Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukweli ulio wazi ni kwamba dunia inaelekea kwenye zahma ya mabadiliko ya tabianchi:Guterres

Senegal ni moja kati ya nchi 6 zilizoathirika na ukame mkali mwaka huu
UNOCHA/Eve Sabbagh
Senegal ni moja kati ya nchi 6 zilizoathirika na ukame mkali mwaka huu

Ukweli ulio wazi ni kwamba dunia inaelekea kwenye zahma ya mabadiliko ya tabianchi:Guterres

Tabianchi na mazingira

Tuko katika wakati muhimu kwa sayari yetu. Lakini wacha tuwe wazi  kuna hatari kubwa ambayo mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Glasgow unaweza usizai matunda, ameonya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo akizungumza na waandishi wa Habari mjini Roma Italia kunakofanyika mkutano wa mataifa 20 yaliyoendelea kiuchumi duniani au G-20.

Guterres amesea “matangazo kadhaa ya hivi karibuni ya mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuwa yanatoa taswira mwanana, lakini kwa bahati mbayá, hii si hali halisi ni udanganyifu.”

Amekumbusha kwamba michango ya sasa iliyoamuliwa kitaifa ambayo ni ahadi rasmi za serikali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi bado inaiadhibu dunia kwa ongezeko mbaya lajoto la nyuzijoto 2.7C.

“Hata kama ahadi za hivi majuzi zilikuwa wazi na za kuaminika na kuna maswali mazito kuhusu baadhi yao bado tunaelekea katika janga la mabadiliko ya tabianchi. Hata katika hali bora zaidi, joto bado litapanda zaidi ya nyuzi joto mbili. Hiyo ni zahma”.Amesisitiza Guterres

Tunahitaji hamasa na vitendo zaidi

Katibu Mkuu amesema “Ikiwa tunataka mafanikio ya kweli  na sio maneno tu basi tunahitaji tamaa zaidi na hatua zaidi. Hilo litawezekana tu kwa uhamasishaji mkubwa wa utashi wa kisiasa. Na hilo linahitaji uaminifu miongoni mwa wahusika wakuu. Leo, uaminifu ni mdogo na kuna maswali mazito ya uaminifu.”
  
Ameongeza kuwa dunia inashuhudia viwango vya hatari vya kutoaminiana miongoni mwa mataifa makubwa, miongoni mwa wanachama wa G20, kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea zikiwemo nchi zinazoibukia kiuchumi.

Katika tarifa yake amesisitiza kuwa lengo muhimu zaidi la mkutano huu wa kilele wa G20 lazima liwe kurejesha uaminifu kwa kukabiliana na vyanzo vikuu vya kutoaminiana vinavyotokana na dhuluma, ukosefu wa usawa na migawanyiko ya kisiasa na kijiografia.

“Ombi langu kwa G20 ni kuchukua hatua madhubuti za pamoja kuziba pengo la uaminifu katika nyanja tatu.”
Mosi amesema ni usawa wa chanjo ambapo amesema amekuwa akizisukuma nchi za G20 kushika usukani wa kimataifa katika mipango ya chanjo kuweza kumfikia kila mtu kila mahali. Lakini mipango hiyo haikufanikiwa kwa sababu ya migawanyiko ya kisiasa na kijiografia.

Hivyo ametoa wito”Nazitaka nchi za G20 kusaidia kikamilifu mkakati huu na kuratibu hatua zao kwa ajili ya mafanikio. Hiyo ndio njia pakee ya kumaliza janga la COVID-19 kwa kila mtu kila mahali.”

Pili tofauti kubwa ya rasilimali kwa ajili ya kujikwamua na janga hili inamomonyoa uaminifu.

Mathalani amesema nchi za uchumi wa hali ya juu zinawekeza karibu asilimia 28 ya Pato lao la ndani katika kufufua uchumi, wakati kwa nchi za kipato cha kati, idadi hiyo inashuka hadi asilimia 6.5 na kwa nchi zenye maendeleo duni ni chini ya asilimia mbili ya kiasi kidogo zaidi.

Shirika la Fedha Duniani (IMF) linakadiria kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ukuaji wa jumla wa uchumi kwa kila mwananchi Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara utakuwa asilimia 75 chini kuliko mataifa mengine duniani.

Kujikwamua kunakuza ukosefu wa usawa na huku ni kinyume na maadili.

Hivyo amezitaka nchi za G20 kupanua wigo wa mpango wa kusimamisha madeni hadi mwaka ujao na kuufanya mkakati huo upatikane kwa nchi zilizo hatarini zaidi na zenye mapato ya kati ambazo zinaomba msaada.

Kwa kuzingatia mfumo wa pamoja wa kushughulikia madeni, pia tunahitaji mbinu ya msamaha wa madeni ambayo inafanya kazi na inapatikana kwa wote wanaohitaji na tuko mbali nayo. Nchi zisilazimishwe kuchagua kati ya kulipa madeni yao au kuwahudumia watu wao.
  
Tatu, uaminifu unadhoofishwa na ukosefu wa matarajio ya mabadiliko ya tabianchi katika kuyadhibiti, kukabiliana nayo na ufadhili wa fedha.

Tunahitaji matamanio zaidi ya kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi ili kutufikisha kwenye njia inayoaminika ya hadi nyuzi joto 1.5 C, lengo ambalo sayansi inatuambia ni mustakabali endelevu pekee wa dunia yetu.”

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba hili linahitaji hatua madhubuti sasa kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi duniani kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030. 

Nchi za G20 zina wajibu mahususi amesema wa kuweka lengo la nyuzijoto 1.5C kwani zinawakilisha karibu asilimia 80 ya hewa chafuzi duniani.

Kulingana na kanuni ya majukumu ya kawaida lakini tofauti kulingana na hali ya kitaifa, nchi zilizoendelea lazima ziongoze juhudi.

Tunahitaji juhudi katika kila nyanja

Matarajio ya kukabiliana na hali hiyo yanamaanisha wafadhili ikiwa ni pamoja na benki za maendeleo za kimataifa kutenga angalau nusu ya fedha zao za mabadiliko ya tabianchi ili kuyakabili na kujenga mnepo. 
Amesema G20 lazima iongoze msukumo mkubwa ili hili liwezekane kwani matarajio juu ya ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na kufanya vyema katika ahadi ya kutoa dola bilioni 100 kila mwaka kwa nchi zinazoendelea.

“Ninakaribisha juhudi zinazoongozwa na Canada na Ujerumani kusaidia kutufikisha huko. Ni hatua ya kwanza lakini imechelewesha kwa miaka mingi msaada mkubwa zaidi.” 

Guterres amesema kwa bahati mbaya, ujumbe kwa nchi zinazoendelea kimsingi ni huu: Hundi iko njiani kwenye barua. 

Amesisitiza kuwa “Wanasayansi wako wazi juu ya ukweli halisi, viongozi lazima wawe wazi katika matendo yao. Glasgow inaweza kuwa hatua ya mageuzi kuelekea ulimwengu salama na unaojali mazingira kwa watoto na wajukuu zetu. Hutujachelewa, lakini lazima tuchukue hatua sasa. Ninawasihi viongozi wa G20 waonyeshe mshikamano ambao watu wanataka na ulimwengu wetu unahitaji sana na hii inaanza kwa kujenga upya uaminifu na kwanza kabisa, miongoni mwa wanachama wao.”