Corona yatishia harakati za kutokomeza Surua- WHO

Mama akiwa amembeba mwanae mwenye umri wa miezi mitatu wakati anapatiwa chanjo dhidi ya Surua kwenye kituo cha afya jijini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
© UNICEF/Karel Prinsloo
Mama akiwa amembeba mwanae mwenye umri wa miezi mitatu wakati anapatiwa chanjo dhidi ya Surua kwenye kituo cha afya jijini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Corona yatishia harakati za kutokomeza Surua- WHO

Afya

Licha ya kwamba idadi ya wagonjwa wa surua imepungua ikilinganishwa na miaka  iliyotangulia, kasi ya kutokomeza ugonjwa huo inapungua huku milipuko mipya ikiripotiwa, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO na kituo cha Marekani cha kudhibiti na kuzuia magonjwa, CDC.
 

Ripoti hiyo imesema janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limevuruga huduma za kawaida za utoaji wa chanjo, na kubadili tabia ya kusaka huduma za afya kote duniani.

“Wakati mikakati ya kujikinga na COVID-19 kama vile kuvaa barakoa, kunawa mikono, na kuepuka kuchangamana nazo pia zinasaidia kupunguza kusambaa kwa virusi vinavyosababisha surua, serikali na wadau wa afya duniani wanapaswa kupatia kipaumbele mbinu za kusaka na kuwapatia chanjo watoto dhidi ya surua na hivyo kupunguza uwezekano wa milipuko na vifo vinavyoepukika kutokana na ugonjwa huo,” imesema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo iliyotolewa mjini Atlanta Marekani na Geneva Uswisi imesema mwaka jana pekee wa 2020, zaidi ya watoto milioni 22 walikosa dozi ya kwanza ya chanjo dhidi ya surua, ikiwa ni watoto milioni 3 zaidi ikilinganishwa na mwaka 2019, ongezeko kubwa katika miongo miwili na linaweka upenyo wa mlipuko wa surua.

Kevin Cain Mkurugenzi wa chanjo CDC amesema “idadi kubwa ya watoto ambao hawajachanjwa chanjo ya surua, milipuko ya surua na vifaa vya kubaini na kuchunguza ugonjwa huo vimeelekezwa kusaidia janga la Corona au COVID-19 ni sababu ya ongezeko la uwezekano wa vifo vitokanavyo na surua na madhara makubwa kwa watoto.”

Mwaka 2020, COVID-19 ilisababisha kuahirishwa kwa kampeni za chanjo ya surua katika nchi 23 na hivyo zaidi ya watu milioni 93 kuwa hatarini kuambukizwa surua.

Amesema ni lazima kuchukua hatua sasa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na kuziba pengo la ukosefu wa kinga.

Surua ni moja ya magonjwa hatari na ambukizi duniani lakini unakingwa kwa kutumia chanjo. Katika miaka 20 iliyopita, chanjo dhidi ya surua imeepusha vifo zaidi ya milioni 30 duniani kote.