Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufadhili mpya kuwezesha watoto milioni 370 kupata chanjo ya polio duniani

Mtoto mvulana akipewa chanjo wakati wa kampeni ya chanjo ya polio huko Kisangani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Julai 2022.
© UNICEF/Jean-Claude Wenga
Mtoto mvulana akipewa chanjo wakati wa kampeni ya chanjo ya polio huko Kisangani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Julai 2022.

Ufadhili mpya kuwezesha watoto milioni 370 kupata chanjo ya polio duniani

Afya

Katika kuhakikisha watoto duniani kote wanapatiwa chanjo ya polio pamoja na kuimarisha ubunifu katika sekta ya afya wadau wa masuala ya afya hii leo wametangaza kutoa msaada wa zaidi ya dola bilioni 1.17. 

Katika mkutano wa pamoja uliofanyika hii leo huko Brussels Ubelgiji wadau hao ambao ni Kamisheni ya Ulaya, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na Wakfu wa Bill & Melinda Gates wameeleza kutoa fedha hizo kwa mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa ambayo ni lile la Afya ulimwenguni WHO na la kushughulikia masuala ya watoto UNICEF. 

Akitangaza Msaada huo Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula Von der Leyen kwa furaha amesema “Tunaenda kuifutilia mbali polio kwenye uso wa dunia.” Akitolea mfano ambavyo kwa ushirikiano dunia iliweza kupambana na janga la COVID-19 basi ndivyo Msaada huu utakavyowezesha kukabiliana na Polio. 

Naye Mwenyekiti Mwenza wa Wakfu wa Bill & Melinda Gates Bi. Bill Gates amesema lengo hasa ni kuhakikisha hakuna mtoto sehemu yeyote duniani anayeteseka kutokana na ugonjwa huo mbaya. 

Bi. Gates amesema hii haitakuwa mara ya kwanza kwani “Shukrani kwa ubunifu wa kimatibabu, ulimwengu ulifanikiwa kutokomeza ugonjwa wa ndui. Leo tuko kwenye harakati za kumaliza ugonjwa huu mwingine wa virusi vya polio.”

Mpaka sasa virusi vya polio bado vimeenea katika nchi mbili pekee - Pakistan na Afghanistan.

Umoja wa Mataifa washukuru 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus alitoa shukran kwa wadau hao akieleza kuwa kuhakikidha watoto ambao wanapata chanjo kwa uchache au wale ambao hawajapata kabisa chanjo wanafikia ni suala muhimu sana na tena kwa kuzingatia watoto hao wengi wanaoishi katika maeneo ya pembezoni au yaliyo tabu kufikiwa . 

“Ufadhili huu hautatusaidia kuhakikisha kunaondoa kabisa ugonjwa wa Polio duniani pekee bali pia utasaidia kujenga mifumo stahimilivu ya afya kwa watoto na jamii zilizo hatarini kupata polio na changamoto nyingine nyingi za afya.” Dkt.Tedros 

“Hakuna mtoto anayepaswa kuugua ugonjwa unaoweza kuzuilika kwa urahisi.” Amesema Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Catherine Rusell nakuongeza kuwa “Kutokomeza Polio ni suala linaloweza kufikiwa, lakini maendeleo bado ni tete na lazima tubaki kuwa makini.”

Mkuu huyo wa UNICEF ana imani kuwa ufadhili huu mpya utasaidia kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo ya kutokomeza polio, huku wakiimarisha mifumo ya afya katika jamii. 

Matumizi ya fedha

Nusu ya fedha hizo zitagharamia chanjo ya polio ambayo inatarajiwa kuweza kuwafikia takriban watoto milioni 370 kila mwaka, kutoa huduma muhimu za afya kwa watoto pamoja na kampeni za polio. Pia kutakuwa na chanjo za surua na chanjo nyinginezo za kawaida. Pia fedha hizo za chanjo ya polio zitasaidia kuimarisha mifumo ya afya ili kujiandaa vyema na kukabiliana na vitisho vya afya vinavyojitokeza, kama COVID-19, Ebola na magonjwa mengine. 

Na nusu ya pili ya fedha hizo zitaenda kwenye kusaidia masuala ya uvumbuzi wa mifumo ya afya katika nchi za kipato cha chini na cha kati. Hii ni pamoja na ufadhili mpya kwa mipango inayoungwa mkono na Kamisheni ya Ulaya kama vile chanjo na matibabu yanayotegemea mRNA kupatikana zaidi kwa watu katika nchi za kipato cha chini na cha kati.