Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa chakula DRC watia wasiwasi: UN

Miti milioni moja imepandwa ikiwa ni moja ya juhudi za kulinda mazingira nchini DRC
CIFOR/Axel Fassio
Miti milioni moja imepandwa ikiwa ni moja ya juhudi za kulinda mazingira nchini DRC

Ukosefu wa chakula DRC watia wasiwasi: UN

Msaada wa Kibinadamu

Ripoti ya utafiti mpya uliofanywa na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la Chakula na Kilimo -FAO na la mpango wa chakula duniani WFP imeeleza matokeo mapya yanaonesha janga la ukosefu wa chakula nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo -DRC lina dalili ndogo ya kupungua, na linaweza kuwa baya zaidi katika miezi ijayo iwapo msaada hautaongezwa.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo huko Roma, Italia inasema takriban watu milioni 27 sawa na robo ya idadi ya watu wote wa DRC wanakabiliwa na dharura ya hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula, hali  ambayo imechangiwa na mavuno hafifu, vurugu zilizosababisha watu kuyakimbia makazi yao, magonjwa na kuharibika kwa miundombinu.

Mwakilishi wa FAO nchini DRC Aristide Ongone amesema “Njia pekee ya kuvunja mzunguko na kubadili mwelekeo huu ni kuwasaidia kuongeza uthabiti wao na uzalishaji." 

Akiunga mkono kauli hiyo mwakilishi wa WFP nchini humo Peter Musoko amesema takwimu hizo zilizotolewa leo ni wito wa kufanya mambo tofauti na kwa umoja 

Musoko ameongeza kuwa "hali ilivyo kwa sasa, ni kama tunaokoa mashua inayovuja. Tunahitaji kuja pamoja mashirika ya kimataifa, serikali, na sekta binafsi, tujadiliane na kuwapa matumaini watu wa nchi hii.”

Mradi wa kuejesha na kuboresha ardhi Kaskazini mwa DRC umeleta tija
CIFOR/Axel Fassio
Mradi wa kuejesha na kuboresha ardhi Kaskazini mwa DRC umeleta tija

Mradi wa pamoja 

Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNICEF, FAO na WFP yamezindua mradi wa kupambana na njaa mijini, na katika viunga vya Kinshasa. Mradi huo unalenga kutoa pesa taslimu kwa watu 100,000 walio hatarini zaidi katika wilaya ya N'sele, iliyoathiriwa sana na kuzorota kwa uchumi kutokana na janga la COVID-19.

Pamoja na mradi huo, FAO imejikita kwenye kusaidia kutoa mbegu na pembejeo za kilimo kwa watu milioni 1.1 katika nchi nzima ya DRC na imetoa ombi la dola milioni 65, lakini hadi sasa imepata msaada wa dola milioni 4.5 kutoka kwa wafadhili.

Nalo shirika la WFP limesema linauhitaji wa dola milioni 99 na inapanga kuwafikia watu milioni 8.7 nchini DRC kuwapatia msaada wa chakula, lishe na fedha taslimu.