Surua bado ni mwiba, idadi ya wagonjwa yafurutu ada, yaua watu 200,000 utoaji chanjo wakwama- WHO

12 Novemba 2020

Ugonjwa wa surua ulisababisha vifo vya watu wapatao 207,000 mwaka jana pekee baada ya muongo mzima wa mkwamo wa kupanua wigo wa utoaji wa chanjo, limesema shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO na kitu cha Marekani cha udhibiti wa magonjwa, CDC.
 

Katika ripoti yao ya pamoja iliyotolewa leo, WHO na CDC wamesema “idadi ya vifo mwaka 2019 ilikuwa asilimia 50 zaidi ya kiwango cha chini zaidi cha mwaka 2016 na katika kanda zote za WHO, idadi ya wagonjwa iliongezeka na kuwa wagonjwa 869,770 duniani kote.”

Mwaka huu kumekuwepo na idadi ndogo ya wagonjwa, lakini janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 linarudisha nyuma mafanikio katika utoaji chanjo, ambapo watu zaidi ya milioni 94 wako hatarini kukosa chanjo ya surua katika nchi 26 kutokana na kusitishwa kwa kampeni za chanjo, ikiwemo katika nchi ambazo bado kuna milipuko.

Mtoto mwenye umri wa miezi 7 akitibiwa dhidi ya surua kwenye hospitali moja huko Samoa kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo visiwani humo.
©UNICEF/Allan Stephen
Mtoto mwenye umri wa miezi 7 akitibiwa dhidi ya surua kwenye hospitali moja huko Samoa kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo visiwani humo.

Surua bado ipo

“Kabla ya janga la COVID-19, dunia ilikuwa inahaha na janga la surua na bado lipo,” amesema Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwenye taarifa hiyo. “Wakati mifumo ya afya inazidiwa uwezo kutokana na janga la COVID-19, katu tusiruhusu vita yetu dhidi ya moja ya gonjwa hatari zaidi itokomee kwa sababu tu ya kupambana na janga lingine.”

Surua ni ugonjwa ambao unaweza kuzuilika, lakini mafanikio yake yanahitaji asilimia 95 ya watoto wote wapatiwe chanjo kwa wakati, na chanjo hiyo ni dozi mbili dhidi ya surua ambazo ni  MCV1 na MCV2. Kwa sasa utoaji wa chanjo ya surua, MCV1 imekwama duniani kote kwa zaidiya muongo mmoja na kiwango cha utoaji ni kati ya asilimia 84 na 85, ilhali utoaji wa chanjo dhidi ya surua, MCV2 umekuwa ukiongezeka lakini ni kwa asilimia 71 pekee.

Natasha Crowcroft, mshauri mwandamizi wa kiufundi kuhusu ugonjwa wa surua na rubella, WHO amesema habari njema ni kwamba chanjo dhidi ya surua zimeokoa maisha ya zaidi ya watu milioni 25.5 duniani kote tangu mwaka 2000. Lakini kiwango kidogo ufikiaji wahusika kinamaanisha kwamba idadi ya watoto wasio na kinga ilikuwa inaongezeka kila mwaka.

Tarehe 24 Aprili 2017, mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya surua huko kambini Beerta Muuri mjini Baidoa nchini Somalia.
UNICEF/Yasin Mohamed Hersi
Tarehe 24 Aprili 2017, mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya surua huko kambini Beerta Muuri mjini Baidoa nchini Somalia.

Mkwamo wa utoaji chanjo

 “Suala kubwa siyo eneo kubwa lisilokuwa na huduma ya chanjo, bali ni mkwamo wa utoaji wa chanjo hiyo,” amesema Dkt. Crowcroft wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi.
 “Ni kama vile, unajua, kuwasha moto kwenye msitu, inafika wakati unalipuka. Na ndivyo ilikuwa mwaka 2019, ambako milipuko ilishamiri kwenye maeneo ambayo hayakuwa na kampeni za kutosha za chanjo kwa miaka kadhaa,” amesema Dkt. Crowcroft.

Ameongeza kuwa iwapo una kiwango cha utoaji wa chanjo cha asilimia 80, basi unatambua kuwa kila kitu kiko sawa lakini si kweli na kisha milipuko inaibuka.

Kusitasita kutoa chanjo

Mifumo dhaifu ya afya na kushindwa kufikia watoto ili kuwapatia chanjo ndio tatizo kubwa duniani kote na suala la watu kusita kupatia chanjo watoto wao, ni tatizo la ziada katika baadhi ya nchi.

Wiki iliyopita, UNICEF na WHO walitoa wito wa pamoja wa kuepusha milipuko ya surua na polio, wakitaka nyongeza ya dola milioni 255 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kushughulikia pengo la ukosefu wa kinga dhidi ya surua katika mataifa 45 yaliyo hatarini zaidi kupata milipuko.

Mataifa ambayo hivi karibuni yamekumbwa na milipuko mikubwa ya surua ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Madagascar, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Georgia, Kazakhstan, Macedonia Kaskazini, Samoa, Tonga na Ukraine.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter