa: Mfanyakazi kutoka Ethiopia

Adanesh Worko, mfanyakazi kutoka Ethiopia ambaye anafanya kazi za ndani kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut anasema, “mawakala wa ajira na waajiri wanatuona kama bidhaa. Wakati mwingine tunapigwa na tunazuia kula chakula, hatuwezi kuhama kutoka familia moja inayokuajiri hadi nyingine kwa sababu ya mkataba.”

Worko anasema “Mama mwenye nyumba anakuambia, nimekununua nilipe dola 2000 na kisha utaenda kokote utakako.”

Wamepokonywa haki zao

Haki zao za msingi siyo tu zimeporwa bali pia haziheshimiwi, wakifanya kazi kwa muda usiotambulika, muda mrefu huku nyaraka zao kama hati za kusafiria na vibali vya ukaazi vikihifadhiwa na mmiliki, na uhuru wa kutembea, kuwasiliana na familia au kufurahia maisha vikiwa vimedhibitiwa.
Takwimu za hivi karibuni kutoka mashirika ya haki za binadamu zinaonesha kuwa takribani wafanyakazi wa ndani 250,000 wanaishi Lebanon na wengi wao ni wanawake ambao wana vibali vya kazi na wanatoka Ethiopia, Ufilipino, Bangladesh na Sri Lanka.

Mfumo wa Kafala ni kandamizi kwa wafanyakazi

Mfumo huu unampatia mdhamini udhibiti wa mfanyakazi na maisha yake na hivyo kumtumbukiza katika hatari ya mateso na ukatili kwa ujira wa katiya dola 150 hadi 400 kwa mwezi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya haki za binadamu, chini ya mfumo huu wa Kafala, mfanyakazi hawezi kusitisha mkataba bila ridhaa ya  mwajiri wake ambaye ndiye amemdhamini kwa kati ya dola 2000 hadi 5000 kupitia mawaka wa uajiri.
Sheria haizuii mwajiri kuzuia au kushikilia hati ya kusafiria ya mfanyakazi. Iwapo atatoroka uwepo wake nchini Lebanon unakuwa ni kinyume cha sheria.

Hati yangu ya kusafiria anayo mwajiri, mume kanitelekeza na watoto

Maria, mwenye umri wa miaka 30 ni mfanyakazi mhamiaji kutoka Ufilipino. Machozi yanambubujika wakati anaelekea nyumbani akiwa na watoto wake watatu, mkubwa akiwa na umri wa zaidi ya miaka 6.
Alipoulizwa hadhi yake ya kazi, anasema anafanya kazi kwa mwanamke mmoja eneo la Mar Elias karibu na Beirut kwa ujir wa kiwango cha chini ya mshahara cha Lebanon ambacho ni kidogo mno kumwezesha kukimu mahitaji ya familia yake. 

Maria anasema aliolewa na mlebanon lakini mumewe huyo alimtelekeza na akakataa kusajili watoto wao watatu na yeye mwenyewe Maria alishindwa kuwasajili kwa sababu hati yake ya kusaifiria anashikilia mwajiri wake.

Wafanyakazi wa ndani wahamiaji  nchini Lebanon wamepoteza ajira zao
IOM/Muse Mohammed
Wafanyakazi wa ndani wahamiaji nchini Lebanon wamepoteza ajira zao

Tunafanya kazi kutokomeza mfumo wa Kafala- UNWomen

Mkurugenzi shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake UNWomen nchini Lebanon, Rachel Dore-Weeks, amethibitisha kuwa wanafanya kazi kuhakikisha mfumo huo wa udhamini wa wafanyakazi au Kafala unatokomezwa.

“Wafanyakazi wanakosa ulinzi na wanakuwa  hatarini kukumbwa na aina mbalimbali za ukatili wa kimwili, kingono na kiuchumi,” amesema Bi. Dore-Weeks.

Wafanyakazi si tu wanalipwa ujira mdogo, hata likizo wananyimwa

Bi. Dore-Weeks amesema wafanyakazi wahamiaji wanalipwa ujira mdogo, na wakati mwingine hawalipwi kabisa hasa wakati huu ambapo uchumi umeporomoka na likizo ndio kabisa hakuna.

Ni kwa mantiki hiyo mwakilishi huyo wa UNWOmen amesisitiza juhudi za kushirikiana na mashirika mengine ili wafanyakazi wahamiaji Lebanon wapate haki zao. Mratibu wa kitengo cha taasisi ya Kafa cha kuzuia usafirishaji haramu na ukatili Julie Khoury, amesema mipango ambayo wanatekeleza ambayo inapata msaada kutoka UNWomen ni pamoja na huduma kwa wafanyakazi wahamiaji wanawake ambao wanakumbwa na ukatili wa kingono na vipigo kutoka kwa waajiri au wadhamini wao. Wanawapatia malazi, msaada wa kisheria, kijamii, afya na kisaikolojia.

Amezungumzia pia vitendo vya kujiua vinavyofanywa na wafanyakazi hao wa ndani akisema vinachochewa na kunyimwa haki zao za msingi.