Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Athari za COVID-19 katika ajira ni mbaya kuliko zilivyotarajiwa:ILO

Mwanamke akifanyakazi katika kiwanja cha nguo nchini Lesotho
ILO/Marcel Crozet
Mwanamke akifanyakazi katika kiwanja cha nguo nchini Lesotho

Athari za COVID-19 katika ajira ni mbaya kuliko zilivyotarajiwa:ILO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ufufuaji wa ajira umekwama duniani kote na tofauti kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea zinatishia uchumi wa dunia nzima, llimeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani (ILO). 

Shirika hilo linakadiria kuwa saa za kimataifa watu walizofanya kazi mwaka huu zitakuwa asilimia 4.3 chini ya viwango vya kabla ya janga la COVID-19,ikiwa ni sawa na kazi za siku nzima milioni 125.  

Kwa mujibu wa shirika hilo haya ni masahihisho makubwa ya makadirio yaliyofanywa mwezi Juni, ya asilimia 3.5 au kazi milioni 100 za wakati wote. 

Toleo la nane la ripoti ya ILO ya tathimini ya : “COVID-19 na ulimwengu wa kazi” pia linaonya juu ya tofauti kubwa kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea, likisema kuwa zitaendelea bila msaada kamili wa kifedha na kiufundi. 

Tofauti za kikanda 

Katika robo ya tatu ya 2021, kwa mujibu wa UNDP jumla ya saa zilizofanywa kazi katika nchi zenye kipato cha juu zilikuwa chini kwa asilimia 3.6 kuliko robo ya nne ya 2019, kabla ya janga hilo kuanza. 

Kinyume chake, pengo katika nchi za kipato cha juu limesimama katika asilimia 5.7 na katika nchi za kipato cha chini kwa asilimia 7.3. 
Kwa mtazamo wa kikanda, Ulaya na Asia ya Kati zilipata hasara ndogo zaidi kwa saa, karibu asilimia 2.5. Hii ilifuatiwa na Asia na Pasifiki kwa asilimia 4.6. 
Afrika, Amerika na Mataifa ya Kiarabu yalionyesha kupungua kwa asilimia 5.6, 5.4 na 6.5 mtawalia. 

Tofauti hii kubwa inachangiwa kwa kiasi kikubwa na tofauti kubwa iliyopo katika uanzishaji wa chanjo na vichocheo vya  upatikanaji wa fedha. 

Makadirio yanaonesha kuwa kwa kila watu 14 waliopewa chanjo kamili katika robo ya pili ya 2021, kazi moja inayolingana ya muda wote iliongezwa kwenye soko la ajira la kimataifa. Hii kwa kiasi kikubwa imeleta ahueni. 

Kwa kukosekana kwa chanjo yoyote ile ulimwenguni, upotezaji wa saa zilizofanyiwa kazi ungesimama kwa asilimia sita katika robo ya pili ya 2021, badala ya asilimia 4.8 iliyorekodiwa. 

Kutokuwepo usawa katika utoaji chanjo, inamaanisha kuwa athari zilikuwa kubwa zaidi katika nchi zenye kipato cha juu, zisizofaa katika nchi za kipato cha kati na karibu alimia sifuri katika nchi za kipato cha chini. 

Kulingana na ILO pengo hili la usawa linaweza kushughulikiwa kwa haraka kupitia mshikamano mkubwa wa kimataifa kuhusiana na chanjo. 

Shirika hilo linakadiria kuwa ikiwa nchi zenye mapato ya chini zingekuwa na ufikiaji sawa wa chanjo, kujikwamua kwa saa za kazi kungewezesha kuzifikia nchi tajiri zaidi katika robo moja tu. 

Vichocheo vya fedha visivyo sawa 

Vichocheo vya kifedha viliendelea kuwa sababu nyingine muhimu katika njia za kujikwamua na janga la COVID-19 kiuchumi. Lakini, pengo hilo bado halijashughulikiwa, na karibu asilimia 86 ya hatua zote zimewekwa katika nchi zenye kipato cha juu. 

Kwa wastani, ongezeko la vichocheo vya fedha vya asilimia moja ya pato la taifa la kila mwaka viliongeza saa za kazi za kila mwaka kwa asilimia 0.3 ikilinganishwa na robo ya mwisho ya mwaka 2019. 

Janga hilo pia limeathiri uzalishaji, na kusababisha tofauti kubwa zaidi. Pengo la uzalishaji kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea linakadiriwa kuongezeka hadi kiwango cha juu zaidi tangu 2005. 

Mkurugenzi mkuu wa ILO, Guy Ryder, ameangazia usambazaji usio sawa wa chanjo na uwezo wa kifedha akisema kwamba "yote mawili yanahitaji kushughulikiwa haraka." 

Amesema katika wito wa kimataifa wa kuchukua hatua kwa ajili ya kujikwamua na COVID-19 unaolenga binadamu, mwelekeo uliyopitishwa mwaka jana na mkutano wa kimataifa wa wafanyakazi ambao unazitaka nchi kuhakikisha kwamba ahueni yao ni jumuishi, endelevu na yenye mnepo. 

"Ni wakati wa kutekeleza mwelekeo huu, ambao unaenda sanjari na kuunga mkono ajenda ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na vichocheo vyake vya kuharakisha fursa za kazi na ulinzi wa Jamii," amesema Bwana Ryder.