WHO kupunguza gharama za vipimo vya VVU na kaswende kunusuru maisha ya watoto

15 Novemba 2021

Ili kusaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI- VVU na Kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hii leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa ulimwenguni limetangaza kupunguza gharama ya vipimo vya haraka vya magonjwa hayo baada ya kuingia mkataba wa ushirikiano na makampuni ya Clinton Health Access Initiative (CHAI), MedAccess na SD Biosensor. 

Kwa mujibu wa WHO vipimo hivyo sasa vitapatikana kwa gharama ya chini ya dola moja. Hii inafanya kuwa vipimo cha bei nafuu zaidi sokoni vilivyopitishwa na WHO kwa ajili ya VVU na kaswende. 

"Tangazo la bei mpya ni muhimu. Kushuka huku kwa bei kutasaidia nchi nyingi zaidi kumudu kufanya upimaji wa VVU na kaswende na kuharakisha mchakato katika kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kutoa huduma kwa watu muhimu, ambapo maambukizi yote mawili ni ya kawaida." Amesema Meg Doherty, mkurugenzi wa mipango ya kimataifa ya WHO kuhusu VVU, homa ya ini na maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STIs). 

Zaidi ya wajawazito milioni 2 huambukizwa VVU na kaswende kila mwaka 

Kila mwaka, takribani wanawake milioni 1.3 wanaoishi na VVU hupata mimba na chini ya wajawazito milioni 1 huambukizwa kaswende.  

Licha ya kuwepo kwa uchunguzi na matibabu ya bei nafuu, VVU ambayo haijatambuliwa na ambayo haijatibiwa na maambukizi ya kaswende kati ya wajawazito yanaendelea kuathiri vibaya maisha ya kina mama wengi na watoto wao. 

Kulingana na WHO vipimo vipya ambavyo ni rahisi kutumia ambavyo vimependekezwa na shirika hilo vitasaidia kurahisisha huduma  na kuziwezesha nchi nyingi zaidi  kukomesha maambukizi ya magonjwa hayo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (MTCT) .

Kwa kiasi kikubwa shirika hilo linasema nchi nyingi zaidi zinafuata mapendekezo ya WHO na kuanza kutoa huduma hiyo ya vipimo vya haraka vya pamoja vya VVU na kaswende katika kliniki za huduma ya mama na mtoto hususan katika ukanda wa Afrika. 

Kwa mwaka 2020 WHO inakadiria kwamba wahisani wakubwa na serikali walinunua zaidi ya vipimo milioni 5 kwa ajili ya VVU na kaswende na miongoni mwa nchi zilizokwisha anza utekelezaji ni Nigeria. 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter