Tukiadhimisha siku ya miji tudhibiti hatari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga mnepo:UN 

Cap Haitien mji ulio pani ya Kaskazini ya Haiti kabla ya machafuko ya sasa ya kisiasa
MINUJUSTH/Leonora Baumann
Cap Haitien mji ulio pani ya Kaskazini ya Haiti kabla ya machafuko ya sasa ya kisiasa

Tukiadhimisha siku ya miji tudhibiti hatari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga mnepo:UN 

Tabianchi na mazingira

Leo ni siku ya miji duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mastaifa amesema ingawa kupanda kwa kina cha bahari kunaweza kuweka zaidi ya watu milioni 800 katika miji ya pwani kwenye hatari ya moja kwa moja ifikapo mwaka 2050, chini ya asilimia 10 ya fedha za mabadiliko ya tabianchi kwa maeneo ya mijini zinakwenda katika hatua za kukabiliana na kujenga mnepo. 

Katika ujumbe wake kwa siku inayoadhimishwa kila mwaka Oktoba 31Antonio Guterres , ametoa wito wa azimio jipya la kukabiliana na changamoto za mijini, kupunguza hatari na kubuni suluhu za kudumu. 

Kauli mbiu ya mwaka huu inaangazia “Kurekebisha miji kwa kustahimili mabadiliko ya tabianchi” 

Vituo vya ubunifu 

"Miji ni vitovu vya uvumbuzi na ustadi wa kibinadamu na vituo vya uwezekano wa hatua za mageuzi ili kutekeleza malengo ya maendeleo Endelevu (SDGs) na kujenga ulimwengu usio na hewa ukaa, unaostahimili mabadiliko ya tabianchi na haki ya kijamii," amesema Bw. Guterres. 

Hata hivyo, alibainisha kuwa zaidi ya watu bilioni moja sasa wanaishi katika makazi yasiyo rasmi, huku asilimia 70 wakiwa katika hatari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi. 

Hivi sasa, ni asilimia tisa tu ya fedha za mabadiliko ya tabianchi kwa miji zimetengwa kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo na kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko hayo huku miji katika nchi zinazoendelea, ikipokea kiasi kidogo sana kuliko wenzao nchi tajiri zaidi. 

Kuhimili na kulinda 

Bw. Guterres amesema hili lazima libadilike, na akasisitiza ombi lake la muda mrefu la kutaka nusu ya fedha zote za mabadiliko ya tabianchi zitumike katika kukabiliana na hali hiyo. 

"Tunahitaji mtazamo unaozingatia watu na jumuishi katika kupanga, kujenga na kusimamia miji," ameongeza. "Miundombinu thabiti, mifumo ya tahadhari ya mapema na zana za kifedha ili kupunguza hatari, ni nyenzo muhimu kama miji iantaka kuwa na mnepo na uwezo wa kuishi na maisha ya wakaazi wao." 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kusema kuwa miji imekuwa vitovu vya janga la COVID-19 na iko kwenye mstari wa mbele wa janga la mabadiliko ya tabianchi, lakini inaweza kuongoza njia ya kujikwamua kutoka kwa janga hili, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, na kupata mustakabali bora kwa mabilioni ya watu.