Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa ndani 76 wauawa DRC katika kipindi cha wiki mbili, UNHCR yapaza sauti

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa MONUSCO wakifanya doria katia eneo la Ituri ili kuzuia vitendo vya ADF.
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa MONUSCO wakifanya doria katia eneo la Ituri ili kuzuia vitendo vya ADF.

Wakimbizi wa ndani 76 wauawa DRC katika kipindi cha wiki mbili, UNHCR yapaza sauti

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNCHR lina wasiwasi mkubwa kutokana na matukio ya mauaji jimboni Ituri na Kivu Kusini katika wiki mbili zilizopita ambako jumla ya wakimbzi wa ndani 76 wameuawa na makumi kadhaa wamejeruhiwa.

Msemaji wa UNHCR Boris Cheshirkov amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, USwisi hii leo kuwa chanzo kikuu cha mashambulizi hayo ni mivutano ya kikabila, wizi wa mifugo na ukosefu wa uhakika wa shughuli za kujipatia kipato.

Tukio la hivi karibuni ni huko kituo cha kuhifadhi wakimbizi wa ndani cha Ndjala kwenye ukanda wa kiafya wa Droro jimboni Ituri ambako siku ya Jumapili wanamgambo wenye bunduki, mapanga na visu waliua watu 26 wakiwemo wanawake 10 na watoot 9. Watu wengine 11 walijeruhiwa.

Tukio la pili la tarehe 21 mwezi huu wa Novemba katika eneo hilo hilo la Droro na Tché ambako watu 44 waliuawa na zaidi ya makazi yao 2,200  kuteketezwa kwa moto.

“Hivi sasa takribani watu 20,000 waliokuwa wamesaka hifadhi kwenye vituo hivyo wamekimbilia Rhoe kusaka usalama karibu na kituo cha kijeshi cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani , DRC, MONUSCO na kutokana na kuzidiwa uwezo familia zilizowasili hivi sasa zinaishi nje,” amesema Cheshirkov.

Watoto wakimbizi wa ndani wakicheza katika kituo rafiki kwa watoto kambini Droro, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
© UNICEF/UN0377403/Roger LeMoyne
Watoto wakimbizi wa ndani wakicheza katika kituo rafiki kwa watoto kambini Droro, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Awali kituo hicho chenye uwezo wa kuhifadhi watu 21,000 kinahifadhi wakimbizi 48,000 na wapya waliombilia sasa wamefanya idadi kuwa 70,000 na mahitaji makubwa ni chakula, malazi, huduma za afya na msaada wa kisaikolojia.
Tukio la tatu ni huko mji wa Mikenge jimboni Kivu Kusini ambako tarehe 14 mwezi Novemba watu wenye silaha walishambulia na kuua watu 7 wakiwemo watoto 6 na mjamzito mmoja.

Kwa sasa UNHCR inataka pande zote ziheshimu maeneo ya raia na huduma za kibinadamu sambamba na kuhakikisha huduma za kibindamu zinafikia wahitaji.

Pamoja na hilo, UNHCR inakumbushia ombi lake la kusaidia DRC ambalo hadi sasa imepatikana asilimia 52 tu ya dola milioni 204.8 zinazohitajika kuokoa wananchi wa DRC.