Kwa mwenendo wa sasa, takriban barubaru 76 watakufa kutokana na UKIMWI kila siku ifikapo 2030 -UNICEF

Kijana anayeishi Peru aliyepatikana kuwa anaishi na VVU mapema mwaka 2018
© UNICEF/Daniele Volpe
Kijana anayeishi Peru aliyepatikana kuwa anaishi na VVU mapema mwaka 2018

Kwa mwenendo wa sasa, takriban barubaru 76 watakufa kutokana na UKIMWI kila siku ifikapo 2030 -UNICEF

Afya

Vijana barubaru 76 wanakadiriwa kuwa watafariki dunia kila siku ulimwenguni kote kati ya mwaka hu una 2030 iwapo uwekezaji sahihi hautafanyika kuzuia Virusi Vya Ukimwi, VVU miongoni mwa kundi hilo, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF iliyotolewa leo kuelekea siku ya Ukimwi duniani tarehe mosi mwezi ujao. 

Sauti ya Delar Chanceline, barubaru kutoka Chad akisema kuwa alizaliwa na VVU na hakufahamu hali  yake hadi mama yake alipomweleza akiwa na umri wa miaka 14.

Hofu yake Chanceline ni kwamba marafiki akiwaeleza kuhusu hali ya kuishi na VVU, basi atanyanyapaliwa, jambo ambalo anasema linaumiza.

Chanceline ni miongoni mwa barubaru ambao ripoti hiyo ya UNICEF yenye jina, watoto, VVU na ukimwi:Dunia mwaka 2030, inataka uwekezaji zaidi ili wasinyanyapaliwe na wapate huduma zinazostahili.

“Ripoti inaonesha dhahiri kuwa dunia haiku katika njia sahihi katika vita vya kutokomeza ukimwi miongoni mwa watoto na barubaru ifikapo 2030,” amesema Henrietta Fore, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF.

Hata hivyo Bi Fore amesema kuna matokeo chanya katika programu za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama hadi mtoto lakini haijakwenda mbali zaidi, wakati programu za kutibu VVU na kuzuia kuenea miongoni mwa watoto ni chini ya matarajio.

Matumaini kutoka kwenye ripoti ni kwamba idadi ya watoto na barubaru watakaokufa kutokana na sababu zitokanazo na ukimwi itapungua kutoka 119,000 hadi 56,000 mwaka 2030.

Mtoto mchanga akitolewa sampuli za damu ili apimwe VVU katika moja ya vitu vya kuchunguza Virusi Vya Ukimwi, VVU huko Kyrgyzstan
UNICEF/Aleksei Osipov
Mtoto mchanga akitolewa sampuli za damu ili apimwe VVU katika moja ya vitu vya kuchunguza Virusi Vya Ukimwi, VVU huko Kyrgyzstan

Ripoti imetaja sababu mbili kuu za kasoro kwenye vita dhidi ya VVU miongoni mwa watoto na barubaru, mosi ni upungufu wa kasi ya kuzuia VVU miongoni mwa watoto na kosa la kutoaangazia vichochezi vinavyosababisha hali hiyo kwani kundi hilo la watu hawajui hali yao ya VVU na pili wale wamepatikana kuwa na virusi hivyo na kuanza tiba hawazingatii tiba.

Kwa sasa watoto milioni tatu na barubaru wanaishi na VVU kote ulimwenguni na zaidi ya nusu wako Afrika Mashariki na Kusini.

Ripoti imependekeza mambo muhimu katika kuziba pengo ikiwa ni kuwezesha vipimo vinavyolenga familia kwa ajili ya kugundua na kutibu watoto wanoishi na VVU ambao hawajapimwa; kuimarisha teknoloji ya utafiti katika vituo vya huduma ili kuimarisha vipimo kwa watoto wachanga; matumizi zaidi ya jukwaa za kidijitali kuimraisha taarifa kuhusu VVU miongoni mwa barubaru; kuwepo huduma rafiki kwa vijana na program zinazowafikia barubaru.

UNICEF imesema ili kushinda vita dhidi ya VVU ni lazima kuongeza kasi ya kupunguza maambukizi kwa vizazi vijavyo.