Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fedha ndio mtihani mkubwa kwa nchi kukabiliana na afya na mabadiliko ya tabianchi:WHO

Wahudumu wa afya nchini Iran wakiangalia vifaa vya matibabu huku nchi hiyo ikiendelea kupambana na virusi vya corona.
WHO/Iran
Wahudumu wa afya nchini Iran wakiangalia vifaa vya matibabu huku nchi hiyo ikiendelea kupambana na virusi vya corona.

Fedha ndio mtihani mkubwa kwa nchi kukabiliana na afya na mabadiliko ya tabianchi:WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO leo limesema nchi nyingi zimeanza kuweka kipaumbele cha afya katika juhudi zao za kuwalinda watu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini ni takriban robo tu ya wale waliofanyiwa utafiti hivi karibuni na Shirika hilo wameweza kutekeleza kikamilifu mipango au mikakati yao ya kitaifa ya afya na mabadiliko ya tabianchi.

Nchi zinaripoti kwamba ukosefu wa fedha, athari za COVID-19, na uhaba wa rasilimali watu ni vikwazo vikubwa vya maendeleo. 

Ripoti hiyo ya WHO ya utafiti wa afya na mabadiliko ya tabianchi ya mwaka 2021 imegundua kuwa zaidi ya robo tatu ya nchi zilizofanyiwa utafiti zimeendeleza au ziko katika mchakato wa kuendeleza mipango au mikakati ya kitaifa ya afya na mabadiliko ya tabianchi. 

Asilimia 85% ya nchi sasa zina kitengo maalum cha kuzingatia afya na mabadiliko ya tabianchi ndani ya wizara zao za afya. 

Athari za COVID-19 kwa afya na rasilimali kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi  

Kwa ujumla, uchunguzi wa WHO unaonesha kuwa uhaba wa fedha unasalia kuwa kikwazo kikuu cha utekelezaji kamili wa mipango ya kitaifa ya afya na mabadiliko ya tabianchi, iliyotajwa na asilimia 70% ya nchi ikilinganishwa na asilimia 56% mwaka wa 2019.

Kikwazo cha pili muhimu zaidi ni rasilimali watu, wakati karibu theluthi moja ya nchi zilibainisha ukosefu wa ushirikiano kati ya sekta kama kikwazo kikuu. 

Takriban nusu ya nchi zinaripoti kuwa dharura ya COVID-19 imepunguza maendeleo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuelekeza wafanyikazi wa afya na rasilimali kwa janga hilo, na linaendelea kutishia uwezo wa mamlaka ya afya ya kitaifa kupanga na kulidhibiti na kujiandaa kwashinikizo na mishtuko ya kiafya inayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi. 

"Utafiti huo mpya wa WHO unaangazia jinsi nchi nyingi ambavyo haziungwi mkono na haziko tayari kukabiliana na athari za kiafya za mabadiliko ya tabianchi. Tuko hapa COP26 kuhimiza ulimwengu kusaidia vyema nchi zilizo na uhitaji na kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunafanya kazi bora zaidi kulinda idadi ya watu dhidi ya tishio kubwa la afya ya binadamu ambalo tunakabiliana nalo leo, "amesema Dkt. Maria Neira, mkurugenzi wa idara ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na afya katika shirika la WHO. 

Bibi anapata chanjo ya COVID-19 katika hospitali ya Kathmandu, Nepal.
© WHO/Blink Media/Uma Bista
Bibi anapata chanjo ya COVID-19 katika hospitali ya Kathmandu, Nepal.

Kuondoa vikwazo vinavyozuia nchi kutekeleza mipango yao 

Duniani kote zaidi ya karibu theluthi mbili ya nchi zilizofanyiwa utafiti zimefanya tathmini ya hatari na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na afya au ziko katika mchakato wa kufanya hivyo, wakati karibu nchi zote asilimia 94% zinajumuisha masuala ya afya katika michango yao iliyoamuliwa kitaifa (NDCs) kwenye  mkataba wa Paris. 

"Hoja za kiafya za kutaka kuongezwa kwa hatua za mabadiliko ya tabianchi ziko bayana. Kwa mfano, karibu asilimia 80% ya vifo vinavyosababishwa na uchafuzi wa hewa vinaweza kuepukwa ikiwa viwango vya sasa vya uchafuzi wa hewa vitarejeshwa kwa miongozo ya ubora wa hewa vya WHO, "ameongeza Dkt Neira. 
Leo hii, "Changamoto sasa ni kuondoa vikwazo vinavyozuia nchi kukamilisha na kutekeleza mipango," amehitimisha Tara Neville, afisa wa kiufundi katika idara ya mazingira na afya wa WHO na pia mwandishi mkuu wa ripoti hiyo.