Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano wa kimataifa wahitajika kufikia amani na usalama Afrika:UN

Mwanamke na watoto wake wakiume wakiwa wamesimama nje ya nyumba yao kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani huko Baboua, Jamhuri ya Afrika ya Kati -CAR
© UNICEF/Florent Vergnes
Mwanamke na watoto wake wakiume wakiwa wamesimama nje ya nyumba yao kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani huko Baboua, Jamhuri ya Afrika ya Kati -CAR

Mshikamano wa kimataifa wahitajika kufikia amani na usalama Afrika:UN

Amani na Usalama

Naibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo amesisitiza umuhimu wa amani na usalama barani Afrika, wakati akiwashukuru mabalozi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kusaidia Umoja wa Mataifa kuangazia suala hilo, na jinsi nchi zote wanachama zinavyoweza kufanya kazi na Muungano wa Afrika AU, kanda zingine na vikundi vya kanda, ili kufanya maisha kuwa salama zaidi katika bara zima.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Amina Mohammed ametoa angalizo kwa Baraza kuhusu "mienendo kadhaa ya wasiwasi" ambayo Waafrika wanakabiliana nayo leo.

Katika hotuba yake naibu Katibu Mkuu ameangazia mizigo ya kijamii na kiuchumi iliyoletwa na COVID-19, akisema haijaathiri tu utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) barani Afrika, lakini pia imezidisha umaskini, ukosefu wa usawa na vichochezi vyote vya migogoro.

"Limepunguza utoaji wa huduma za umma, kuvuruga minyororo ya ugavi, kupunguza shughuli za kiuchumi, na kukwamisha makubaliano ya amani na utatuzi wa migogoro", amesema.

Kuanzia kwenye mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan mapema wiki hii hadi kuendelea kwa vita katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia, na vitisho vinavyoendelea vya ugaidi na itikadi kali, amesema anashuhudia "kuongezeka kwa unyakuzi wa mamlaka kwa nguvu na kuongezeka kwa wanamgambo kote Afrika.”

Ushirikiano mpana zaidi

Amesema licha ya maendeleo haya ya kutisha, Waafrika wanaendelea kufanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya bara lenye ustawi, endelevu na la amani, kwa kuzingatia kanuni za kimataifa za haki za binadamu, kama inavyoshuhudiwa kutokana na kuongezeka kwa ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa, AU na mashirika ya kikanda juu ya uendelevu, mchakato wa maendeleo, uchaguzi na amani.

Bi Mohammed ametoa mfano wa Libya, ambapo Umoja wa Mataifa, AU, Umoja wa nchi za Kiarabu UAE, na Muungano wa Ulaya, wanajitahidi kuunga mkono makubaliano ya kusitisha mapigano na kujiandaa kwa uchaguzi ujao.

"Pia tunafanya kazi kwa karibu na AU na mashirika ya kikanda, kusaidia nchi za Sahel na kwingineko, ikiwa ni pamoja na kushughulikia kurejea kwa mamluki na wapiganaji wa kigeni katika nchi zao," amesema.

Usaidizi wa operasheni za UN

Operesheni maalum za kisiasa za Umoja wa Mataifa, operesheni za kulinda amani, na timu za nchi barani Afrika zinaendelea kutoa msaada wa kina kwa mipango mingine ya amani na mabadiliko ya kisiasa ikiwa ni pamoja na Cameroon, Mali, Somalia na Sudan Kusini.

Na mara baada ya majadiliano yanayoendelea kuhusu mgawanyo wa majukumu kati ya AU na Jumuiya za kiuchumi za kikanda na taratibu kukamilika, Bi. Mohammed amesema "anatarajia kuendelea kutumia fursa na nguvu za kila shirika na kujenga mikakati madhubuti ya kuzuia na kutatua migogoro kama janga la COVID-19  na mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuathiri bara hili, haswa wanawake na vijana."

Kukumbatia mshikamano wa kimataifa

Ushirikiano mkubwa wa Umoja wa Mataifa na AU na mashirika madogo ya kikanda lazima uungwe mkono na nchi wanachama wote.

