Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utumaji fedha kimtandao ulinusuru familia za kijijini mwaka 2020 

Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa  jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote
Picha-IFAD
Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote

Utumaji fedha kimtandao ulinusuru familia za kijijini mwaka 2020 

Ukuaji wa Kiuchumi

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD umesema ingawa kiwango cha wahamiaji kutuma fedha nyumbani kimtandao  wakati wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 mwaka 2020 kimeongezeka, bado kaya za vijijini zilishindwa kunufaika vyema na utumaji huo kutokana na kukosa miundombinu ya kidijitali ya kupokea fedha hizo. IFAD imesema hayo ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya familia kutumiana fedha.

Mathalani nchini Nepal katika maeneo ya vijijini Pushpa Raut na familia yake wanategemea fedha za kujikimu kutoka kwa  mumewe afanyaye kazi ughaibuni. 

Pushpa anasema, "mume wangu amekuwa anafanya kazi nje ya nchi kwa miaka 10 sasa. Hivi sasa yuko Dubai akifanya kazi zinazohusiana na ushonaji.” 

Mumewe ni miongoni mwa wafanyakazi wahamiaji milioni 200 ambao hutuma fedha nyumbani, fedha zitumiwazo kwa mahitaji ya chakula, karo za shule na afya. 

Ilikadiriwa kuwa utumaji fedha ungalipungua kwa sababu ya  janga la COVID-19, kutokana na vikwazo vya kutembea na kufungwa kwa benki,  lakini kiwango hicho kilipungua kwa asilimia 1.6 pekee hadi kufikia dola bilioni 540, hali inayoonesha umuhimu wa utumaji fedha.

Maria Bibiana Carreara, wa kampuni ya Bancolumbia itumayo fedha kwa njia ya mtandao anasema, “COVID-19 imeonesha kuwa ijapokuwa wacolumbia walipata shida za kiuchumi, waliendelea kutuma fedha kusaidia familia zao.” 

IFAD inasema utumaji fedha kimtandao uligeuka kimbilio na kiwango cha fedha zilizotumwa kwa simu za kiganjani pekee kiliongezeka kwa asilimia 65 na kufikia dola bilioni 12.7 mwaka 2020 pekee. 

Hata hivyo ukosefu wa intaneti ya uhakika vijijini unafanya familia za vijijini siyo tu zishindwe kupokea fedha kiganjani bali pia ziingie gharama kubwa kupata huduma hiyo. 

Ni kwa mantiki hiyo Meike Van Ginneken afisa kutoka IFAD anasema “katika dunia ya uchumi wa kisasa, utumaji fedha kimtandao ndio taswira ya utandawazi na jamii ya kimataifa inapaswa kushirikiana kuifanya huduma hiyo siyo tu iwe rahisi bali pia ifikie mamilioni ya familia na jamii ambako wanaishi.” 

Takwimu zinaonesha kuwa mtu 1 kati ya 7 duniani anategemea fedha zinazotumwa kutoka kwa jamaa hivyo IFAD inasema kurahisisha huduma hiyo ya kiteknolojia kunamaanisha kuwatoa mamilioni ya watu kutoka katika lindi la umaskini.