Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wataka wafanyakazi wake kuachiwa mara moja nchini Ethiopia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari nchini Italia
UNTV screen grab
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari nchini Italia

Umoja wa Mataifa wataka wafanyakazi wake kuachiwa mara moja nchini Ethiopia

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amerudia wito wake wa kutaka kuachiliwa huru mara moja kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliowekwa kizuizini nchini Ethiopia. 

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema Katibu Mkuu Guterres anavyofahamu mpaka sasa ni kuwa watumishi hao wanashikiliwa bila kufunguliwa mashtaka, na hakuna taarifa maalum iliyotolewa kuhusiana na sababu za kukamatwa kwao. 

“Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanafanya kazi muhimu na bila upendeleo nchini Ethiopia. Katibu Mkuu anasisitiza wajibu wa kuheshimu haki na kinga za wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wa wafanyakazi wa kimataifa na wa Ethiopia, pamoja na kuwalinda wafanyakazi wa wote wanaoshughulika na masuala ya kibinadamu nchini Ethiopia, ikiwa ni pamoja na kutowekwa kizuizini kiholela.” Amesema Dujarric

Ameongeza kuwa, Katibu Mkuu ameelezea wasiwasi wake juu ya ripoti za kukamatwa kwa watu kiholela na kuwekwa kizuizini, kitendo kinachoongeza mgawanyiko na chuki kati ya makundi. 

“Ametoa wito kwa mamlaka kutoka hadharani na kuzungumza bila shaka na kukemea kulengwa kwa kabila au makundi fulani na kuonesha kujitolea kwao kusimamia haki za binadamu na utawala wa sheria. “amesema msemaji huyo wa Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu amesema mwenendo wa mzozo wa kijeshi hautaleta amani na utulivu ya kudumu nchini Ethiopia na amezitaka pande husika kukomesha uhasama na kuweka kipaumbele kwenye kuboresha ustawi wa raia kwakuwa changamoto zinazoikabili Ethiopia zinaweza tu kutatuliwa kwa mazungumzo yanayowashirikisha Waethiopia wote.