Akinukuu Ajenda Yetu ya Pamoja, amesisitiza haja ya "kukumbatia tena mshikamano wa kimataifa" kutafuta njia mpya za kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya watu wote katika kila nchi.

Amezungumzia hatua tatu za dharura, akianza kwa kutanguliza mwitikio wa COVID-19 barani Afrika kupitia "hatua za haraka za usambazaji wa chanjo, kuimarisha mifumo ya afya ya kitaifa na uwekezaji unaohitajika sana katika kujitayarisha".

Naibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza tena "kuzingatia maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa, ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu na ajenda ya mwaka 2063 ya AU akisema ni "kiini cha juhudi zetu za pamoja".

Ameongeza kuwa "Hatimaye, maendeleo endelevu na shirikishi ni fursa yetu bora ya kushughulikia vyanzo vya migogoro na kufikia mustakabali wa amani na ustawi kwa wote".

Maendeleo endelevu na shirikishi ndiyo nafasi yetu bora ya kushughulikia vyanzo vya migogoro  amesisitiza naibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Fanyeni kila juhudi

"Kuendelea kupata rasilimali za kutosha, zinazotabirika, na endelevu ambazo zitaleta maendeleo ya maisha, amani na mamlaka ya usalama barani Afrika", ni hoja ya mwisho ya naibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Katika suala hili, ameangazia umuhimu wa hatua madhubuti katika amani, maendeleo na mbinu za kibinadamu, katika bara zima, "katika kuanzisha maono ya pamoja, katika kuhakikisha ushirikiano na ulinzi wa uwekezaji".

Chini ya mwongozo wa nchi wanachama, Bi. Mohammed amethibitisha kwamba Umoja wa Mataifa "utafanya juhudi zote kudumisha ushirikiano wetu kuwa na ufanisi zaidi ili kuwasaidia Waafrika wote kujenga bara lenye umoja, ustawi, ushirikiano na amani".

Afrika inaombi

Kwa niaba ya Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Rais wa Ghana, Nana Addo Dankwa Akufo-Addo, amehimiza ushirikiano wenye ufanisi zaidi kati ya Afrika na Umoja wa Mataifa akitoa wito wa kuwepo kwa mshikamano wa ngazi ya juu na uelewa zaidi wa vitisho vya sasa.

Pia amesisitiza haja ya wanawake na vijana zaidi kujumuishwa katika hatua zote za maamuzi na kutatua migogoro, ikiwa ni pamoja na kunyamazisha mtutu wa bunduki, na kutoa wito wa kuboreshwa changamoto za usalama, kama vile vitisho vinavyotokana na magaidi na shughuli za upinzani ambazo zinadhoofisha serikali zilizochaguliwa kidemokrasia.

Nadharia mbaya

Wakati Kenya ndio inayoshikilia wadhifa wa Urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu , Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo ameonya kwamba tofauti za kisiasa na simulizi potofu, ambazo zinaenea katika bara hilo, zimekuwa "zinatumiwa" hata katika nchi zenye demokrasia thabiti zaidi.

Pia alieleza kuwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa na AU unakabiliana na vitisho vya ugaidi vinavyozidi kuwa vya hali ya juu huku hatua za kimataifa zikipungukiwa katika nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa chanjo, na kuhimiza mazungumzo mapya kuhusumchakato wa usalama wa Afrika.

Utulivu wa kifedha

Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Mfuko wa ufadhili na amani wa Muungano  wa Afrika, Donald Kaberuka amesema hadi sasa, ushirikiano wa UN na AU, ukijumuisha usalama, umekuwa wa dharura na kusukuma Jumuiya hiyo kutathmini tena umuhimu wa kusaidia operesheni za amani za Afrika kupitia tathmini ya  michango.

Ametoa wito wa ufadhili zaidi unaotabirika kushughulikia dharura za amani na usalama pamoja na juhudi za muda mrefu za utulivu.