Lebanon chukueni hatua mnusuru wananchi- OHCHR

21 Januari 2020

Ghasia kati ya waandamanaji na vikosi vya  usalama nchini Lebanon vimezua hofu kubwa katika ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa  Mataifa, OHCHR.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa ofisi hiyo Marta Hurtado amesema, “tuna hofu kubwa na ongezeko la matukio ya mapigano hivi karibuni kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama Lebanon,” akiongeza kuwa, “baadhi ya waandamanaji wameamua kutumia ghasia hizo kuelezea machungu  yao na vikosi vya  usalama vimejibu ambapo wakati mwingine vimetumia nguvu kupita kiasi.”

Bi. Hurtado ametoa mfano kuwa mwishoni mwa wiki kwenye mji mkuu Beirut, waandamanaji walijaribu kuvamia jengo la Bunge na kuvurumushia mawe, alama za barabarani na aina mbalimbali za taka askari wa usalama wa ndani.

Katika tukio hilo, baadhi ya mashine za kutolea fedha au ATMs, ofisi za benki na maduka  yaliporwa na hata maeneo ya umma yaliharibiwa.

Kwa mujibu wa Bi. Hurtado, vikosi vya usalama vilidhibiti waandamanaji kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi, mabomu ya maji na risasi za mpira na kwamba, “kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya  habari, vijana wanne walifyatuliwa risasi za mpira kwa karibu na kusabababisha macho yao kuharibika kupindukia.”

Amenukuu takwimu za chama cha msalaba mwekundu cha Lebanon na ulinzi wa raia zinazoonesha kuwa takribani watu 377 kati yao 142 polisi walijeruhiwa jumamosi ya tarehe 18 mwezi huu wa Januari na watu wengine 90 walijeruhiwa siku iliyofuatia.”

Msemaji huyo wa OHCHR amekumbusha kuwa, “maafisa wa usalama wanapaswa kuzingatia kanuni na viwang vya kimataifa vya matumizi ya nguvu hususan kanuni ya uhalali wa kutumia nguvu kwa uwiano wa tukio na mazingira husika.”

Hata hivyo amekaribisha tamko la kamanda wa kikosi hicho cha usalama wa ndani, ISF la kutambua umuhimu wa kujizuia wakati wa kukabiliana na waandamanaji wanaofanya ghasia na pia kulinda waandishi wa habari na wale wanaoandamana kwa amani.

Amekumbusha kuwa watu wana haki ya kushiriki kwenye masuala ya umma na kupanga mambo yanayogusa maisha yao ikiwemo kuandamana kwa amani na kuelezea shaka na shuku zao.

Halikadhalika amekumbusha waandamanaji kuwa wanapaswa kutekeleza wajibu huo bila kufanya ghasia.

Ofisi hiyo ya haki za binadamu imetaka mamlaka za Lebanon kufanya uchunguzi huru na wa kina usioegemea upande wowote kuhusu mlipuko wa hivi karibuni wa ghasia na vitendo vya wanaotiwa korokoroni kutendewa mambo mabaya.

Amegeukia pia wanasiasa kutekeleza matamanio ya wananchi na kusongesha juhudi za kuunda serikali jumuishi na tulivu ili hatimaye ishughulikie matakwa ya wananchi ambao wanakumbwa na shida kutokana na janga la kiuchumi.

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter