Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo dhidi ya surua na polio yaendelea ili kuokoa mustakabali wa watoto Somalia 

Mtoto mwenye umri wa miaka 9 akipata chanjo. Katika maeneo mengine duniani, upatikanaji wa huduma za afya kama hizi zimekuwa ni changamoto.
© UNICEF/Moreno Gonza
Mtoto mwenye umri wa miaka 9 akipata chanjo. Katika maeneo mengine duniani, upatikanaji wa huduma za afya kama hizi zimekuwa ni changamoto.

Chanjo dhidi ya surua na polio yaendelea ili kuokoa mustakabali wa watoto Somalia 

Afya

Malaki ya watoto nchini Somalia wamechanjwa dhidi ya ugonjwa wa surua na polio wakati wa kampeni ya chanjo kudhibiti mlipuko wa magonjwa hayo hatari, imeeleza taarifa ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM.

Akina mama wamekaa kati viti vilivyowekwa chini ya mti nje ya kituo cha afya cha Hamar-Jajab mjini Moghadishu nchini Somalia wakisubiri watoto wao kuchanjwa dhidi ya surua na polio.   

Aina ya polio ambayo iko kwenye mzunguko kwa sasa ni tofauti na ile polio iliyotangazwa kuwa imetokomezwa barani Afrika lakini hii nayo inaweza kuziweka hatarini jamii ambazo si watoto wengi wamechanjwa na hivyo kuwaacha wakiwa wamepooza katika maisha yao yote.  Aina hii polio tayari imewafanya watoto 19 kupooza tangu mwaka 2017. 

Sehemu ya kwanza ya kampeni ya chanjo ilifanyika mwezi uliopita katika mkoa wa Benadir ambao unajumuisha na kuuzunguka mji mkuu wa Somalia, Moghadishu, ambako ni makazi ya idadi kubwa ya watu waliotawanywa nchini Somalia na pia kituo cha wasomali wanaosafiri kimataifa. 

Nchini Somalia mtoto mmoja kati ya saba hufariki dunia kabla ya kutimiza miaka mitano na mara nyingi vifo hivi vinazuilika kwa kutumia chanjo. Ni kwasababu hiyo Nadijo Sirad Alina watoto wake watatu  amekuwa akisubiri hapa kwenye kituo cha afya cha Hamar-Jajab katika msururu mrefu na tena katika jua kali la asubuhi. Mama huyu mwenye umri wa miaka 30 mara tu baada ya kutoka ndani ya kituo anasema, “watoto wangu wote hivi sasa wana afya kwa hivyo sina hofu hata kama kuna mlipuko wa ugonjwa kwa kuwa ninafahamu wamechanjwa.”  

Watoto wa Nadijo walikuwa miongoni mwa watoto wengi katika eneo la Benadir ambao walilengwa na utoaji wa chanjo dhidi ya surua na polio kama anavyoeleza Mohamud Shire Mohamed ambaye ni Afisa wa utokomezaji Polio anayefanya kazi na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO,“kampeni hii imefanyika katika wilaya zote 17 za Mogadishu kwa lengo la kuwafikia watoto 492,000, lengo ambalo lilifikiwa. Pia tulitoa Vitamini A na vidonge vya minyoo ili kuongeza kinga na kuua vimelea.” 

Kwa mujibu wa maafisa wa afya wa eneo hilo, zoezi la chanjo limetokana na kuzuka kwa ugonjwa wa surua hivi karibuni mjini Mogadishu. Kuanzia mwanzo wa mwaka huu wa 2020, ugonjwa wa surua umeathiri watoto 744 katika mkoa wa Benadir, hiyo ikiwa ni karibu nusu ya maambukizi yote yaliyoripotiwa Somalia. Ugonjwa huu wa kuambukiza sana, kwa watoto wasio na chanjo unaweza kusababisha homa na upele kati ya dalili nyingine na matatizo mengine mabaya zaidi ya ugonjwa wa surua ni pamoja na upofu, ubongo kuvimba, kuhara, upungufu wa maji mwilini, na maambukizi mazito ya mfumo wa upumuaji kama vile nimonia. 

Sehemu ya pili ya kampeni hii ya chanjo inafanyika mwezi huu wa Oktoba ambayo inafanyika nyumba kwa nyumba ikilenga kuwafikia watoto milioni 1.6 katika mikoa ya kusini na katikati mwa Somalia.